Walionaswa na TAKUKURU wakimshawishi Askari amwachie ndugu yao aliyekamatwa na bangi wahukumiwa jela Kigamboni

NA DIRAMAKINI

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke jijini Dar es Salaam imewakamata Hamis Abdul Hamis na Abdalah Hamis Ngaoma wakazi wa Maweni Kigamboni jijini Dar es Salaam kwa tuhuma za kushawishi kisha kutoa rushwa kwa Askari Polisi DC Hamis Masana wa Kituo cha Polisi Kigamboni.

Holle Makungu ambaye ni Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke ameyabainisha hayo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo amesema,kitendo hicho ni kinyume cha kifungu cha 15 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11/2007.

"Awali tulipokea taarifa mnamo Januari 23, 2023 kuwa kuna wananchi wanamshawishi Askari Polisi huyo wa Kituo cha Polisi Kigamboni kutaka kumpatia kiasi cha shilingi laki nane ili aweze kumwachia huru ndugu yao aliyekamatwa kwa tuhuma za kukutwa na kiasi kikubwa cha bangi.

"Tuliifanyia kazi taarifa hii kupitia timu yetu ya Kigamboni na baada ya kujiridhisha, mtego uliandaliwa na kuweza kuwanasa Hamis Abdul Hamis na Abdalah Hamis Ngaoma wakati wakitoa rushwa hiyo.

"Watuhumiwa walifikishwa katika Mahakama ya Wilaya Kigamboni na Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU Evelyn Daimon tarehe 25/01/2023 na kufunguliwa Shauri la Jinai namba CC.8/2023 mbele ya Hakimu wa Mahakama hiyo Mhe. Is-haq Bakari Kuppa.

"Wote wawili walikiri makosa yao ambapo Abdalah Hamis Ngoma alihukumiwa kwenda jela miaka mitatu au kulipa faini ya shilingi laki sita na Hamis Abdul Hamis alihukumiwa kwenda jela miaka mitatu au kulipa faini ya shilingi laki tatu kwa kosa la kushawishi.

"Washtakiwa wote walipelekwa kuanza kutumikia kifungo baada ya kushindwa kulipa faini. Aidha shilingi laki nane za rushwa iliamuliwa kuingizwa Serikalini kupitia Idara ya Mahakama,"amefafanua.

Wakati huo huo, Holle Makungu ambaye ni Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke amenatoa rai kwa watumishi wote wa umma kuiga alichokifanya askari huyo, kwani tafiti zinaonyesha kuwa watoa hongo au rushwa ni wengi ila taarifa hazitolewi.

"Kwa kuwa baadhi ya watumishi wenye dhamana tumekuwa wabinafsi kwa kupenda kujineemesha wenyewe kwa kupokea fedha tusizo stahili na kujisahaulisha viapo vyetu vya uadilifu.

"Nitumie nafasi hii kutoa onyo kwa wananchi wenye fikra za kutoa rushwa kwa watumishi wa umma kuwa, kutoa rushwa ni kosa chini ya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11/2007 na hivyo tutaendelea kuwakamata wale wote wanaotoa sawa na tunavyowakamata wanaopokea.Kuzuai rushwa ni jukumu lako na langu, tutimize wajibu wetu,"amefafanua.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news