Karibu Balozi Dkt.Chana

NA ELEUTERI MANGI-WUSM

REJEA mabadiliko madogo ya Bazara la Mawaziri aliyofanya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Februari 14, 2023 ambapo alimteua Mhe. Balozi Dkt. Pindi Hazara Chana kuwa Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo na kumuapisha Februari 15, 2023 Ikulu jijini Dar es salaam kushika wadhifa huo mpya akitokea Wizara ya Maliasili na Utalii.
Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa sasa kipenga kimepingwa ikiwa imepata Waziri Mpya Mhe. Balozi Chana, mwanadiplomasia na mwanasiasa ambaye anaendelea kuongoza sekta alizowahi kuhudumu ndani na nje ya nchi yetu.

Akiongea mara baada Viongozi wapya kuapishwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Ikulu jijini Dar es Salaam, Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Mpango amewasisitiza viongozi hao kuwa wanajua maadili ya kiserikali na kuwahimiza washirikiane na kubadilishana uzoefu ili kufikia malengo ya hayo.

Makamu wa Rais Dkt. Mpango amesema takwimu zinaonesha sekta ya Utamaduni inakua kwa kasi kuliko sekta zote nchini na inaajiri vijana wengi ambao ni tegemeo la taifa kesho.

“Mhe. Pindi Chana ukaitendee haki, vijana wetu wanategemea sana hiyo sekta…Uwe na mashirikiano kati yako wewe na watendaji, mkae kama timu moja ya kuwaletea maendeleo Watanzania,” amesema Dkt. Mpango.

Je, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana ni nani?

Yeye ni mbobezi katika masuala ya Sheria mwenye Shahada ya Uzamivu (PhD) ya Sheria ya Chuo cha Mzumbe kuanzia 2010 hadi 2013, Shahada ya Uzamili ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (LL.M) kuanzia mwaka 2001 hadi 2003 na Shahada ya Kwanza ya Sheria (LL.B) mwaka 1994 hadi 1991 Chuo Kikuu cha Peoples Friendship (Lumumba), Moscow nchini Russia.

Kama hilo halitoshi Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amehudumu Ubunge katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa awamu tatu, mwaka 2005 hadi 2010, 2010 hadi 2015 na kuanzia 2020 hadi sasa. Nafasi hii ya Ubunge ndiyo imefungua njia kwa Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana kuaminiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan na kumpa dhamana ya kuongoza wizara kadhaa na sasa yupo katika Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Kabla ya uteuzi huo, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amehudumu katika nafasi kama hiyo katika Wizara za Maliasili na Utalii kabla ya hapo alikuwa Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge).

Hadi sasa ni Mjumbe wa Kamati ya Katiba na Mambo ya Sheria, Wizara ya Mambo ya Katiba na Sheria, eneo ambalo anatumia vema taaluma yake ya Sheria. Bila ya kusahau ameiwakilisha nchi yetu nchini Kenya akiwa Balozi kuanzia mwaka 2017 hadi 2020.

Aidha, Mhe. Waziri Balozi Dkt. Pindi Chana amekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba, Haki na Utawala Bora kuanzia mwaka 2010 hadi 2014, Mjumbe wa Baraza la Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya kuanzia mwaka 2012 hadi 2013, Mjumbe wa Baraza la Sanaa la Taifa kuanzia mwaka 2009 hadi 2013 na Kamishna wa Tume ya Pamoja ya Fedha kuanzia mwaka 2009 hadi 2013.

Kalamu yangu haiwezi kusahau kuwa yeye ni miongoni mwa Wanasiasa wanawake Tanzania, amewahi kufanyakazi ya kusimamia taasisi za elimu nchini akiwa Mjumbe wa Baraza la Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili kuanzia mwaka 2008 hadi 2013 na Mjumbe wa Baraza la Chuo cha kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kuanzia mwaka 2009 hadi 2010.

Kwenye diplomasia, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amewahi kuwa Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania wa Umoja wa Mataifa Nairobi, nchini Kenya katika Shirika la Umoja wa Mataifa la Makazi (UN Habitat) na Mazingira (UNEP) mwaka 2017 na Katibu wa Chama Cha Mapinduzi Mahusiano ya Kimataifa 2016 na Mwenyekiti wa Mabalozi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Nairobi nchini Kenya kuanzia mwaka 2019 hadi 2020.

Kazi alizofanya Waziri Balozi Dkt. Pindi Chana zinamfanya awe na mawanda mapana ya kiuongozi ndiyo maana anapewa Wizara mbalimbali kutekeleza majukumu yake.

Waziri huyu ni mfano wa kuigwa, anauzoefu wa kufanya kazi kuanzia ngazi ya chini ambayo ndiyo imekuwa njia mwafaka ya kuijua Serikali na kuitumikia kwa moyo wake wote.

Alifanya kazi ya kuwa Mwanasheria wa Elimu ya Utafiti na Utunzaji wa Mazingira Tanzania Mwaka 2000 hadi 2010, Afisa Sheria wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa kuanzia 2000 hadi 2005.
Vile vile amefanyakazi katika Kampuni ya Sheria ya Uingereza akiwa Katibu mwaka 1997 hadi 1999, amefanyakazi katika Benki ya Barclays, Uingereza mwaka 1995 hadi 1998, kampuni ya Cocacola Co. Ltd. mwaka 1996 hadi 1997na Mtangazaji wa Benki ya Urusi mwaka 1994 hadi 1995.

Huo ni umahiri mkubwa wa uongozi wa Mhe. Waziri Balozi Dkt. Pindi Chana, hakika huyu ni nguli na mbobezi katika masuala ya Sheria ndiyo maana kazi anazofanya zinasadifu uadilifu wake kwa taaluma yake na Taifa lake.

Kwa heshima zote mwandishi wa Makala haya anamtakia kazi njema Waziri Balozi Dkt Pindi Chana katika majukumu yake mapya ili kuwahudumia Watanzania katika Sekta hizo tatu yaani Utamaduni, Sanaa na Michezo bila kumsahau Katibu Mkuu mpya wa wizara hiyo ndugu Saidi Othuman Yakubu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news