NA MWANDISHI WETU
WATUMISHI wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wamepongezwa kutokana na jitihada kubwa za kukuza diplomasia ya uchumi zilizofanyika mwaka 2022.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akizungumza wakati wa mkutano wake wa kwanza na Watumishi wa Wizara hiyo tangu kuteuliwa kwake kwenye wadhifa huo mwezi Oktoba 2022.(Picha na Wizara ya Mambo ya Nje).
Hayo yamesemwa Januari 6,2023 jijini Dodoma na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Lawrence Tax (Mb) wakati wa kikao chake cha kwanza na watumishi wa wizara tangu ateuliwe kushika wadhifa huo mwezi Oktoba 2022.
Maeneo ambayo Mhe.Waziri Dkt. Tax ameyataja kuwa wizara imeyaratibu kwa ufanisi unaoridhisha ni pamoja na ziara za viongozi wa kitaifa nje ya nchi, ushiriki wa viongozi katika mikutano ya kikanda na kimataifa, na uandaaji wa mikutano ya Tume za Kudumu za Pamoja za Ushirikiano (JPCs).
Amesema, majukumu hayo ambayo sio mepesi kuyatekeleza, yamekuwa na manufaa makubwa nchini katika nyanja za kidiplomasia na uchumi.
Dkt.Tax amewasihi watumishi kuendeleza jitihada hizo huku wakizingatia weledi, uzalendo na uadilifu katika kusimamia maslahi ya Taifa wakati wa utekelezaji wa majukumu kwenye majukwaa ya kikanda na kimataifa.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akiwa na Naibu Katibu Mkuu, Balozi Fatma Rajab wakati wa mkutano kati ya Mhe. Dkt. Tax na watumishi wa wizara hiyo.
Ameongeza kuwa, watumishi hawana budi kuboresha utendaji kazi ili wakidhi matarajio ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe.Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambayo pamoja na mambo mengine, inalenga kuboresha uhusiano wa kikanda na kimataifa kwa faida za kiuchumi na kisiasa.
Mhe. Waziri amewasihi watumishi wote kuzingatia masuala ya kisheria, kikanuni, miongozo, na miiko iliyowekwa wakati wanatekeleza majukumu yao.
Mkurugezni wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, Bw. Alex Mfungo akizungumza wakati wa mkutano na Watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Waziri Dkt.Tax.
Masuala hayo ni pamoja na kulinda Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kutambua mipaka ya majukumu yao na kutunza siri, kukamilisha maboresho ya Sera ya Mambo ya Nje ya Mwaka 2001 kwa wakati ili iakisi mabadiliko na maendeleo yanayotokea duniani hivi sasa.
Pia kubuni mfumo wa ufuatiliaji utakaokuwa na uwezo wa kupima utendaji wa wizara na wa mtumishi mmoja mmoja, kufanya kazi kwa ushirikiano katika idara na vitengo, idara na idara hadi uongozi mzima wa wizara.
Masuala mengine ni kufanya kazi kwa weledi, kujituma na uzalendo ili kuondokana na kasumba ya kufanya kazi kwa mazoea, utunzaji wa kumbukumbu ambao ni jambo muhimu kwenye mwendelezo wa utekelezaji wa majukumu ya wizara.
Kuimarisha mawasiliano ndani ya wizara, ofisi za Balozi, taasisi zilizo chini ya wizara na wadau wengine, kuendelea na matumizi mazuri ya rasilimali fedha ambayo yamefanya wizara kupata Hati Safi katika Miaka ya Fedha 2019/2020 na 2020/2021 na kuongeza kasi katika kutekeleza miradi ya maendeleo, hususani ujenzi na ukarabati wa ofisi za Balozi.
Awali, wakati anasoma taarifa kuhusu utendaji wa wizara hiyo, Katibu Mkuu, Balozi Joseph Sokoine alieleza hatua mbalimbali ambazo wizara inazichukua ili kuboresha utendaji wa majukumu ya Wizara. Hatua hizo ni pamoja na ununuzi wa vitendea kazi, uboreshaji wa maslahi ya watumishi, mafunzo ya muda mrefu na mfupi kwa watumishi na kuboresha muundo wa utumishi nje ya nchi.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Naibu Waziri, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb), Naibu Katibu Mkuu, Balozi Fatma Rajab, watumishi wa wizara na taasisi zilizo chini ya wizara.