NA GODFREY NNKO
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mheshimiwa Angellah Kairuki licha ya kuwapongeza wakuu wa wilaya, wakurugenzi na maafisa elimu mkoani Dar es Salaam pia amewataka kuhakikisha ndani ya wiki moja wanafunzi wote wanafika shule.
Amesema, kuchelewa kwa baadhi ya wanafunzi kufika shule kwa wakati ni changamoto kubwa kwa walimu ambao wanaendelea kufundisha, kwani itakuwa vigumu kuweza kwenda sambamba na mtiririko wa masomo na wale ambao walitangulia awali.
"Niwapongeze wakuu wa wilaya,wakurugenzi,maafisa elimu nimeona kazi nzuri ambayo mmeendelea nayo wiki nzima, kuendelea kuhamasisha wananchi wetu na jamii kwa ujumla kuwapeleka watoto shule na ninaamini ndani ya wiki moja ikiwezekana basi tufikie asilimia 100.
"Kwa kweli hili niendelee kutoa rai, msibweteke pamoja na kwamba tumefikia asilimia 75 kwa sasa kwa Mkoa wa Dar es Salaam, lakini tujitahidi kufikia asilimia 100 ili watoto hawa waende kwa kasi ya pamoja;
Mheshimiwa Kairuki ametoa maagizo hayo Januari 25, 2023 katika kikao kazi cha uboreshaji wa usimamizi wa elimu msingi, na sekondari na maafisa elimu kata, wakuu wa shule za sekondari, walimu wakuu wa shule za msingi na viongozi wa elimu ngazi ya halmashauri mkoani Dar es Salaam.
Amesema, katika eneo hilo, upande Halmashauri ya Wilaya ya Kigamboni bado liko chini kwa asilimia 60. "Hivyo ni vyema tukasimame kidete kiwango hiki kije juu kwenye hii idadi Kigamboni naomba sana kiongezeke.
"Upande wa Ubungo bado kiwango kiko asilimia 64 katika usajili wa kuripoti kwa wanafunzi wetu wa kidato cha kwanza,ninawaombeni sana tuendelee kuongeza kasi zaidi, ikifuatiwa na Kinondoni ambayo iko asilimia 75 ambayo iko wastani."
"Lakini pia Ilala asilimia 76, Temeke asilimia 84, nataka asilimia hizo 16 zilizobakia ndani ya siku saba zinifikie. Orodha ya wote walioenda shule binafsi ninayo, wanaotakiwa kusajiliwa yote ninayo, nitakuja kujiridhisha kichwa kwa kichwa.
"Na nitafanya sampling ya shule kadhaa, sasa endapo ikatokea data hazijaendana Afisa Elimu na wengine wote wanaohusika kwenye hili hatutaelewana.
"Ninaomba kila mmoja kwa nafasi yake aliyekasimiwa madaraka, takwimu hizo nikija uwe na uhakika nazo na kila mwanafunzi anayestahili kusajiliwa awe ameweza kusajiliwa,"amefafanua Mheshimiwa Waziri Kairuki.
Wakati huo huo, Mheshimiwa Waziri Kairuki amesema anatamani kuona wenye mahitaji maalum nao wana haki ya kusoma.
Pia amesema,hatataki kuona wenye mahitaji maalumu wanabakia majumbani. "Kwenye ripoti ijayo nitapenda kujua watoto wenye mahitaji maalumu idadi yao kwa darasa la awali, darasa la kwanza ambao wameweza kuandikishwa.
"Tuendelee kuhamasisha hata kama Ilala wamefikia asilimia 110 tuwapongeze kwa upande wa darasa la kwanza, Kigamboni darasa la kwanza asilimia 94. Asilimia 87 Kinondoni, asilimia 85 Ubungo ambapo tunapata wastani kwa Mkoa wa Dar es Salaam kwa darasa la kwanza kwa asilimia 95.
"Tuendelee kuongeza kasi, kwa upande wa uandikishaji wa elimu ya awali Jiji ni asilimia 118 kwa waliotarajiwa tuwapongeze sana. Kigamboni asilimia 80, Kinondoni asilimia 59 bado tuongeze nguvu, Temeke asilimia 64, Ubungo asilimia 45 bado wako chini lazima tuongeze nguvu na hii inanipa maswali mengi katika halmashauri nyingine wako vizuri,"amebainisha Mheshimiwa Kairuki.
