Jamii yatakiwa kushirikiana na walimu kuinua taaluma

NA MWANDISHI WETU

JAMII imetakiwa kutoa ushirikiano kwa walimu ili kuleta ufanisi utakaochangia kuboresha taaluma ya wanafunzi wa madarasa ya awali na la kwanza kwenye shule za msingi za umma.
Kauli mbalimbali zimetolewa Februari 14,2023 na walimu wanaoshiriki mafunzo ya kuwajengea uwezo na mbinu za ujifunzaji na ufundishaji KKK yanayotolewa na Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania wilayani Nkasi.

Shule Bora ni programu ya serikali inayolenga kuinua ubora wa elimu jumuishi,mazingira salama ya kujifunzia kwa wasichana na wavulana kwenye shule za umma nchini Tanzania na inafadhiliwa na Shirika la Misaada la Uingereza (UKaid) kutoka Serikali ya Uingereza.

Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Kirando iliyopo Nkasi Gerald Kossamu amesema wazazi na serikali wanatakiwa kuungana kuondoa tatizo la uhaba wa vyumba vya madarasa na upungufu wa walimu unaoathiri ufundishaji.
Kossamu alisema shule yake ina changamoto ya wingi wa wanafunzi ambapo hadi kufikia (jana ) Februari 13 mwaka huu shule imeandikisha jumla ya wanafunzi wa elimu ya awali 443 na wanafunzi 601 wa darasa la kwanza.

“Msongamano ni mkubwa madarasani ambapo shule ina wanafunzi 3,174 na walimu 23 ambao hawatoshi . Walimu inawawia ugumu katika ufundishaji hata namna ya kudhibiti utoro.Serikali itusaidie madarasa ya kutosha,” alisema Mwalimu Kossamu.


Happiness Aristides ni mwalimu wa taaluma toka shule ya msingi Mteta iliyopo Laela, halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga alisema wazazi na walezi washirikishwe ili waweze kudhibiti utoro wa watoto unaochangia kufeli masomo.

Happiness aliongeza kusema watoto wanastahili kupendwa na kusaidiwa ili wa waone umuhimu wa kujifunza na kuzingatia masomo hususan walio madarasa ya awali na darasa la kwanza ndio maana mafunzo kwa walimu ni muhimu.
Kuhusu manufaa ya mafunzo ya programu ya Shule Bora ,mwalimu Happiness alisema yamemsaidia kujiamini kwa kupata mbinu stahiki za kufundisha madarasa ya awali.

Kwa upande wake Mratibu wa Programu ya Shule Bora Tanzania toka Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) Mwesiga Kabigumila alisema lengo la mafunzo kwa viongozi hao wa walimu ni kuwajengea mbinu na uwezo wa kumudu na kutambua tabia za wanafunzi na jinsi ya kuwahudumia.

Mwesiga aliongeza kusema kumekuwepo na tatizo la utolewaji wa taarifa zisizo za uhakika au uhalisia toka kwa walimu na baadhi ya wasimamizi wa elimu hatua inayopoelekea serikali au mradi kushindwa kutambua shida za watoto kutomudu KKK.

“Ni bora walimu wakuu, wasimamizi wa shule na maafisa elimu kujikita katika utoaji taarifa sahihi ili kusaidia taifa na mradi wa Shule Bora kuweka mikakati ya suala la ujifunzaji na ufundishaji KKK,” alisisitiza Mwesiga.
Programu ya Shule Bora imeendesha mafunzo ya uboreshaji wa ufundishaji na ujifunzaji wa darasa la awali, la kwanza na la pili ambapo leo ilikuwa zamu ya kundi la pili walimu wakuu, walimu wa taaluma, waratibu elimu kata na waelimisha rika toka shule arobaini (40) za msingi za mkoa wa Rukwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news