NA MWANDISHI WETU
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa wa Mheshimiwa Rais wa awamu ya nane wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi jumla ya miradi 215 imesajiliwa kupitia Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 3.26.
Muonekano wa Hoteli ya Kilindini, iliyopo Pwani Mchangani, Wilaya ya Kaskazini “A”, Zanzibar, ambayo imefunguliwa rasmi Januari 11, 2023 na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ikiwa ni sehemu ya shamrashamra kuelekea Maadhimisho ya Miaka 59 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
“Miradi yote hii inatarajiwa kutoa ajira zaidi ya 13,000. Mafanikio haya yote kwa kipindi hiki kifupi, yamechangiwa na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Nane zikiwemo sera na mipango madhubuti iliyowekwa na Chama cha Mapinduzi kupitia Ilani yake ya Uchaguzi ya Mwaka 2020.”
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo Jaruari 11, 2023 baada ya kuzindua mradi wa hoteli ya Kilindini yenye hadhi ya nyota tano inayomilikiwa na kampuni ya KILINDINI COMPANY LIMITED iliyoko katika kijiji cha Pwanimchangani wilaya ya Kaskazini A ikiwa ni sehemu ya matukio muhimu yaliyojumuishwa katika maadhimisho ya sherehe za kutimiza miaka 59 ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikata utepe kuashiria ufunguzi wa Hoteli ya Kilindini, iliyopo Pwani Mchangani, Wilaya ya Kaskazini “A”, Zanzibar, Januari 11, 2023. Ikiwa ni sehemu ya shamrashamra kuelekea Maadhimisho ya Miaka 59 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akifafanuliwa jambo na Afisa Rasilimali Watu, Othman Hussein, baada ya ufunguzi wa Hoteli ya Kilindini, iliyopo Pwani Mchangani, Wilaya ya Kaskazini “A”, Zanzibar, Januari 11, 2023. Ikiwa ni sehemu ya shamrashamra kuelekea Maadhimisho ya Miaka 59 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Amesema wananchi wana kila sababu ya kuyaenzi mapinduzi hayo kwa sababu ndicho chombo kilichowavusha kutoka katika gharika za kutawaliwa na kubaguliwa katika nchi yao.
“Kwa mnasaba huo, sherehe hizi za kuadhimisha Mapinduzi matukufu ya Zanzibar zinakua ni sehemu ya historia muhimu kwani zinatukumbusha jinsi ambavyo wakulima na wafanyakazi wanyonge walivyokataa madhila ya kubaguliwa na kunyanyaswa.”
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na wananchi, baada ya ufunguzi wa Hoteli ya Kilindini, iliyopo Pwani Mchangani, Wilaya ya Kaskazini “A”, Zanzibar, Januari 11, 2023. Ikiwa ni sehemu ya shamrashamra kuelekea Maadhimisho ya Miaka 59 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
“Kukusanyika kwetu hapa katika kijiji cha Pwani Mchangani ni kielelezo kingine cha uwepo wa amani na usalama katika nchi yetu. Uwepo wa amani na usalama umekuwa chachu katika kuvutia wawekezaji wengi wa kigeni na hivyo, kuvifanya visiwa vyetu vya Unguja na Pemba kuwa sehemu sahihi ya kuwekeza mitaji yao.”
Amesema kuwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan na Rais Dkt.Mwinyi wanao mkakati endelevu wa kukuza sekta ya uwekezaji nchini ikiwemo kushirikisha sekta binafsi nchini na kuvutia mitaji kutoka nje kwa lengo kuhakikisha nchi zetu zinakuwa na uchumi imara.