Waziri Simbachwene ahimiza mapambano dhidi ya udhalilishaji wanawake na watoto

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu, Mhe. George Simbachawene ametoa wito kwa walezi na jamii kwa ujumla kupiga vita dhidi ya udhalilishaji kwa Wanawake na Watoto mambo ambayo yanapoteza heshima na haiba kwa nchi yetu.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu, Mhe. George Simbachawene akipata maelezo kutoka kwa mtaalamu kuhusu ramani ya ujenzi wa kituo cha afya Uzi.

“Tushirikiane katika kutokomeza udhalilishaji, kupinga, kuwafichua na kuwafikisha katika vyombo vya sheria wale wote wanaofanya unyama huu kwa wanawake na watoto, lakini pia hatuna budi kurejesha utamaduni wetu wa malezi ya pamoja ili kulidhibiti janga hili kwa jamii na Taifa kwa ujumla.”

Wito huo ameutoa Januari 6, 2023 wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi ujenzi wa kituo cha afya Shehia ya Uzi Mkoa wa Kusini Unguja katika sherehe ya kuadhimisha miaka 59 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu,Mhe. George Simbachawene akiweka jiwe la msingi katika Kituo cha afya Uzi Mkoa wa Kusini Unguja.

"Katika shughuli yetu kuu ya uwekaji wa jiwe la msingi la mradi wetu huu, ambayo tayari tumeshaifanya kwa ukamilifu wake, lililobaki kwetu ni kuhakikisha mradi huu unakamilika kwa hatua zilizobakia ili kukidhi malengo tuliyoyakusudia.

"Tunaendelea kushuhudia mapinduzi makubwa ya kiuchumi yanayoendelea kufanyika nchi nzima na hii inathibitisha kauli ya mwaka huu isemayo “Mapinduzi yetu ndio Amani yetu tuyalinde kwa Maendeleo yetu”.

"Aidha, Serikali zetu zote mbili ya SMT na SMZ zimeendelea kusogeza huduma mbalimbali kwa wananchi wake na tunashuhudia ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo huu wa ujenzi wa Kituo cha Afya katika Shehia zetu za Uzi na Ng’ambwa. Mradi ambao unafadhiliwa na Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ambao ni miongoni mwa matunda ya Mapinduzi yetu yaliyofanyika Januari 12, mwaka 1964."
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu, Mhe. George Simbachawene akizungumza jambo na Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Mhe. Rashid Hadid Rashid.

“Ujenzi huu wa Kituo cha Afya umekuja baada ya kuona upo uhitaji mkubwa wa jengo hili kwa wanajamii wa Shehia zetu za Uzi na Ng’ambwa, hali ambayo itarahisisha upatikanaji wa huduma bora ya afya kwa wananchi hususani mama na watoto,”amesema Waziri.

Waziri amesisitiza ushirikiano wa hali na mali katika ufuatiliaji, usimamizi na utekelezaji wa mradi ili uweze kukamilika kwa wakati na kwa ubora wa hali ya juu. 

Pia, amewaomba viongozi wa Mkoa, Wilaya, Baraza la Mji Kati na Shehia zote kuwa karibu katika kusimamia utekelezaji wa mradi huo muhimu kwa jamii na Taifa kwa ujumla na kuendelea kutoa msaada pale unapohitajika ili kufanikisha ukamilishaji wa mradi kwa wakati.

Akimkaribisha mgeni Rasmi Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Mhe. Rashid Hadid Rashid amewapongeza TASAF kwa jinsi wanavyoshirikiana na serikali katika kutekeleza miradi ya maendeleo.

“Katika kipindi kifupi cha miaka miwili wameweza kujenga ukumbi wa mitihani, Kizimkazi Dimbani na katika masuala ya Kilimo cha Mwani, wazee wetu wanashughulika na kilimo hicho na walikuwa wanapata tabu kuchukua Mwani baharini kuja juu, TASAF imewajengea ngazi ili iwe rahisi kufika juu.”

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF), Bw. Ladisius Joseph Mwamanga amesema, TASAF inajenga uwezo wananchi kwa kukuza rasilimali watu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

“Napenda kuwapongeza wananchi kwa ushirikiano mkubwa ambao wameuonesha katika ujenzi wa kituo cha afya uzi, mradi umesimamiwa kwa ukaribu na wananchi wenyewe wa Shehia ya Uzi na Ng’ambwa.”
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu, Mhe.George Simbachawene (kulia) akisalimiana na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Khamis Hamza Khamisi.

Awali katika risala ya wananchi iliyosomwa na Bi.Lemi Khalifa amesema utekelezaji wa mradi ulianza mwezi wa nane 2022 kwa kusimamiwa na kamati kuu mbili ikiwemo kamati ya Shehia na kamati ya usimamizi ngazi ya jamii CMC.

“Mradi ulitengewa kiasi cha milioni 184,8 21,428 kati ya hizo shilingi milioni 134,270.261 zimetumika na ujenzi unaendelea.”

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news