DCEA yanasa kilo 23.84 za mirungi Temeke, fahamu ukweli kuhusu mirungi

NA DIRAMAKINI

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) hivi karibuni ilifanya operesheni maalum katika Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam na kukamata dawa za kulevya aina ya mirungi kilo 23.84.
Dawa hizo zilikutwa zikiwa zimehifadhiwa ndani ya nyumba ya Rhoda Mohamed Salum (48) ambaye ni mkazi wa Lukongo eneo la Wailes wilayani Temeke akiwa anajiandaa kuzisafirisha kwenda nje ya nchi.

Aidha, kesho yake katika dampo la Kituo cha Polisi Chang'ombe, kiasi hicho cha dawa za kulevya kiliteketezwa chini ya uangalizi wa baadhi ya wadau kutoka taasisi zinazotambulika kisheria kama ilivyoelekezwa kisheria kwenye kanuni ya 14.

Washiriki hao ni Mwakilishi wa Kamishna wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Temeke, Mwakilishi wa Inspekta Jenerali wa Polisi, Mwakilishi wa Mkemia Mkuu wa Serikali na Mwakilishi kutoka Ofisi ya Mashtaka nchini.

Uteketezaji huo ulifanyika kuendana na matakwa ya kifungu cha 36(1) cha Sheria ya Kudthibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ambacho kinaruhusu uteketezwaji wa baadhi ya dawa za kulevya kwa kuzingatia hali ya hatari ya dawa hizo,

Kuharibika kwake, athari za mazingira, ufinyu wa mahali maalum pa kuhifadhia au kwa kuzingatia masuala mengine yanayofanana nayo kwa kuwa mirungi hiyo ilikuwa mibichi, kulikuwepo uwezekano mkubwa wa kuharibika na kupoteza uhalisia wake, hivyo ilikuwa muhimu kuteketezwa kwa dawa hizo.

Aidha, mamlaka hiyo imeeleza kuwa, upelelezi wa shauri hili bado unaendelea na utakapokamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani.

MIRUNGI NI NINI?

Kwa mujibu wa DCEA, mirungi ni aina ya dawa ya kulevya inayotokana na mmea unaoitwa “Catha edulis”. Mmea huo una kemikali za cathinone na cathine ambazo huongeza kasi ya utendaji wa mfumo wa fahamu. 

Mirungi ilikuwa inatumika tangu enzi za mababu kwenye nchi za pembe ya Afrika hususani Ethiopia, Eritrea, Kenya, Somalia pamoja na Rasi ya Arabuni nchini Yemen. 

Mirungi hutumika zaidi kwenye mikusanyiko ambayo hujumuisha zaidi wanaume ingawa katika miaka ya karibuni wanawake wamejiingiza katika matumizi. 

Nchini kwetu mirungi hustawi na hupatikana kwa wingi katika mikoa ya Kilimanjaro- Same, Tanga- Lushoto na Arusha Mlima Meru. 

Kiasi kingi cha mirungi huingizwa nchini isivyo halali kutoka nchi jirani ya Kenya ambako ni zao halali la biashara. Mirungi hufahamika kwa majina ya gomba, veve, miraa, kangeta, mkokaa, colombo, asili, mbaga, alenle, nk.

MADHARA YA MIRUNGI

  • Huongeza kasi ya mapigo ya moyo hivyo kuweza kuongeza shinikizo la damu, kiharusi na hata kusababisha kifo.
  • Husababisha vidonda vya utumbo mdogo, saratani ya mdomo, koo na tumbo
  • Husababisha upungufu wa msukumo wa kufanya tendo la ndoa, kumaliza haraka na kutoweza kudumu kwenye tendo la ndoa kwa muda mrefu
  • Hupunguza ubora wa mbegu za kiume na kuvuruga mfumo wa utokaji wake na hata kusababisha ugumba
  • Mtumiaji hukosa usingizi na ulevi ukiisha mwilini husababisha usingizi mzito unaoweza kusababisha ajali hasa kwa madereva
  • Huchochea ukatili, fujo, ugomvi, kuongea sana masuala ya kusadikika na kuhangaika.
  • Mtumiaji hukosa kabisa hamu ya kula na kupungua uzito.
  • Mirungi husababisha upungufu wa maji mwilini na kuleta tatizo la kukosa choo pamoja na ugonjwa wa bawasiri
  • Mtumiaji mirungi akiikosa mirungi hupata uchovu, sonona, hasira za ghafla, kutetemeka, kushindwa kutulia na njozi za kutisha (night mares)
  • Utumiaji mirungi huozesha meno na yale yanayosalia hubadilika rangi, fizi kuuma na harufu ya mdomo.
  • Mirungi huharibu ufanisi wa ini mwilini katika kuchuja sumu za mwili
  • Mirungi huamsha magonjwa ya akili yanayojitokeza kwa vipindi “mwezi mchanga” kwa watumiaji wenye tatizo hilo
  • Wanawake wanaotumia mirungi kipindi cha ujauzito wana hatari ya kupata maumivu ya kifua, kuongezeka kwa mapigo ya moyo na msukumo wa damu
  • Matumizi ya mirungi yanaweza kusababisha kuzaliwa kwa watoto wenye uzito mdogo ambao huweza kukataa kunyonya kutokana na ladha ya maziwa kubadilishwa na viuatilifu vinavyotumika kwenye kilimo cha mirungi
  • Watumiaji mirungi hujikuta wakipenda kuvuta sigara au kunywa pombe wanapokosa usingizi hivyo kudhuru zaidi afya zao.
  • Mtumiaji wa mirungi hutumia fedha ambazo zingekidhi mahitaji ya familia kununulia mirungi hivyo kusababisha migogoro
  • Utafunaji mirungi hutumia muda mwingi na hufanyika muda wa kazi au muda ambao mtumiaji hutakiwa kujumuika na familia yake hivyo kushusha uzalishaji na ukaribu wa familia.

Sheria inasemaje kuhusu mirungi?

Mirungi katika taifa letu ni haramu.

Kujihusisha kwa namna yoyote na mirungi (kulima, kuuza, kuhifadhi, kutumia, nk)ni KOSA LA JINAI na adhabu yake inafikia hadi kifungo cha maisha

Baadhi ya nchi za Ulaya ambazo awali ziliruhusu matumizi ya mirungi zimeanza kuiharamisha baada ya kuona madhara yake

Utamsaidiaje mtumiaji wa mirungi

Mtumiaji anaweza kupunguza kiasi anachotumia taratibu na hatimaye kuacha. Aidha, asasi za kiraia huwasaidia watumiaji kuacha kwa kuwapa unasihi. Nyumba za upataji nafuu ‘sober house’ ambako hupitishwa kwenye hatua 12 za upataji nafuu. Kwa msaada zaidi tembelea tovuti www.dcea.go.tz

Ujumbe kwa jamii

  • Mirungi HAIONGEZI ufanisi kazini, ufaulu katika masomo, udereva wala nguvu za kiume
  • Wazazi na walezi wawalee watoto katika maadili mema ikiwemo kuwa nao karibu na kuwasikiliza
  • Vijana wajifunze na kuzingatia stadi za maisha
  • Epuka kutumia dawa za kulevya pamoja na kujiepusha na makundi hatarishi yanayoweza kukuingiza kwenye utumiaji

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news