NA MUNIR SHEMWETA-WANMM
WAZIRI wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Dkt.Angeline Mabula ametaka kutolewa mafunzo ya maadili kwa Mawakala wa Mali Zisizohamishika (madalali).
Dkt.Mabula amesema hayo Januari 30, 2023 wakati akifungua mafunzo ya muda mfupi ya Mawakala wa Mali Zisizohamishika (MADALALI) yanayoendeshwa na Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) kwa kushirikiana na Chama cha Mawakala wa Mali Zisizohamishika (AREA) yanayofanyika jijini Dar es Salaam.
Amesema, pamoja na mafunzo yanayotolewa kuwa ya kitaalamu zaidi, lakini upo umuhimu mkubwa wa kutolewa mafunzo yanayohusu maadili kwa kuwa eneo hilo limekuwa likisababisha malalamiko mengi kwa jamii.
Kwa mujibu wa Dkt.Mabula, wapo madalali wanaolalamikiwa kufanya vitendo vya utapeli ambapo huwadanganya wateja na kusababisha wateja hao kununua viwanja huku wakijua fika kuwa viwanja hivyo ni mali ya watu wengine na mwisho wa siku hujipatia fedha isivyo halali.
Amebainisha kuwa, katika baadhi ya nchi zikiwemo Kenya na Afrika Kusini fani ya madalali inaheshimika na kuthaminiwa kwa kuwa imewekewa utaratibu wa usimamaizi na hivyo masuala ya uadilifu na weledi yanazingatiwa na kusimamiwa ipasavyo.
Amesema, Kenya inayo sheria ya usajili wa mawakala inayojulikana kama Estate Agents Act ya mwaka 1984 iliyorekebishwa mwaka 2012 huku Afirika Kusini ikiwa na Sheria ya Property Practitioners Act ya mwaka 2019 iliyounda mamlaka ya usimamaizi wa wataalamu wa masuala ya milki wakiwemo mawakala wa usimamizi wa mali zisizohamishika.
Amekipongeza Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) pamoja na Chama cha Mawakala wa Mali Zisizohamishika (AREA) kwa kubuni mpango wa mafunzo unaoelenga kuhakikisha kuwa fani ya uwakala wa mali zisizohamishika inaendeshwa kitaalamu.
Amesema, wizara yake iatatoa ushirikiano mkubwa ili kuhakikisha fani ya mwakala inaboreshwa ili shughuli za mawakala wa mali zisizohamishika ziweze kuanyuka kwa ufanisi na tija.
Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala wa Mali Zisizohamishika (AREA), Erick Rweikiza amesema, dhamira ya chama chake ni kuweka mazingira bora ya kuelimisha wanachama juu ya taaluma na kujenga umoja wa kibiashara pamoja na kutetea maslahi ya wanachama ili kuweka mazingira bora kwa wapangishaji, wauzaji na wanunuzi aliowaeleza kuwa ndiyo waajiri wa mawakala.
‘’Nia ni kuwafundisha wasio na ajira kujiajiri kupitia taaluma ya mawakala wa mali zisizohamishika,’’ amesema Rweikiza.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Bishara (CBE), Prof. Edda Lwoga amesema, elimu inayotolewa na chuo chake kwa mawakala inatolewa chini ya mpango kabambe wa kuwafikia vijana wa kitanzania na kurasimisha shughuli zisizo rasmi zinazofanywa na jamii kubwa ya watanzania.
‘’Katika kutambua juhudi za serikali kwenye mpango wa kurasimisha taaluma ikiwa ni pamoja na kusajili mawakala sisi kama chuo tumejidhatiti na tuko tayari kushirikiana na serikali kwenye mchakato ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kuhakikisha watendaji wana viwango vinavyokubalika kabla ya kuajiriwa,"amesema Profesa Edda Lwoga.