NA MWANDISHI WETU
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu, Mheshimiwa George Simbachawene ameridhishwa na kasi ya ujenzi wa kiwanda cha kupiga chapa cha Serikali ambacho mpaka sasa msingi wa jengo na ujenzi wa boma la jengo, kuta, kupiga plasta na kupauwa vimeshafanyika.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu, Mhe. George Simbachawene akitoa maelekezo kwa watendaji wa Ofisi ya Mpiga Chapa wa Serikali mara baada ya kujionea maendeleo ya ujenzi wa kiwanda kipya cha Mpiga chapa Mkuu wa Serikali.
“Hiki kiwanda tunatarajia kukifunga mitambo na mashine za kisasa ili kiweze kufanya jukumu la kuchapa nyaraka za Serikali na shughuli za Mpiga Chapa ziweze kufanyika kwa ufanisi.”Kauli hiyo ameitoa alipotembelea na kujionea maendeleo ya ujenzi wa kiwanda hicho cha Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali kilichopo Kisasa katika Jiji la Dodoma tarehe 17 Julai 2023.
"Ofisi hii ni muhimu sana kwa nchi, ni lazima iwe Ofisi bora kwa sababu nyaraka nyingi za siri za serikali zinapaswa kuchapwa na Ofisi ya Mpiga Chapa wa Serikali."
Waziri Simbachawene amempongeza Rais Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda hicho cha mpiga chapa wa serikali kwa kiasi cha shilingi billioni 1.88.
“Serikali imetoa pia kiasi cha shilingi milioni 350 ambazo zitatumika kufanyia ukarabati kiwanda na Mashine za Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali jijini Dar es Salaam ikiwa ni pamoja na kiasi kingine cha shilingi billioni 1.4 kwa ajili ya kununua malighafi kwa viwanda vinavyondelea na uzalishaji, cha Dodoma na Dar es salaam.”
Amefafanua, kiwanda kipya cha Dodoma cha Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali imetoa kiasi cha shilingi billioni 3.9 ambayo itasaidia kununua mitambo mipya na ya kisasa ili kuhakikisha nyaraka zote muhimu za serikali zinachapishwa katika kiwanda hicho.
“Nembo ya Taifa, Bendera ya Taifa na Mhuri ni vitu ambavyo vimewekwa katika uangalizi wa Ofisi ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali.”
Naye Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali,Bw. George Lugome ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kutoa fedha kwa ajili ya kuboresha Idara ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali kwa kuiwekea majengo yenye uwezo wa kuwa na miundo mbinu mizuri na mashine za kisasa ambazo zitasaidia kuchapa nyaraka zenye alama ya siri.
“Sheria ya alama za Taifa ya mwaka 1971 inatamka wazi kabisa kwa yoyote anayekiuka au anaibadili nembo ya Taifa au alama za Taifa anastahili kupewa adhabu ya kifungo cha miaka miwili jela,” amesema Lugome.
Ametoa wito kwa taasisi binafsi zinazotaka kujihusisha na uchapaji wa nyaraka kuhakikisha wanathibitishwa na Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali na Ofisi ya Usalama ya Serikali ili waweze kupata kibali.