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Wariri Kairuki amewapongeza Dar es Salaam katika suala la ufaulu hususani katika matokeo ya kidato cha sita.
Amesema, kwa kiasi kikubwa wamekuwa wakienda vizuri kwa wastani, ukiangalia asilimia 98 walikuwa wamefaulu kidato cha sita jambo ambalo ni nzuri.
"Vile vile upande wa kidato cha nne mmejitahidi kufanya vizuri, isipokuwa katika wastani wa daraja la kwanza hadi daraja la tatu bado ukiangalia idadi ni ndogo sana, ukiangalia kwa wastani ni chini ya asilimia 35. Na mwaka huu tunaweka malengo nchi nzima ufaulu wa division one hadi three kwa kidato cha nne isipungue asilimia 50 kwenda juu.
"Kwa pamoja twende kwa haki kwa misingi ya taaluma zetu tuwajengee umahiri na kujiamini wanafunzi wetu. Zipo shule bado ukiziangalia division one hadi three ni wachache sana na division four hadi zero ni wengi sana.
"Lazima kila mmoja kwa namna yake aende akatafakari na kutathmini kuona nini kimesababisha matokeo ya namna hii kusudi tunapoelekea matokeo ya 2023 basi tuweze kupata matokeo ambayo ni bora zaidi.
"Ni imani yangu katika matokeo ya mwaka huu tutapiga hatua, lakini tujipange zaidi na kuondoa udanganyifu kwa sababu ukibainika ni kosa la jinai kwako na mwanafunzi na unaweza ukajikuta unapata adhabu ambayo hujaitarajia maishani mwako,"amefafanua Waziri Kairuki.
Akizungumzia kwa upande wa matokeo ya kidato cha pili, Mheshimiwa Kairuki amesema, kwa Mkoa wa Dar es Salaam kuna changamoto kidogo.
"Katika matokeo ya kidato cha pili bado kumekuwa na changamoto, tunaona kwa Mkoa wa Dar es Salaam wanaorudia ambao wamerudia kwa mwaka 2022 darasa ni takribani wanafunzi 6,550 hii ni idadi kubwa sana ni vyema tukaendelea kujipanga kuhakikisha idadi hii haipo kabisa.
"Ukiangalia takwimu za mwaka 2021 waliorudia kidato cha pili walikuwa wanafunzi 3,242 lazima mkaangalie nini shida iliyosababisha mkafikia hapoi na kuangalia namna ya kupata ufumbuzi.
"Lakini pia darasa la nne kwa mwaka 2022 tumeshuhudia wanafunzi waliorudia darasa la nne wanafunzi 1,657 wanaotokea Mkoa wa Dar es Salaam, tunapoendelea kujiwekea mpango mkakati eneo hili lazima liangaliwe pia,"amefafanua na kuelekeza Mheshimiwa Waziri Kairuki.
Mbali na hayo, Mheshimiwa Waziri Kairuki amesema, kwa upande wa darasa la saba anawapongeza Mkoa wa Dar es Salaam kwa kuwa na asilimia 97 ya ufaulu.
RC Dar
Akizungumza katika kikao kazi hicho kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Amos Makalla, Mkuu wa Wilaya wa Ilala, Mheshimiwa Ng'wilabuzu Ndatwa Ludigija amesema, walitarajia kuandikisha watoto wa elimu ya awali 46,994. Hadi kufikia Januari 20, 2023 jumla ya wanafunzi 34,178 wameandikishwa sawa na asilimia 75.
"Katika Jiji la Dar es Salaam tumeandikisha watoto 13,108 sawa na asilimia 118. Lakini Manispaa ya Kigambani tumeandikisha watoto 3,439 sawa na asilimia 80, Manispaa ya Kigamboni tuliandikisha watoto 6,014 sawa sawa na asilimia 59, Temeke tumeandikisha watoto 6,522, sawa na asilimia 64, Manispaa ya Ubungo tumeandikisha watoto 5,042 sawa na asilimia 45, hivyo kufanya jumla ya asilimia 75 kama nilivyoeleza,"amefafanua Mkuu huyo.
