NA MWANDISHI WETU
KATIBU Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu, Dkt. John Jingu ametoa rai kwa wakulima kuongeza msukumo katika kilimo chenye tija kwa kutumia mbinu za kisasa za kilimo ambazo zinahusisha teknolojia ili kuleta matokeo mazuri zaidi.
Makatibu Wakuu na Wadau wa Kilimo wakiwa katika Kikao cha Tathimini ya Usimamizi na Ushauri wa Programu ya Kuendeleza Kilimo Awamu ya Pili kilichofanyika Ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu jijini Dar es Salaam.(Picha na OWM).
Wito huo ameutoa katika kikao cha Kamati ya Tathmini ya Usimamizi na Ushauri wa Programu ya Kuendeleza Kilimo Awamu ya Pili kilichohusisha Makatibu Wakuu na Wadau wa Kilimo kilichofanyika Februari 17, 2023 katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Waziri Mkuu jijini Dar es Saalam.
Dkt.Jingu amesema, dhamira ya Serikali ni kuona wakulima wanatumia rasilimali kidogo na kupata faida zaidi.
Aliongezea kuwa, Serikali itaendelea kubuni mbinu mbalimbali za kufanya katika kuimarisha sekta ya Kilimo na Mifugo ili kuongeza ufanisi kwa manufaa ya Taifa.
“Mwelekeo ni kwamba shughuli wanazofanya ziwe na mwelekeo wa kibishara kwa maana kilimo ni biashara na uvuvi ni biashara,” alisema Dkt.Jingu.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Nazael Madalla amesema uvuvi wetu bado tunatumia mbinu za zamani, lakini sasa tunaenda kutoa boti mpya za kisasa zitakazofanya wavuvi waongeze tija.
Ameongeza kusema kuwa, jitihada hizo zinaenda sambamba na kutoa mikopo kwa wafugaji wa samaki kwenye vizimba katika ziwa Viktoria kwa kuwapatia vizimba vya samaki na vifaranga vya samaki na chakula cha samaki.
Dkt. Salim Nandonde Mratibu wa Taifa, wa Programu ya kuendeleza Kilimo Awamu ya Pili akitoa wasilisho wakati wa Kikao cha Tathimini.
“Lengo ni kuongeza uzalishaji wa samaki na kutimiza malengo tuliyopewa na Mhe. Rais wa kuongeza tani za uzalishaji wa samaki ifikapo Mwaka 2026,” alisema Dkt.Madalla.
Aidha, Serikali itaenda kutoa mikopo kwa wakulima wa zao la Mwani katika ukanda wa Pwani ili waweze kununua vifaa na waweze kuongeza uzalishaji wa zao la Mwani.
"Tunaimani zao hili litakuwa na mchango mkubwa sana katika kuinua kipato na kuboresha maisha hasa kwa wakina mama ambao ndiyo wakulima wakubwa wa zao la Mwani na vyote hivi ni katika utekelezaji wa Usimamizi na Ushauri wa Programu ya Kuendeleza Kilimo Awamu ya Pili,"alisisitiza Dkt. Madalla.
Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Dkt. Maduhu Kazi amesema Mpango wa Usimamizi na Ushauri wa Program ya Kuendeleza Kilimo Awamu ya Pili ni mpango jumuishi unaohusisha wizara kupitia Jeshi la Magereza na Jeshi la Polisi ambayo yanajihusisha na shughuli mbalimbali za kilimo na uwekezaji.