NA GODFREY NNKO
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imesema, vyombo vya habari nchini vina mchango mkubwa katika sekta mbalimbali hususani upande wa Sekta ya Fedha na Uchumi kwani vinatekeleza jukumu kubwa la kuchakata taarifa sahihi kwa ajili ya kuelimisha umma wa Watanzania.
Naibu Gavana, Julian Banzi Raphael ambaye anashughulikia Utawala na Udhibiti wa Ndani wa Benki Kuu wakati akizungumza kw aniaba ya Gavana wa BoT,Emmanuel Tutuba katika semina hiyo. (Picha na BoT).
Hayo yamebainishwa Februari 27, 2023 katika Ofisi Ndogo za Makao Makuu ya BoT jijini Dar es Salaam na Naibu Gavana, Julian Banzi Raphael ambaye anashughulikia Utawala na Udhibiti wa Ndani wa Benki Kuu wakati akimwakilisha Gavana wa BoT,Emmanuel Tutuba katika semina kwa wahariri wa vyombo vya habari nchini.
Semina hiyo ambayo iliandaliwa na BoT iliwakutanisha pamoja wahariri mbalimbali ambapo waliangazia kwa kina kuhusu majukumu ya msingi ya Benki Kuu na namna inavyosimamia watoa huduma ndogo za fedha.
Banzi amesema,Benki Kuu inaamini wahariri na waandishi wa habari wakiwa na uelewa wa kutosha kuhusu masuala ya fedha na uchumi nchini watakuwa kwenye nafasi nzuri ya kufikisha ujumbe ulio sahihi na kwa lugha rahisi kwa wananchi.
Kwa nini BoT?
Jukumu la msingi la Benki Kuu ya Tanzania ni kuandaa na kutekeleza sera ya fedha inayolenga kudhibiti mfumuko wa bei na kujenga mfumo wa fedha ulio imara na unaofaa kwa ukuaji endelevu wa uchumi wa taifa.
Aidha, Benki Kuu ya Tanzania ina mamlaka ya kutoa leseni, kudhibiti na kusimamia benki na taasisi za fedha zikiwemo benki za biashara, taasisi za huduma ndogo za fedha, benki za jamii, benki za maendeleo, kampuni za karadha, taasisi za mikopo ya nyumba, watoa huduma ndogo za fedha, taasisi za taarifa za wakopaji, maduka ya kubadilisha fedha za kigeni na ofisi za uwakilishi za benki zilizoko nje.
Pia, Benki Kuu ina wajibu wa udhibiti na usimamizi wa masuala ya kifedha (uwekezaji) wa mifuko ya hifadhi ya jamii nchini Tanzania. Jukumu la msingi katika udhibiti na usimamizi wa taasisi za fedha ni kuhakikisha kuna uthabiti, usalama na ufanisi wa mfumo wa fedha na kupunguza uwezekano wa wenye amana kupata hasara.
Aidha, Serikali ilitunga Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha Na.10 ya mwaka 2018 mwezi Novemba 2018 ili kusimamia biashara ya huduma ndogo za fedha na kuhamasisha ukuaji na uendelezaji wa sekta hiyo.
Naibu Gavana huyo amesema kuwa, kufanikisha kwa sekta hiyo ukuaji wake utasaidia kuimarisha benki kuweza kukusanya rasilimali kwenda kwenye shughuli za kijamii na kiuchumi.
“Ndugu wahariri tuneona tuwashirikishe ninyi ili muweze kuelekeza ujumbe kwa wananchi kuhusu umuhimu wa sekta hii katika masuala ya kiuchumi na maendeleo ya nchi yetu. Hapo nyuma kulikuwa na changamoto kidogo kwa taasisi za huduma ndogo za fedha kama vile zinazotoa mikopo midogo midogo,hivyo Bunge lilitunga sheria ili kuondoa changamoto hizo.
"Ni vizuri mkapata nafasi ya kuelezwa kuhusu sekta hiyo ndogo ya fedha na changamoto zilizokuwepo ambazo zilikuwa zinawaumiza wakopaji,"amebainisha.
Katika hatua nyingine, Banzi amewataka wahariri kuchangia mawazo yao ili kuimarisha na kulenga kutatua matatizo yanayojitokeza katika sekta hiyo kwa ustawi bora wa sekta hiyo nchini.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Bw.Bakari Machumu akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa TEF,Deodatius Balile ameipongeza Benki Kuu kwa kuwapa mafunzo hayo muhimu ikizingatia kuwa, Taifa letu linaendelea kupitia katika mapinduzi makubwa zaidi ya kiuchumi.
"Tunashuhudia nchi yetu ikipita katika mapinduzi makubwa zaidi ya kiuchumi, na hatua zinazokuja au tunazoziona maana yake mambo yanavyokwenda yanakuwa makubwa zaidi ikilinganishwa na huko tulikotoka, sasa kama vyombo vya habari tusipokuwa na uelewa, tutakayokuwa tunayaeleza, mlioko huku ndani mtakuwa mnashangaa sana.
"Lakini kumbe, ninyi mnapokuwa mnajiboresha, tunatakiwa twende sambamba. Twende sambamba kwa maana sisi tupate ufahamu, kwa sababu masuala ya kiuchumi si mepesi sana, kwa hiyo tunapongeza kwa juhudi hizi za Benki Kuu kuhakikisha kwamba, wahabarishaji wanahabarishwa kwanza, kwa hilo tunashukuru.
"Na tungependa kuwe na mikakati ambayo itasaidia hata kuwe na waandishi maalumu wa masuala ya biashara na uchumi wapitishwe katika mabadiliko ya kisera,"amefafanua Bw.Machumu.