NA MWANDISHI WETU
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera Bunge na Uratibu, Mhe.George Simbachawene amewataka watendaji wa Serikali kuendelea kutatua changamoto za wananchi zinazowakabili ili kuchochea kasi ya maendeleo nchini.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Mhe. George Simbachawene akiwa katika picha ya pamoja na Timu ya Menejimenti ya ofisi yake mara baada ya ufunguzi wa mafunzo yao ya Idara ya Ufuatiliaji na Tathmini yaliyofanyika Dodoma leo. (Picha na OWM).
Mheshimiwa Simbachawene ametoa kauli hiyo wakati akifungua mafunzo ya siku mbili ya kujenga uwezo kwa Menejimenti ya Ofisi ya Waziri Mkuu yaliyolenga kuwajengea uelewa kuhusu Idara ya Ufuatiliaji na Tathmini ya Utendaji wa Shughuli za Serikalini yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi uliopo Njedengwa jijini Dodoma leo Januari 19, 2023.
Waziri amehimiza kila mtendaji wa Serikali kuhakikisha anatekeleza majukumu yake kwa ufanisi huku akitatua changamoto za wananchi katika eneo lake la kazi.
Ameongezea kuwa, ni muhimu kwa watendaji kuwajibika kwa kuyafikia malengo ya Serikali ya Awamu ya Sita huku wakileta matokeo chanya yatokanayo na utendaji mzuri wa kazi zao za umma.
"Hakikisheni mnakuwa watu wa msaada kwa wengine katika kuyatekeleza majukumu yenu, muwe watengeneza furaha na hii iwe kipimo kwa kila mwenye kukufikia huku ukizingatia taratibu za utumishi wa umma na sheria zilizopo,"amesema Waziri Simbachawene.
Aidha, amewaasa waendelee kutumia taaluma zao kuleta matokeo chanya kwa Serikali na jamii huku wakijitathimini utendaji wa kila siku.
“Ni sahihi kujitathimini kila iitwapo leo ili kuona namna unavyoleta matokeo chanya kwenye utendaji wako wa kila siku, matokeo utayoyapata yatatusaidia kuongeza tija,”amesisitiza Waziri Simbachawene.
Akieleza umuhimu wa mafunzo hayo amewataka kuhakikisha mafunzo yanawafikia watendaji katika ngazi zote ili kuendelea kuongeza uelewa kwa watumishi wa umma.
"Mafunzo haya yawafikie watumishi wote katika idara na vitengo vyetu bila kumuacha nyuma mtu yeyote ili kuleta chachu katika utendaji na kuondokana na tabia ya mazoea,"amesema.
Pia ameongezea kuwa, matokeo ya mafunzo haya yatumike kuboresha mifumo ya uratibu, usimamizi na ufuatiliaji wa shughuli za Serikali ili kuwa na uwezo wa kupima utendaji wa wizara na taasisi mbalimbali za Serikali kisayansi.
Aidha, uwekwe utaratibu ambao utawezesha uchambuzi wa taarifa za kisekta na kutoa mrejesho wa maeneo yanayohitaji kuboreshwa au kupewa msukumo zaidi.
"Ili kuendelea kuboresha shughuli za uratibu naamini uwepo idara mpya ya ufuatiliaji na tathmini itasimamia hili na kuhakikisha kunakuwa na mrejesho kwa wizara na taasisi zote ili kuimarisha uwajibikaji,"amehimiza.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Dkt.John Jingu amesema, mafunzo haya yanalenga watendaji wa Serikali kufanya kazi kwa ufanisi kwa weledi na kwa namna ambayo itakidhi mahitaji pia yatajikita katika majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu katika eneo la uratibu wa shughuli za serikali, na jukumu la kufanya kazi ya ufuatiliaji na tathmini ya utendaji wa shughuli za Serikali.