BORA SHULE SI SHEREHE

NA LWAGA MWAMBANDE

HIVI karibuni Mbunge wa Jimbo la Masasi mkoani Mtwara, Mheshimiwa Geoffrey Mwambe amewataka wazazi mkoani humo kutumia fedha kusomesha watoto wao badala ya kuzielekeza zaidi kwenye sherehe za utamaduni.
Picha na Getty Images.

Mheshimiwa Mwambe alibainisha kuwa, wazazi wengi kwenye Halmashauri ya Mji Masasi hawazingatii suala la elimu kwa watoto wao, lakini wako tayari kufanya sherehe.

"Na nimewaambia hivi, kama hamtanipa ubunge tena mwaka 2025 kwa sababu ya kupinga sherehe yaani mimi niko tayari kabisa...mpaka nikamwambia mkurugenzi futa hivyo vibali vya utamaduni kila siku."

Aidha, Mheshimiwa Mwambe ameungwa mkono na Mbunge wa Tandahimba, Mheshimiwa Katani Ahmed ambaye anasema, hakuna mtu anayekataa suala la utamaduni, lakini vitendo hivyo vikiendelea kufumbiwa macho, Sekta ya Elimu mkoani humo itaendelea kudumaa.

"Mamilioni ya fedha yanayotumika katika kipindi hiki yalikuwa yanatosha kupeleka watoto shule na wazazi kuchangia chakula shuleni, lakini watu tupo tunaangalia tu."

Miongoni mwa sherehe hizo ambazo zimekuwa zikitumia muda mwingi na fedha katika maeneo mengi hususani ukanda wa Pwani na mikoa ya Kusini ni pamoja na kumcheza mwali, vigodoro na ngoma.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema kuwa, heri maisha kuyaboresha kwa elimu bora kuliko kuteketeza fedha kupitia sherehe. Endelea;

1.Tumia fedha somesha, wala si kusherehesha,
Watoto kuwawezesha, elimu kuwafundisha,
Hapo mwawaimarisha, katika yao maisha,
Bora shule si sherehe, maisha kuyaboresha.

2.Wazazi awaamsha, ujumbe wake watosha,
Wanavyojishughulisha, fedha wakizizalisha,
Watumie kusomesha, siyo kustarehesha,
Bora shule si sherehe, maisha kuyaboresha.

3.Wazazi atukumbusha, ujumbe unaokosha,
Mali tunazozalisha, ziweze tuimarisha,
Starehe zapotosha, na tena zatukausha,
Bora shule si sherehe, maisha kuyaboresha.

4.Wazazi kujizamisha, mambo ya kusherehesha,
Nguvu kuzitumikisha, shereheni zikaisha,
Jua ni kujidunisha, siyo kujenga maisha,
Bora shule si sherehe, maisha kuyaboresha.

5.Vema kujifurahisha, ila si fedha kuisha,
Watoto kutosomesha, ni kujidharaulisha,
Bora sherehe komesha, na watoto elimisha,
Bora shule si sherehe, maisha kuyaboresha.

6.Inaoneshaonesha, wengine wanachemsha,
Kazi wajitumikisha, hata mali kuzalisha,
Na zote wanazamisha, kwenda kujisherehesha,
Bora shule si sherehe, maisha kuyaboresha.

7.Wabunge wawakumbusha, na tena wawaamsha,
Ni elimu wafundisha, akili kuzipandisha,
Watoto kuelimisha, kwawajenga kimaisha,
Bora shule si sherehe, maisha kuyaboresha.

8.Geoffrey Mwambe tingisha, wananchi elimisha,
Ahmed Katani shusha, wananchi kuwavusha,
Wazidi jishughulisha, watoto kuelimisha,
Bora shule si sherehe, maisha kuyaboresha.

9.Wabunge watusomesha, ndivyo wajiwajibisha,
Kwa vile tumeonesha, twapenda jisherehesha,
Watoto kuelimisha, twajizungushazungusha,
Bora shule si sherehe, maisha kuyaboresha.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news