WEWE ANZA NAYE MUNGU

NA LWANAGA MWAMBANDE

KIUNGO mshambuliaji wa Simba SC, Clatous Chama kutoka nchini Zambia amesema kuwa, kila jambo analotaka kulifanya na analolifanya lazima amshirikishe Mungu kwanza na kumshukuru, hivyo wengine wanaweza kufanya hivyo na wataona matokeo mazuri.

"Jambo la kwanza kama nilivyosema awali,na nitaendelea kulisema hili kuwa, kipaji changu na hapa nilipofikia ni kwa neema za Mungu, kila wakati ninapofanya jambo lango huwa ninamshirikisha Mungu kwanza."

Kwa maneno hayo ya hekima kutoka kwa Chama, mshairi wa kisasa Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa, kuanza na kumaliza na Mungu ni ushindi mkubwa katika maisha. Endelea;


1. Wewe anza naye Mungu,
Umshirikishe Mungu,
Mwisho maliza na Mungu,
Kasema Clatous Chama.

2. Kwa mafanikio yako,
Katika shughuli zako,
Mtu ana neno kwako,
Ni huyu Clatous Chama.

3. Udambwiudambwi wake,
Huo uchezaji wake,
Sifa kwa Mungu si kwake,
Kasema Clatous Chama.

4. Na matamanio yake,
Kwa wachezaji wenzake,
Wazidi kiwango chake,
Kasema Clatous Chama.

5. Kujisifu anagoma,
Kujikweza anagoma,
Mungu ni yake salama,
KasemaClatous Chama.

6. Sikia hiyo vijana,
Kwa mazoezi kazana,
Ila msijejivuna,
Kasema Clatous Chama.

7. Ni mchezaji wa Simba,
Kwa Lusaka ndiye Mwamba,
Hajisifii umwamba,
Kasema Clatous Chama.

8. Wapo wenzangu na Mimi,
Umewakaa umimi,
Ashauri hawasomi,
Kasema Clatous Chama.

9. Kama unanyenyekea,
Baraka ukipokea,
Utazidi endelea,
Kasema Clatous Chama.

10. Sifa zinapokujia,
Kwa Mungu wahamishia,
Na Mungu afurahia,
Kasema Clatous Chama.

11. Heshima akichukua,
Vile Mungu wamwinua,
Naye atakuinua,
Kasema Clatous Chama.

12. Mungu atusaidiie,
Ushauri tusikie,
Mioyoni uingie,
Toka kwa Clatous Chama.

13. Kijikweza utashushwa,
Kijishusha tapandishwa,
Ndivyo tunahadharishwa,
Kasema Clatous Chama.

14. Ushauri mujarabu,
Uovu wetu watibu,
Tuweze kujiratibu,
Kasema Clatous Chama.

15. WEWE ANZA NAYE MUNGU,
FANYA UKIWA NA MUNGU,
MALIZA SIFA KWA MUNGU,
USHAURI WAKE CHAMA.

16. MUNGU TUPE UTULIVU,
TUKIWA NA USHUPAVU,
SIFA TUSITOE SIFA,
TUKUADHIMISHE MWEMA.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news