NA DIRAMAKINI
WATUMISHI mbalimbali wa Mungu kutoka nchini wamesema wataendelea kusimama imara kuujenga Umoja wa Mitume na Manabii Tanzania (UMMT) huku wakiendelea kuamini kuwa,nyakati za mwisho wengine watajitenga na imani huku wakisikiliza roho zidanganyazo kwa ajili ya kuwapoteza wengine.
Hayo wameyasema kwa nyakati tofauti wakati wakielezea kuhusu msimamo wao wa kuendelea kuujenga na kuimarisha umoja huo ambao umedhamiria kuwaunganisha hapa nchini ili waendelee kulihubiri neno la Mungu nyakati zote iwe changamoto au raha.
Mwenyekiti Msaidizi wa Umoja wa Mitume na Manabii Tanzania (UMMT) Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro,Chief Apostle JR amesema kuwa, Kilimanjaro wataendelea kusimamia imara na Rais wa Umoja wa Mitume na Manabii Tanzania, Dkt.Nabiijoshua Aram Mwanytala.
"Kama kiongozi katika Mkoa wa Kilimanjaro na Wilaya ya Hai, Mheshimiwa Rais Nabiijoshua Aram Mwantyala nikuahidi kwamba tupo pamoja Kilimanjaro na tutaungana na wewe hatua kwa hatua, hakuna mahali tutarudi nyuma iwe kwa jasho, iwe kwa gharama ya fedha au kwa gharama ya muda.
"Lakini tutahakikisha tunafika kwenye kusudi, kwa sababu Umoja wa Mitume na Manabii Tanzania, ni kusudi la Mungu kwa nyakati tulizonazo. Hatuwezi kupita kirahisi, lazima tukubaliane hukumu inayotokea, lakini tuna uhakika kwamba tutashinda, maandiko yanasema kwamba, walitoka kwetu, lakini hawakuwa wa kwetu, kama wangekuwa wa kwetu, wangekaa na sisi.
"Mtu anayetoka katikati ya umoja huu ina tafsri kweli, kwamba, tulikuwa naye lakini hakuwa wa kwetu, na ndiyo maana alishindwa kuwa na sisi. Kwa hiyo, wengine ambao wapo kwenye umoja, wafahamu kuwa, ukitaka kutoka kwenye umoja, unatafuta kuwa mshirikina, kwa sababu umoja ni kusudi la Mungu, na kwa sababu ni kusudi la Mungu, unapokuwa nje ya umoja unakuwa nje ya kusudi na makandokando huwa yamebeba mauti.
"Kwa hiyo sisi hatutashangaa sana, kwa sababu unaweza kuwa katikati yetu, lakini usiwe wa kwetu, saa ya kutoka ikifika unachemka unaenda,lakini niseme wale tuliopo, shika sana ulicho nacho,asije mtu akachukua taji yake, shetani huwa hachukui taji ya mtu, bali mtu huwa anaichukua, kwa hiyo ukichezea nafasi kuna watu Mungu atawaweka pale kwa ajili yako, na wewe utaendelea kuzurura na baadaye utarudi,"amefafanua Chief Apostle JR.
Umoja wa Mitume na Manabii Tanzania (UMMT) unaongozwa na Rais Dkt.Nabiijoshua Aram Mwantyala ambaye pia ni Kiongozi Mkuu wa Huduma ya Sauti ya Uponyaji Tanzania yenye makao yake makuu mjini Morogoro.