NA DIRAMAKINI
ZIKIWA zimepita siku kadhaa baada ya Halmashauri ya Wilaya ya Uyui mkoani Tabora kuwasimamisha kazi watumishi wawili wa kada ya afya baada ya kutoleana lugha zisizofaa wakiwa kazini na kusambazwa katika mitandoa ya jamii jambo ambalo ni kinyume na sheria za utumishi wa umma, bado sakata hilo limeonekana kuacha maswali mengi.
Awali akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake,Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Uyui mkoani Tabora, Dkt.Kija Maige amesema kwamba tukio hilo lilitokea Januari 6, mwaka huu katika Zahanati ya Ishilimulwa Kata ya Bukumbi wilayani humo. VIDEO YA MPYA HAPA CHINI
Dkt.Maige aliwataja watumishi hao kuwa ni Rose Shirima ambaye ni muuguzi mkunga na James Chuchu Mteknolojia wa maabara ambao walikuwa wakibishana na kutoleana lugha zisizofaa kazini hali iliyosababisha taaruki kwa umma.
Dkt.Maige amesema, watumishi hao watapumzishwa kutekeleza majukumu yao ya utoaji wa huduma za afya ili kupisha uchunguzi kwa mujibu wa kanuni 37 ya kanuni za utumishi wa umma ya mwaka 2003.
Amesema kwamba, uchunguzi huo utashirikisha mabaraza ya kitaaluma ambayo ni Baraza la Waunguzi Tanzania na Baraza la Wataalam wa Maabara Tanzania ambapo hatua zaidi zitafuata baada ya kukamilika kwa uchunguzi huo.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Uyui, Dkt. Wendy Robert amesema kuwa, mabishano hayo yalionekana mtandaoni na kusababisha taharuki kubwa kwa wananchi na kusema tayari uchunguzi umeanza kufanyika ili kujua chanzo cha mabishano hayo.
Amesema, mabishano hayo yalitokana na mtaalam wa maabara kugomea kutumia kipimo cha malaria kwa ajili ya kinamama wajawazito kwa madai kilikuwa kimekwisha muda wake jambo ambalo si sahihi.
“Vitendanishi hivyo vinamalizika muda wake wa matumizi Aprili 14, mwaka huu jambo ambalo bado kipimo hicho kinafaa kwa ajili ya kupimia wajawazito kujua wingi wa wadudu wa malaria,”amesema Dkt.Wendy .
Amesema kwamba, kipimo hicho cha malaria chenye namba ya utambuzi iliyosajiwa ni 05EDG025B
Naye Mkuu wa Divisheni ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu Wilaya ya Uyui, Hamis Mpume amesema kuwa, watumishi hao watasimama kazi kwa ajili ya kupisha uchunguzi wa tuhuma kwa kuzingatia kanuni na sheria.
Wakati huo huo, kupitia taarifa iliyotolewa na Chama cha Wauguzi Tanzania (TANNA) Januari 12 imesema kabla ya kuanza kurekodiwa kwa video hiyo, kulikuwepo na lugha za matusi zinazodaiwa kutolewa na James Chuchu kwa Rose Shirima hali iliyofanya muuguzi huyo naye kumjibu kwa lugha isiyo na staha bila ya kufahamu kuwa anarekodiwa.
“Hakuna vitendanishi vyovyote vilivyoisha muda wake ambavyo vilikuwa vinatumika katika kituo hicho kama ilivyokuwa inaelezwa na mtekinolojia wa maabara, isipokuwa vitendanishi vilivyopo vinakaribia kuisha muda wake yaani bado vina miezi 3 mbele.
“Hivyo alichokuwa anasimamia muuguzi kilikuwa sahihi kwa kufuata utaratibu wa mfumo wa udhibiti bidhaa lakini pia alikuwa akisimamia maamuzi ya kikao chao cha ndani,” imesema taarifa ya TANNA.
Kupitia taarifa hiyo, TANNA imelaani tukio la kurekodiwa kwa mtumishi huyo kwa kile kilichodai ndani yake kuna chembechembe za udhalilishaji wa utu na unyanyasaji wa kijinsia.
“Tunatumia fursa hii kuwakumbusha watumishi wa Afya na pia kuanzisha na kuimarisha kamati za maadili kuanzia ngazi ya kituo.
“Hii itasaidia kutatua matatizo ya kitaaluma katika ngazi ya kituo na kwa wakati, ili kuzuia matukio yanayoweza kutoa taharuki katika jamii lakini pia kulinda heshima ya taaluma zetu,” imebainishwa kwenye taarifa hiyo.
TANNA imesema, kinaungana na Serikali kusisitiza watumishi kufanya kazi kwa uadilifu na weledi kwa kuzingatia maadili ya Utumishi wa Umma na taaluma husika katika kutekeleza majukumu ya kila siku.
TANNA pia imeishauri Serikali kuongeza ajira za kada ya Afya ili kumpunguzia muuguzi kazi zisizomuhusu.
“Mara nyingi wauguzi wamekuwa wakifanya kazi nyingi hata zisizo za taaluma yao ili mradi kuhakikisha wananchi wanapata huduma wanayoitarajia, lakini hali hiyo kwa namna moja ama nyingine inaathiri utendaji wao katika shughuli za uuguzi na ukunga kwa ufanisi.” VIDEO YA AWALI ILIYOSAMBAA HAPA CHINI
Pia imeishauri Serikali na taasisi binafsi za afya kuajiri kampuni au watu wataoshughulika na usafi wa vituo hospitali ili muuguzi anapoingia kazini akili yake iwe kwa mgonjwa pekee kuepuka kadhia za namna hiyo.