NA MWANDISHI WETU
WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa Barabara ya Igawa-Uyole-Songwe-Tunduma yenye urefu wa kilomita 218 inayojengwa kwa kiwango cha lami kwa njia nne kutawaondolea wananchi kero ya msongamano na ajali na hivyo kurahisisha shughuli za usafirishaji wa abiria na mizigo kwa wakati.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa akizungumza na Wananchi wa Mbeya wakati wa hafla ya Utiaji saini Mkataba wa Ujenzi wa barabara ya Igawa-Uyole-Songwe-Tunduma sehemu ya Nsalaga-Airport kilomita 32 kwa kiwango cha lami, jijini Mbeya.
Akizungumza jijini Mbeya wakati wa utiaji saini wa mkataba wa ujenzi wa barabara hiyo sehemu ya Msalaga hadi Airport yenye urefu wa Kilomita (32) Prof. Mbarawa amewataka wakazi wa mkoa wa mbeya na Songwe kuchangamkia fursa za uzalishaji ili kunufaika uwepo wa barabara hiyo.
“Bidhaa za nchi za Malawi, Zambia na Kongo zinazokwenda na zinazotoka bandari ya Dar es Salaam zitafika kwa urahisi itakapokamilika barabara hii hivyo ni wakati kwa wakazi wa Nyanda za juu Kusini kutumia fursa ya uwepo wa barabara hiyo itakapokamilika,"amesisitiza Waziri Prof Mbarawa.
Naibu wa Waziri Uchukuzi, Atupele Mwakibete, akisalimia wananchi wa mkoa wa Mbeya (hawapo pichani) wakati wa hafla ya utiaji saini Mkataba wa Ujenzi wa Barabara ya Nsalaga-Airport kilomita 32 kwa kiwango cha lami, jijini Mbeya.
Waziri Prof. Mbarawa ameutaka Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) kuhakikisha thamani ya fedha inazingatiwa katika ujenzi wa barabara hiyo na kuhakikisha inakamilika kwa wakati ili kuchochea uchumi wa wananchi wa mikoa ya Mbeya na Songwe.
“Nia ya Serikali ni kuhakikisha inaboresha miundombinu ili wananchi watumie fursa hizo kukuza uchumi binafsi na Taifa kwa ujumla,"amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa akizungumza na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson baada ya hafla ya Utiaji saini Mkataba wa Ujenzi wa Barabara ya Nsalaga-Airport kwa kiwango cha lami, jijini Mbeya.
Kwa upande Spika wa Bunge la Tanzania na Mbunge wa Mbeya Mjini, Dkt.Tulia Ackson ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuimarisha miundombinu nchini hususani mkoani Mbeya hali itakayochochea kupanda kwa uchumi wa Mkoa na Taifa kwa ujumla.
"Barabara hiyo inayounganisha Tanzania na nchi za Malawi na Kongo ikikamilika itakuza biashara katika jiji la Mbeya,"amesema Spika Tulia.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) Mhandisi Rogatus Mativila na Muwakilishi wa kampuni ya China Henan International Coorporation Group Co. ltd (CHICO) wakionesha mikataba ya Ujenzi wa Barabara ya Nsalaga- Airport KM 32 mara baada ya kuisaini jijini Mbeya.
Naye Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Rogatus Mativila amemhakikishia Waziri Prof. Mbarawa kuwa wakala huo umejipanga vizuri kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati na kwa kuzingatia thamani ya fedha.
Mradi huo utakaojengwa na Kampuni ya China Henan International Coorporation Group Co. ltd (CHICO) unatarajiwa kutumia miezi 24 na utagharimu zaidi ya shilingi bilioni 138 utakapokamilika.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Bw.Juma Homera akitoa taarifa ya mkoa kwa wananchi wa mkoa wa Mbeya (hawapo pichani) wakati wa hafla ya utiaji saini Mkataba wa Ujenzi wa Barabara ya Nsalaga.-Airport KM32. kwa kiwango cha lami, jijini Mbeya.(Picha na WUU).
Barabara ya Igawa-Uyole-Songwe-Tunduma ni sehemu ya barabara kuu ya TANZAM na barabara kuu ya nne inayotoka Cape Town Afrika ya Kusini hadi Cairo nchini Misri.