Amesema, mkoa ulitarajia pia kuandikisha wanafunzi wa darasa la kwanza 111,194 na hadi kufikia Januari 20, 2023 jumla ya wanafunzi 107,485 wameandikishwa sawa na asilimia 95.
Katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam amesema, wameandikisha watoto wapatao 41,146 sawa na asilimia 110, Kigamboni 6,572 sawa na asilimia 94, Halmashauri ya Kinondoni watoto 15, 556 sawa na asilimia 87, Halmashauri ya Temeke watoto 27,062 sawa na asilimia 87, Halmashauri ya Ubungo watoto 16,013 sawa na asilimia 85 na kufanya jumla ya asilimia 95 ya wanafunzi walioandikishwa.
"Mheshimiwa Waziri wa Nchi jumla ya wanafunzi 88,682 wamefaulu mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka 2022 na waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza 2023 ambao ni sawa na asilimia 97.02 hadi kufikia Januari 20, 2023 jumla ya wanafunzi 66, 565 sawa na asilimia 75 wameripoti kujiunga na masomo ya kidato cha kwanza katika shule mbalimbali binafsi na serikali wakiwemo wenye mahitaji maalum.
"Mchanganuo katika Halmashauri za Jiji la Dar es Salaam wanafunzi waliojiunga kidato cha kwanza walioripoti ni 23,166 sawa na asilimia 66. Manispaa ya Kigamboni 2,884 sawa na asilimia 60. Kinondoni waliojiunga mpaka sasa ni 10,987 sawa na asilimia 75.
"Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jumla ya wanafunzi ni 19,888 sawa na asilimia 84 na Halmashauri ya Ubungo wanafunzi 9,660 sawa na asilimia 64. Na hi inafanya jumla ya wanafunzi waliojiunga kufikia 66,565 ambao ni wastani wa asilimia 75,"amefafanua Mheshimiwa Ludigija kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Pia amesema,wanaendelea kupokea wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza mwaka huu katika shule mbalimbali.
Mheshimiwa Ludigija amesema, Mkoa wa Dar es Salaam wana idadi kubwa sana ya wanafunzi wanojiunga darasa la awali, msingi na kidato cha kwanza.
Aidha, wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan kwani Mkoa wa Dar es Salaam amewapatia shilingi bilioni 12.5 kutoka kwenye kapu la mama kwa ajili ya madarasa 618 katika shule za sekondari na kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza.
"Mheshimiwa Waziri ujenzi mpaka sasa tuna madarasa 69 ambayo hayajakamilika ambayo tulikutana na changamoto ikiwemo ufinyu wa maeneo ya kujenga, halmashauri zimefanya jitihada mbalimbali katika baadhi ya maeneo walikwenda kufidia kupata maeneo na madarasa haya ambayo hayajakamilika ni madarasa yanayojengwa kwa mtindo wa ghorofa.
"Lakini nikuhakikishie wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza nafasi zipo na wanaendelea kupokelewa. Nikuhakikishie kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa na viongozi wote tupo tayari kusimamia madarasa haya yaweze kukamilika na kutimiza ndoto ya Rais wetu ya kuwa na miundombinu bora na mazingira rafiki ya kufundishia.
"Mheshimiwa Waziri katika mkakati wa uandikishaji darasa la awali mapokezi ya wanafunzi wa kidato cha kwanza 2023 mkuu wetu wa Mkoa Amos Makalla aliitisha kikao kama hiki na maeneo haya haya na ukumbi huu huu na alitoa maelekezo mahususi.
"Ni kwa watendaji wote wa mitaa na kata wakiwemo wenyeviti wa serikali za mitaa na kutoa maelekezo kuhakikisha wanasimamia na kupita nyumba kwa nyumba ili kila mtoto ambaye amefikia umri wa darasa la kwanza na waliofaulu kujiunga form one na wenye mahitaji maalum wote wanakwenda shule.
"Naomba niseme kwamba Mkoa wa Dar es Salaam tumejipanga kuhakikisha tunatimiza mlengo yako na wizara kwa ujumla,"amesisitiza Mheshimiwa Ludigija kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Amos Makalla.