Waziri Kairuki akemea hujuma posho za madaraka kwa walimu

NA ANGELA MSIMBIRA

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe.Angellah Kairuki amekemea vikali tabia ya baadhi viongozi kuomba rushwa ili kupitisha posho za madaraka kwa walimu wakuu.

Kairuki ametoa karipio hilo leo Januari 18, 2023 mkoani Kagera wakati akifungua kikao kazi cha tathmini ya utekelezaji wa mkakati wa elimu na uwekaji wa mpango kazi kwa mwaka 2023.

Amesema, kuna baadhi ya viongozi wa elimu mkoani na wilayani wamekuwa na tabia ya kuomba fedha (rushwa) kwa walimu wakuu wanapofuatilia vocha za malipo za posho ya madaraka.

"Kumekuwepo na taarifa kuwa baadhi ya viongozi mmekuwa mkiomba fedha kwa walimu wakuu ili muidhinishe fedha zao za posho ya madaraka jambo hili si haki na halikubaliki,"amesema Kairuki.

Kutokana na hali hiyo, Kairuki amemuagiza Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI anayeshughulikia Elimu, Dkt.Charles Msonde kuhakikisha fedha za posho za madaraka zinapelekwa moja kwa moja kwenye akauti za benki za wahusika.

“Naibu Katibu Mkuu (Dkt.Msonde) tabia hii ikome mara moja, hivyo naagiza muangalie namna ya malipo ya posho za madaraka ya walimu wakuu zipelekwe moja kwa moja kwenye akaunti za wahusika na kuacha kupitisha kwenye mlolongo mrefu ambao unatumika hivi sasa,"amesisitiza Kairuki.

Amesema, kupeleka fedha kwenye akaunti za wahusika kutapunguza urasimu na michakato mirefu, kuongeza ufanisi na kuwapunguzia walimu mzigo wa kufuatilia fedha.

Aidha, Kairuki ametumia fursa hiyo kuwaonya viongozi wenye tabia hizo na kusisitiza kuwa hawatasita kuwachukulia hatua za kinidhamu wale wote watakaobainika kuomba rushwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news