NA MWANDISHI WETU
WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda ameishukuru Serikali ya Finland kwa namna ambavyo imekuwa ikishirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuendeleza sekta ya elimu, Sayansi na Teknolojia hususan ushirikiano kati ya Vyuo Vikuu vikuu na ufadhili wa miradi kupitia taasisi.
Waziri Mkenda ameeleza hayo jijini Dodoma alipokutana na Waziri wa Finland anayeshughulikia masuala ya Uchumi Mhe. Mika Lintila na ujumbe wake.
Amesema, kwa sasa nchi ya Tanzania inafanya mapitio ya Sera ya elimu ya mwaka 2014 na mabadiliko ya mitaala kwa kuhakikisha elimu inatoa ujuzi bila kuathiri ubora katika taaluma.
"Finland mnafanya vizuri sana kwenye elimu ninaomba ushirikiano uliopo uendelee hasa katika kipindi hiki ambacho tunafanya mabadiliko makubwa ya mfumo wa elimu,"amesema Prof.Mkenda.