Waziri Dkt.Tax ateta na Balozi wa India, Korea, bosi wa Huawei Tanzania

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax amekutana kwa mazungumzo kwa nyakati tofauti na wageni kadhaa waliomtembelea ofisini kwake Mtumba jijini Dodoma.
Wageni hao ni Balozi wa India nchini, Mhe Binaya Pradhan, Balozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea, Mhe. Kim Young Su na Naibu Mkurugenzi wa Kampuni ya Huawei Tanzania Bw. Tao Mian.

Akizungumza na Balozi wa India nchini Mhe. Dkt. Tax amemshukuru Balozi huyo kwa kutenga muda wa kumtembelea kwa mara ya kwanza tangu ateuliwe kwenye wadhifa huo na kueleza kwamba ziara hiyo itamwezesha kuelewa kwa kina hatua mbalimbali zilizofikiwa katika ushirikiano kati ya Tanzania na India na pia kubadilishana mawazo ya namna ya kufanikisha masuala mbalimbali yaliyokubalika katika ushirikiano baina ya nchi hizi mbili.

Amesema Tanzania na India zinashirikiana katika Sekta mbalimbali zenye umuhimu kwa wananchi ikiwemo Sekta ya maji, elimu, teknolojia na afya na kwamba ni wakati sasa kwa nchi hizi mbili kuendelea kutekeleza kwa kasi makubaliano mbalimbali ambayo tayari yamefikiwa ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

“Ushirikiano wetu unaenda vizuri na mambo tunayokubaliana kushirikiana na kufanyia kazi kwa pamoja yanaenda, zaidi tuongeze kasi kuyatekeleza. Niwahakikishie kuwa tutaaendelea kushirikiana ili kuendeleza uhusiano wetu ambao ni wa kidugu na kihistoria, ambao umekuwepo kwa miaka mingi,” amesema Dkt.Tax.

Naye Balozi wa India Mhe. Binaya Pradhan ameeleza kuridhishwa kwake na ushirikiano anaoupata nchini katika kutekeleza majukumu yake na kueleza kwamba Serikali ya India kupitia Hospitali ya Apolo wamekubali kushirikiana na Hospitali ya Muhimbili kupitia Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Hospitali ya Bugando ya jijini Mwanza na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road ya jijini Dar es Salaam katika kutoa huduma na kuwajengea uwezo watumishi katika hospitali hizo ili kusaidia wananchi wa Tanzania.

Kuhusu sekta ya elimu, Balozi huyo amesema wamekuwa wakishirikiana na Chuo cha Teknolojia cha Dar es Salaam (DIT) katika kukiboresha ili kukiwezesha kuwa Kituo bora cha utoaji wa huduma za teknolojia ya habari na mawasiliano nchini.
Akizungumza na Balozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea Mhe. Dkt. Tax amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na nchi hiyo katika sekta kama kilimo, elimu afya na teknolojia ya habari na mawasiliano.

Kwa upande wake, Balozi Kim Young Su amempongeza Mhe. Dkt. Tax kwa kuteuliwa kwenye wadhifa huo ikiwa ni mara yake ya kwanza kukutana naye na kumwahidi ushirikiano. Pia amesema kuwa, Nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika sekta mbalimbali.
Akizungumza na Naibu Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Huawei Tanzania Mhe. Tax ameipongeza kampuni hiyo kwa uwekezaji wao katika masuala ya Teknolojia hususan kupitia mradi wao wa kusambaza huduma za kidigitali vijijini.

“Huawei ni kampuni kubwa na tunathamini uwepo wenu hapa nchini. Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ni mingoni mwa vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hivyo tutaendelea kushirikiana nanyi hususan kwenye kusambaza huduma za kidigitali vijijini na vyuoni ili hatimaye tuweze kufikia ndoto yetu ya kuwa kitovu cha kidigitali,”amesema Mhe. Dkt. Tax.

Kwa upande wake, Bw. Tao Mian alieleza kwamba hapa nchini Kampuni hiyo imetengeneza ajira zaidi ya 1000 ambapo zaidi ya asilimia 70 ya ajira ni za watanzania.Kadhalika Kampuni hiyo inashirikiana na zaidi ya kampuni 70 za ndani, Wahandisi wa TEHAMA zaidi ya 2000 nchi nzima pamoja na vyuo zaidi ya 19 nchini. Aidha, Kampuni hiyo inaendesha mafunzo ya TEHAMA kwa zaidi ya wanafunzi 2000, kuhudumia zaidi ya asilimia 75 ya watanzania na kwamba imekuwa mchangiaji mkubwa wa ujenzi wa miundombinu ya TEHAMA nchini.

“Tunaridhishwa na uungwaji mkono wa Kampuni yetu hapa Tanzania na tunaahidi kuendelea kuchapa kazi ili kuhakikisha huduma za kidigitali zinawafikia wananchi wengi kwa wakati mmoja hususan wale wa vijijini” alisema Bw. Mian.

Pia alimueleza Mhe. Dkt.Tax juu ya mpango kabambe wa kuboresha mawasiliano ya TEHAMA vijijini ambao ni sehemu ya Mkataba wa ushirikiano uliosainiwa baina ya Tanzania na China ambao unatarajiwa kutekelezwa na Kampuni hiyo. 

Katika mradi huo kutakuwa na jumla ya miradi 19 ya kipaumbele, uboreshaji wa mawasiliano vijijini, usambazaji wa umeme Kaskazini Mashariki mwa Tanzania pamoja na miradi 9 ya msaada ambayo itatekelezwa kwa kushirikiana na Mamlaka ya Elimu ya Ufundi Stadi (VETA) na Hospitali ya Zanzibar.

Kampuni ya Huawei Tanzania ambayo imewekeza kwa zaidi miaka 15 nchini, inashirikiana na Kampuni ya Mawasiliano ya Simu Tanzania (TTCL) kusambaza Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ili kuwezesha huduma za kidigitali kupatikana kwa urahisi nchi nzima ambapo hadi sasa mkongo huo umesambaa kwa zaidi ya kilomita 15,000 nchi nzima.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news