Hii hapa sura mpya ya Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA)

NA DIRAMAKINI

KAMATI YA Utendaji ya Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), iliyochaguliwa Februari 5, 2023, ilifanya kikao chake cha kwanza chini ya Mwenyekiti Amir Mhando Jumapili Februari 12, 2023 na kukubaliana mambo mbalimbali kama ifuatavyo:

(A) Mafunzo kwa waandishi wa habari za michezo

Kikao kilichukulia uzito mkubwa suala la kuwajengea uwezo waandishi wa habari za michezo, hivyo kikao kimeielekeza sekretarieti ya TASWA iandae utaratibu wa mafunzo ya mara kwa mara jijini Dares Salaam na mikoani.

Kuhakikisha suala la mafunzo linapewa kipaumbele na ni jambo endelevu kwa waandishi wa habari za michezo kuanzia ngazi ya wahariri, waandishi waandamizi pamoja na waandishi chipukizi, Kamati ya Utendaji imemteua Dk. Egbert Mkoko, ambaye ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kuwa Mwenyekiti wa Kamati
ya Mafunzo na Maadili ya TASWA.

Mkoko ni mtangazaji wa zamani wa Redio Free Afrika, Star Tv, Redio Mlimani na Mlimani Tv. Katibu wa Kamati atakuwa Imani Makongoro, ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa TASWA.

Pia kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa hivi karibuni na Alfred Lucas ambaye ni Katibu Mkuu wa TASWA,kamati imemteua Dk. Dominick Nkolimwa, ambaye ni Mhadhiri wa Chuo cha Ustawi wa Jamii (ISW) Dar es Salaam, akiwa ni Mkuu wa Idara ya Utafiti na Ushauri Weledi ya chuo hicho kuwa Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo. Dk. Nkolimwa na Dkt. Mkoko wote ni wanachama wa TASWA.

Wajumbe ni waandishi nguli nchini Salim Said Salim, Abdallah Majura, Frank Sanga,Mgaya Kingoba, Benny Kisaka, Mahmoud Zubeiry, Sued Mwinyi, Rashid Kejo, Saleh Ally, Beda Msimbe, Nasongelya Kilyinga, Mbonile Burton na Jennifer Sumi.

Kamati hiyo ya Mafunzo na Maadili kwa kushirikiana na Kamati ya Utendaji, pia wataandaa ziara za mafunzo kwa wanahabari wa michezo katika maeneo mbalimbali nchini na nje ya nchi.

(B) Rasimu ya Katiba ya TASWA

Kikao kilijadili suala la kumalizia mchakato wa mabadiliko ya Katiba ya TASWA,ambayo tayari ilishawasilishwa na uongozi uliopita kwa Msajili wa Klabu na Vyama vya Michezo nchini na kutoa maelekezo ya baadhi ya maeneo ya kufanyiwa marekebisho.

Kutokana na hali hiyo, uongozi umelifanyia kazi jambo hilo na kuunda Kamati ya Katiba, ambapo Mwenyekiti ataendelea kuwa Boniface Wambura ambaye amewahi kuwa Mwenyekiti wa TASWA na kitaaluma pia ni mwanasheria na Makamu Mwenyekiti atakuwa Abdul Mohammed aliyepata kuwa Katibu Mkuu wa TASWA.

Wote walikuwa Kamati ya Katiba iliyopita. Wajumbe ambao wote ni wapya ni Ibrahim Bakari, Frank Balile, Issa Ndokeji, Godfrey Lutego, ambaye pia ana taaluma ya sheria, Anna Mwikola, Kepteni Seif Ngowi, Mbwana Shomary, Sophia Ashery, Ezekiel Mwambopo na Thomss ‘Tom’ Chilala, ilihali Katibu wa Kamati hiyo atakuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TASWA, Nasongelya Kilyinga.

(C) Ukaguzi wa hesabu za TASWA

Kikao kilikubaliana ili kusimamia vizuri mfumo wa hesabu za chama, lazima ufanyike ukaguzi wa hesabu za chama, hivyo iwepo Kamati ya Ukaguzi ambayo itaongozwa na mtaalamu wa masuala ya fedha na utawala na itakuwa muongozo kwa chama kuhusu masuala yanayohusu usimamizi wa fedha.

Kutokana na hali hiyo, Kamati ya Utendaji ya TASWA, imemuomba CPA Baraka Katemba, ambaye ni Meneja wa Fedha na Utawala wa Ofisi ya Hakimilki Tanzania (COSOTA) kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ukaguzi ya TASWA. Wajumbe wake ni Kazumari Ibrahim Mfaume ambaye ni Mtathmini wa Benki ya NMB-Makao Makuu Dar es Salaam, Charles Reuben Mtekateka, ambaye ni Mhasibu Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) na Domina Rwemanyila, mtangazaji wa zamani wa Redio Tumaini Dar es Salaam na kwa sasa ni mtumishi wa Shirika la Nyumba (NHC). Katibu wa Kamati atatokana miongoni mwa wajumbe wanaounda Kamati ya Ukaguzi.

(D) Tuzo za TASWA

Kikao kilikubaliana TASWA irejeshe tuzo za za kila mwaka kwa kuwazawadia wanamichezo waliofanya vizuri kwa kila mchezo unaotambuliwa na Baraza la Michezo nchini (BMT), lakini lazima awe amefanya mashindano ya kitaifa yanayotambulika rasmi kwa mwaka unaotolewa tuzo.

Tayari Kamati ya Tuzo za TASWA imeshaundwa ikiwa na waandishi mbalimbali wa habari za michezo pamoja na baadhi ya wachambuzi nguli wa habari za michezo. Kamati itatangazwa wiki ijayo baada ya wajumbe kuthibitisha uteuzi.

(E) Kamati ya Fedha na Mipango

Ili kurahisisha masuala mbalimbali, Kamati ya Utendaji imeunda Kamati ya Fedha na Mipango, ambayo itashirikiana na Kamati ya Utendaji katika kutekeleza majukumu yaliyopangwa.

Kamati hiyo itaongozwa na Mwenyekiti, CPA Shija Richard, ambaye ni mwandishi wa habari wa zamani magazeti mbalimbali nchini, lakini kwa sasa ni Meneja Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Katibu wa Kamati ni Mhazini Mkuu wa TASWA, Dina Ismail. Wajumbe wa Kamati hiyo ni Ramadhani Mbwaduke, George John, Enock Bwigane,Victor Robert Willy, Zena Chande, Jamal Hashim, Mussa Juma, Christina Koroso, Sauli Gilliard, Mashaka Mhando na Masau Bwire.

(F) Media Day Bonanza

Kikao kilijadili tukio lililokuwa linafanywa zamani na TASWA kuwakutanisha pamoja waandishi wa habari na wafanyakazi wa vyombo vya habari, tukio maarufu kama Media Day Bonanza. Jambo hilo linatengenezewa mikakati na muda si mrefu taarifa yake itatolewa.

(G) Waandishi Wanawake na Michezo

Suala la kuwawezesha waandishi wa habari za michezo wanawake pia limetiliwa mkazo na limewekewa mikakati yake, ambapo kikao kimeunda Kamati ya Wanawake, itakayokuwa chini ya Imani Makongoro, ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa TASWA.

Katibu wa Kamati atakuwa Timzoo Kalugira ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TASWA. Wajumbe ni Somoe Ng’itu, Victoria Mungule, Editha Mayemba, Lilian Timbuka, Grace Mkojera, Donisya Thomas, Jane John, Victoria Godfrey, Lightness Sirikwa na Speciroza Joseph.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news