Kiagata Zone watoa msaada wa madawati wilayani Butiama

NA DIRAMAKINI

UMOJA wa Maendeleo wa Kiagata Zone umetoa msaada wa madawati hamsini kwa ajili ya kusaidia shule mbili za msingi ikiwemo Shule ya Kiagata na Nyamihuru zilizopo Wilaya ya Butiama mkoani Mara ikiwa ni hatua ya kuunga mkono juhudi za Serikali za kusaidia kuimarisha sekta ya elimu.
Umoja huo, wa Kiagata Zone ni kikundi kilichoanzishwa na vijana wazawa wa Tarafa ya Kiagata kwa lengo la kuongeza nguvu ya kimaendeleo ndani ya kata zote zilizopo katika tarafa hiyo.

Madawati hayo yametolewa Februari 13, 2023 na mwenyekiti wa umoja huo,Robert Maganya akiwa ameongozana na makamu mwenyekiti wa umoja huo, Ismail Massaro ambapo kila shule imepata mgao wa madawati 25.
Madawati hayo yatapunguza changamoto kwa wanafunzi 150 waliokuwa wakikaa chini pindi wanapokuwa wakiendelea na masomo yao darasani.

Maganya amesema, madawati hayo ni imara na yametengenezwa kwa kuzingatia viwango vya hali ya juu na kila dawati moja limegharimu kiasi cha shilingi 70,000 na amewaomba walimu kuwahimiza wanafunzi kuyatunza madawati hayo ili yaweze kudumu kwa muda mrefu.

Pia mwenyekiti huyo amewasisitiza wazazi na wananchi kuongeza juhudi binafsi za kusukuma maendeeo mbele zaidi na sio kuitegemea Serikali peke yake kwani maendeleo hayo yataleta manufaa kwa jamii nzima.

Naye Makamu mwenyekiti wa umoja huo Ismail Massro amewaomba wazazi na wakazi wa tarafa hiyo kujitokeza kwa wingi kujiunga ndani ya umoja huo wenye lengo la kuleta maendeleo zaidi ndani ya Tarafa ya Kiagata kupitia sekta mbalimbali.
Nao walimu wakuu wa shule zote mbili wameushukuru umoja huo wa 'Kiagata Zone' kwa hatua hiyo njema ya kusaidia madawati kwani utawafanya wanafunzi wasome kwa ufanisi.

Wameomba isiwe mwisho kutoa msaada huo kwani inasaidia kuongeza chachu ya elimu kwa watoto na mahudhurio bora kwa wanafunzi ambao awali walishindwa kuhudhuria kwa ufanisi kutokana na kuhofia kukaa chini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

1 Comments

Previous Post Next Post

International news