NA LWAGA MWAMBANDE
MWISHONI mwa mwaka jana, Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Prof. Abel Makubi alibainisha kuwa, Bima ya Afya kwa Wote itatoa fursa kwa Mtanzania mwenye hali yoyote kwenda kupata matibabu hospitali yoyote ikiwemo Hospitali ya Taifa Muhimbili na nyingine za kibingwa.
Prof. Makubi alisema hayo, alipofanya ziara ya kukagua hali ya utoaji huduma katika Hospitali ya Mkoa ya Amana, ambapo alipata fursa ya kuzungumza na waganga wafawidhi wa Hospitali za Amana, Mwananyamala, Temeke, Tumbi, Mbagala Rangitatu, Kigamboni walioongozwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dkt. Rashid Mfaume.
“Kumbukeni Bima ya Afya kwa Wote itakapopitishwa mgonjwa atakuwa na haki ya kutibiwa hospitali yoyote anayoitaka, yaweza kuwa hospitali ya binafsi au ya serikali, sasa niwakumbushe kujipanga vizuri katika kutoa huduma bora na kutatua kero za wananchi ikiwemo kukaa muda mrefu, matumizi ya lugha nzuri na misongamano isiyo ya lazima,” alisema Prof. Makubi.
Pia, alisema wananchi wana haki ya kupatiwa huduma bora, hususani katika kipindi hiki, ambacho serikali imewekeza katika upatikanaji wa dawa, miundombinu bora, vifaa tiba pamoja na ongezeko la watumishi katika maeneo ya kutolea huduma za afya nchini.
Katibu Mkuu alielekeza uongozi wa hospitali kutoa mafunzo ya huduma kwa mteja, ikiwemo matumizi ya lugha nzuri na zenye staha kwa walinzi wa usalama wanaochaguliwa kwenda katika vituo vya kutolea huduma, ili kuondoa malalamiko yanayoweza kuzuilika kutoka kwa wananchi.
Maelekezo hayo mahususi yalitolewa wakati mwafaka ambapo kwa sasa Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya unatarajiwa kusomwa kwa mara ya pili na ya tatu mapema Februali 9, 2023 na endapo Bunge likiridhia utekelezaji wake utaanza mwezi Julai 2023.
Mshairi wa kisasa,Lwaga Mwambande anasema kuwa,Bima ya Afya kwa Wote ni hakika ya matibabu. Endelea;
1. Bima ya afya kwa wote, hakika ya matibabu,
Inahusu watu wote, si mtoto siyo babu,
Tiba vipimo wapate, bila zozote sababu,
Unachangia kidogo, unawezeshwa kwa sana.
2. Bima hii mwitikio, ugumu wa matibabu,
Kwamba wengine kilio, kukosa pesa sababu,
Kufanyika mapitio, Bima kwa wote ni jibu,
Unachangia kidogo, unawezeshwa kwa sana.
3. Sasa Bunge linaketi, muswada kuuratibu,
Bima ipate tiketi, itujie kwa karibu,
Tusikwamishwe na noti, magonjwa yakiharibu,
Unachangia kidogo, unawezeshwa kwa sana.
4. Bima kwa wote usawa, ukitaka matibabu,
Tiba itayotolewa, kwa watu wote ni jibu,
Hakuna kubaguliwa, pesa ikiwqa sababu,
Unachangia kidogo, unawezeshwa kwa sana.
5. Kufika kuuza mali, kwa fedha za matibabu,
Na vipimo vile ghali, hakutakuwa sababu,
Bima kwa wote asali, itatufuta aibu,
Unachangia kidogo, unawezeshwa kwa sana.
6. Mjadala unaanza, tujisogeze karibu,
Tusikize ukianza, na zake zote sababu,
Toka Songwe hadi Mwanza, tupate yetu majibu,
Unachangia kidogo, unawezeshwa kwa sana.
7. Bima ya afya ni njema, ugonjwa ukiharibu,
Unapata tiba njema, na ya gharama ajabu,
Bima kweli usalama, kwayo tusilete gubu,
Unachangia kidogo, unawezeshwa kwa sana.
8. Hebu ulizauliza, wale watu wajitibu,
Gharama zinaumiza, wanalalama ajabu,
Wanajikimbizakimbiza, yale yanayowasibu,
Unachangia kidogo, unawezeshwa kwa sana.
9. Epuka umasikini, ule wa matibabu,
Uuze vitu vya ndani, ili wapate kutibu,
Bima ya afya saini, huyo kwako ni tabibu,
Unachangia kidogo, unawezeshwa kwa sana.
10. Serikali imewaza, imekwishapata jibu,
Hizi tiba kuziweza, bila kuleta aibu,
Bima ya wote kuwaza, lafurahisha jawabu,
Unachangia kidogo, unawezeshwa kwa sana.
Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602