TEHRAN-Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislam Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ametoa msamaha na punguzo la vifungo kwa maelfu ya watuhumiwa na wafungwa kuelekea maadhimisho ya miaka 44 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na sikukuu za mwezi wa Rajab.
Mapinduzi ya Iran, ambayo pia yanaitwa Mapinduzi ya Kiislamu (1978-79) yalisababisha kupinduliwa kwa Serikali ya Kifalme mnamo Februari 11, 1979, na kusababisha kuanzishwa kwa Jamhuri ya Kiislamu.
Ali Khamenei ameidhinisha pendekezo la Mkuu wa Idara ya Mahakama ya Iran, Gholam Hossein Mohseni Ejei la kupunguziwa vifungo au kuachiwa huru maelfu ya wafungwa wa Kiirani waliokuwa wakitumikia vifungo katika magereza mbalimbali katika Jamhuri ya Kiislam ya Iran.
Miongoni mwa walionufaika na msamaha huo wapo watu waliokamatwa katika miezi ya hivi karibuni kwa kosa la kushiriki katika fujo na vurugu zilizoibuka kwa kisingizio cha kifo cha binti wa Kikurdi Mahsa Amini.
Katika barua yake kwa Kiongozi Muadhamu, Mkuu wa Idara ya Mahakama ya Iran, Gholam Hossein Mohseni Ejei amesema: katika matukio ya hivi karibuni baadhi ya wananchi hususani vijana walifanya vitendo visivyo sahihi kutokana na kuathirika na propaganda za maadui.
Amesisitiza kwa sasa wengi wao wamejuta kwa vitendo hivyo na wanaomba msamaha hasa baada ya kufahamika njama za maadui wa kigeni na makundi yaliyo dhidi ya Mpainduzi ya Kiislamu.
Sura ya 110 ya Katiba ya Iran inampa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu haki ya kupunguza au kuwasamehe wafungwa kutokana na pendekezo la Mkuu wa Idara ya Mahakama ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.(Parstoday)