NA DIRAMAKINI
KLABU ya Yanga ya jijini Dar es Salaam imefanikiwa kubakiza alama tatu za kwanza nyumbani, kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.
Ni baada ya kuifunga TP Mazembe mabao 3-1 kupitia mtanange uliopigwa katika dimba la Benjamin Mkapa lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.
Kupitia mtanange huo wa leo Februari 17, 2023 mabao ya Yanga SC yamewekwa nyavuni na mshambuliaji Kennedy Musonda dakika ya saba, kiungo Mudathir Yahya dakika ya 11 na winga Tuisila Kisinda dakika ya 90.
Aidha, kwa upande wa bao pekee la TP Mazembe la kufutia machozi limefungwa na Alex Ngonga ambaye alipiga mpira wa adhabu na kutinga nyavuni.
Klabu ya Yanga SC imepata alama tatu za kwanza katika kundi hilo baada ya kuchapwa 2-0 kwenye mechi ya kwanza wiki iliyopita na wenyeji, Monastir nchini Tunisia, wakati Mazembe inapoteza mechi ya kwanza ikitoka kushinda 3-1 nyumbani dhidi ya Real Bamako ya Mali.
Mechi nyingine ya Kundi D leo, Real Bamako imelazimishwa sare ya 1-1 na Monastir huko mjini Bamako nchini Mali.
Monastir inaendelea kuongoza kundi hilo kwa pointi zake nna ikifuatiwa na Yanga na Mazembe zenye pointi tatu kila moja, wakati Real Bamako yenye alama moja inashika mkia.
Ikumbukwe kuwa, mchezo Februari 18, 2023 Simba SC ya jijini Dar es Salaam katika mchezo wao wa pili wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Raja Casablanca kutoka Morocco uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa ulimalizika kwa kupoteza mabao 3-0.
Simba SC walianza mchezo kwa kasi kutafuta bao la mapema, lakini Raja walikuwa makini huku wao wakifanya mashambulizi ya kujibu kila wanapopoteza mpira.
Hamza Khabba aliwapatia Raja bao la kwanza dakika ya 30 kwa shuti kali nje kidogo ya 18 baada ya kugongeana pasi kutoka katikati ya uwanja.
Kipindi cha pili, Simba SC ilirudi kwa kasi wakimiliki mpira zaidi, lakini Raja waliziba mianya yote huku wao wakiendelea kufanya mashambulizi ya kujibu.
Sofiane Benjdida aliwapatia Raja bao la pili dakika ya 83 baada ya kumalizia pasi safi kutoka kwa Bentayg.
Dakika mbili baadae mlinzi wa kati wa Raja Ismail Mukadem aliwapatia bao la tatu kwa mkwaju wa penati baada ya mlinzi Joash Onyango kucheza madhambi ndani ya 18.
Kwa matokeo hayo, wanufaika wa fedha za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan ambaye aliahidi kununua kila bao kwa shilingi milioni 5 kwa wawakilishi hao wa Kimataifa, kwa maana ya Simba na Yanga SC ni Yanga ambao watapata shilingi milioni 15 huku Simba ikiambulia shilingi 0.
Mechi zijazo, Februari 26, mwaka huu Yanga watakuwa wageni wa Real huko mjini Bamako na TP Mazembe watawakaribisha Monastir mjini Lubumbashi huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.