Waziri Mkuu:Miradi 630 ya uwekezaji yenye thamani ya dola bilioni 3.7 imesajiliwa TIC

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema katika mwaka wa fedha 2021/2022 miradi mipya ya uwekezaji 630 yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 3.68 inayotekelezwa na makampuni ya India imesajiliwa kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na Ujumbe wa Bunge la India, ulioongozwa na Mheshimiwa OM Birla (wa kwanza kulia) wakati alipokutana nae katika Ofisi ndogo ya Waziri Mkuu Magogoni jijini Dar es Salaam kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dk. Samia suluhu Hassan. Januari 19, 2023. Kushoto ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Amesema hatua hiyo inatokana na jitihada mbalimbali za kuboresha mazingira ya uwekezaji zinazofanywa na Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Hivyo, ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji wengine kutoka nchini India waje wawekeze Tanzania.

Mheshimiwa Majaliwa ameyasema hayo leo Januari 19, 2023 wakati alipokutana na ujumbe wa Bunge la India (Lock Sabha) ulioongozwa na Spika wa Bunge hilo, Mheshimiwa OM Birla. Waziri Mkuu kutana na viongozi hao kwa niaba ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia ambaye yupo nje ya nchi kikazi.

Mheshimiwa Majaliwa amesema Nchi ya India na Tanzania zimekuwa na ushirikiano Mkubwa wa kiuchumi na biashara huku India ikishika nafasi ya tatu kwa kuwa na ushirikiano wa biashara unaofikia Dola za Marekani bilioni 4.58 kwa mwaka 2021 – 2022.

Waziri Mkuu amemuhakikishia Spika huyo kuwa Tanzania itaendeleza ushirikiano wa muda mrefu uliopo kati yake na India. “Rais anamatumaini makubwa na ushirikiano uliopo baina ya nchi ya Tanzania na India na kwamba ushirikiano huo umekuwa na manufaa makubwa kati ya nchi zetu.”

Amesema Tanzania na India zimekuwa na ushirikiano wa muda mrefu katika sekta mbalimbali zikiwemo za uchumi, nishati, maji, elimu, afya, biashara na teknolojia na hivyo kuleta manufaa makubwa.“Mheshimiwa Rais amefurahia ujio wako Nchini Tanzania, ni matarajio yake kuwa ujio huu utakuwa na manafuu makubwa baina ya Nchi zetu.”

“Mwezi juni 2022 tumeshuhudia makampuni sita kutoka nchini India yakitia saini mikataba ya miradi ya maji kwa miji 28 yenye thamani ya zaidi ya dola za Marekani milioni 500 ambayo ikikamilika itawawezesha watanzania zaidi ya milioni sita kupata maji ya uhakika.”

“Nitoe wito kwa Nchi ya India ambayo kwa sasa ni mwenyekiti wa Nchi za G 20, kuwa mtetezi wa Nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania katika suala zima la mabadiliko ya hali ya hewa, Usalama wa chakula, uwezeshaji wa wanawake na vijana pamoja na kupambana na athari za uviko 19”

Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amesema ujio wa Spika huyo na ujumbe alioongozana nao utaboresha uhusiano baina ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Bunge la India kwa wabunge na viongozi wa mabunge hayo kubadilishana uzoefu.“Nitoe wito kwa mabunge yetu haya kuweka utaratibu wa kutembeleana na kubadirishana uzoefu, ili kukuza ushirikiano.”

Pia, Mheshimiwa Majaliwa ameishukuru Serikali ya India kwa ushirikiano na namna ambavyo imeendela kutoa fursa za masomo kwa wataalam wa Tanzania katika sekta mbalimbali nakuiomba nchi hiyo iendelee kutoa ufadhili huo wa masomo katika nyanja nyingine za teknolojia ya mawasiliano, afya, uhandisi, kilimo, maji, madini na gesi.

Kwa Upande wake, Spika wa Bunge la India Mheshimiwa Birla amesema, Bunge la India litakuwa msemaji mzuri wa ushirikiano na maendeleo baina ya Tanzania na India ili nchi hizo ziendelee kunufaika na ushirikiano uliopo.

“Kwa niaba ya Serikali na Bunge la India, tunawasilisha pongezi zetu kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kwa uongozi wake wa mfano, sasa tunaona uchumi wa Tanzania unakuwa kwa kasi na tunaona miradi mikubwa ikitekelezwa, tafadhali fikisha pongezi zetu kwake.”

Mheshimiwa Birla na ujumbe wake yuko katika ziara ya kikazi ya siku tatu Nchini Tanzania ambapo pamoja na mambo mengine atatembelea vituo mbalimbali vya utalii ikiwemo mbuga za wanyama.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news