NA MWANDISHI WETU
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Dkt.Samia Suluhu Hassan iliyopo Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma. Mheshimiwa Waziri Mkuu ameweka jiwe hilo la msingi Januari 6, 2023 wilayani humo.
Mradi huo unatekelezwa kwa awamu mbili kwa gharama ya shilingi bilioni nne kupitia Mradi wa Kuboresha Elimu ya Sekondari (SEQUIP) ambapo awamu ya kwanza ya mradi huu ulianza tarehe 6 April 2022 na unaotarajiwa kukamilika tarehe 30 Januari 2023 na utatumia shilingi bilioni tatu na jumla ya majengo 22 yanajengwa
Hadi kufikia Disemba 31, 2022 kiasi cha shilingi 2.2 zimetumika katika utekelezaji wa mradi huu. Majaliwa amesema shule hiyo itakapokamilila itapokea wanafunzi 1080 ambapo awamu ya kwanza itapokea wanafunzi 600.
Aidha awamu ya pili ambayo ujenzi wake unatarajiwa kuanza ndani ya mwaka huu kwa gharama ya shilingi bilioni 1 inatarajiwa kupokea wanafunzi 480 pale itakapokamilika
Awamu ya pili itahusisha ujenzi wa madarasa 10 yenye ofisi za walimu 3, chumba cha ICT, Maktaba, nyumba 4 za walimu na mabweni 4.
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Dkt. Samia ameamua kuwekeza kwenye elimu ya mtoto wa kike ili kumpunguzia changamoto zilizowakabili na ndio maana ameamua kujenga shule za wasichana nchi nzima“Si kwamba amemtenga mtoto wa kiume hapana, ameamua kwenda nao wote
Pia, Waziri Mkuu amewataka wakandarasi wanaojenga shule hiyo kuhakikisha wanakamilisha ujenzi wa shule hiyo katika muda uliopangwa ili waanze kupokea wanafunzi shule ya Sekondari Dkt. Samia Suluhu Hassan inatarajia kuanza kupokea wanafunzi wa kidato cha tano Julai, 2023.
Naye Naibu Waziri Ofisi ya Rais (TAMISEMI) Dkt. Festo Dugange amesema watahakikisha wanasimamia ujenzi wa mindombinu iliyobaki katika shule hiyo ili ikamilike na ianze kudahili wanafunzi
Akizungumza kuhusu Sekta ya Afya Dkt. Dugange amesema kuwa halmashauri zote 184 zitapata magari mawili ikiwa moja ni la wagonjwa (ambulance) na moja ni kwa ajili ya usimamizi wa huduma za afya.