NA MWANDISHI WETU
NAIBU Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete ameitaka Bodi ya Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) kuhakikisha miradi yote inayotekelezwa na kampuni hiyo inakamilika kwa wakati na kuzingatia thamani ya fedha.
Naibu Waziri wa Uchukuzi Atupele Mwakibete (kushoto) akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni za Huduma za Meli Tanzania (MSCL) Erick Hamisi, wakati wa zoezi la ushushwaji wa meli ya Mv. Mwanza katika Ziwa Victoria, jijini Mwanza.
Naibu Waziri Mwakibete ametoa kauli hiyo jijini Mwanza wakati wa hafla ya ushushaji wa meli ya MV Mwanza hapa kazi tu ambayo ujenzi wake kwa sasa umefikia asilimia 82.
Naibu Waziri Mwakibete amesema Serikali itaendelea kuwekeza katika sekta ya usafiri wa majini kupitia ujenzi wa meli katika Ziwa Viktoria na Tanganyika lengo likiwa kurahisisha usafiri na usafirishaji na kuchochea uchumi wa mikoa inayozunguka maziwa hayo na nchi jirani.
“Ujenzi wa meli hizi umekuja wakati muafaka sababu tuna bidhaa nyingi zinazolimwa katika mikoa iliyoko katika maziwa haya, lakini nchi Jirani pia zina bidhaa nyingi ambazo wanahitaji kuzileta Tanzania na sisi kupeleka za kwetu, hivyo kukamilika kwa meli hii na nyingine zilizopangwa kujengwa kutachagiza sana biashara,”amesema Naibu Waziri Mwakibete.
Muonekano wa Meli mpya ya Mv Mwanza “Hapa kazi tu” inayojengwa na kampuni za Gas Enter Ship-Building Engineering na Lang Nam Corporation za nchini Korea, baada ya kushushwa katika Ziwa Viktoria jijini Mwanza.
Naibu Waziri Mwakibete ametumia nafasi hiyo kuwataka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kuhakikisha inaboresha gati kwenye bandari ambazo meli hiyo itafanya safari zake ili kutokwamisha utoaji wa huduma wakati meli hiyo itakapokamilika.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Adam Malima, amesma kukamilika kwa meli hiyo kutawaunganisha wananchi wa Mkoa wa Kagera, Gaita, Musoma, Simiyu Kenya na Uganda kupitia Ziwa Viktoria kwani wataweza kutoka eneo moja kwenda jingine kwa haraka na hivyo kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa MSCL, Eric Hamis ameishukuru Serikali kwa kuona umuhimu wa Kampuni hiyo kuwa na meli mpya na kukarabati zilizopo kwani matokeo ya miradi hiyo itachangia kukua kwa pato la Kampuni, Mkoa na Taifa kwa ujumla.
Eric amemuhakikishia Naibu Waziri Mwakibete kuwa tayari kampuni kupitia wataalam wake inasimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi yote ya ujenzi na ukarabati wa meli ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kulingana na mikataba iliyowekwa.
Meli ya MV Mwanza Hapa Kazi tu inajengwa na kampuni za Gas Enter Ship-Building Engineering na Lang Nam Corporation za nchini Korea na ujenzi wake umegharimu kiasi cha shilingi bilioni 109 na kukamilika kwake kunatarajia kutoa huduma katika bandari za Kagera, Kemondo, Mwanza, Musoma, Port Bell na Jinja nchini Uganda pamoja na Kisumu Nchini Kenya.