Kliniki za ardhi ziendelee nchini-Waziri Dkt.Mabula

NA GODFREY NNKO

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa Dkt.Angeline Mabula amewataka wananchi kuendelea kuzitumia vema Kliniki za Ardhi ili kero zao ziweze kupatiwa ufumbuzi popote pale walipo nchini.

Hivi karibuni wizara hiyo ilianzisha kliniki za ardhi ambazo wataalam wote wanakutana sehemu moja na wananchi wanafika kusikilizwa kero zao ikiwa ni zoezi endelevu.

Ameyasema hayo Februari 14, 2023 wakati akifungua Mkutano wa Pili wa Wadau wa Sekta ya Ardhi nchini katika Ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo wa pili, umeongozwa na kauli mbiu ya "Usimamizi bora wa ardhi kwa maendeleo endelevu ya biashara na Uwekezaji nchini".

"Kliniki za Ardhi hizi zimekuwa zikifanyika katika maeneo mengi nchini, lengo ni kuwa karibu na mteja kusikiliza changamoto za wananchi na kuzipatia ufumbuzi. Kliniki hizi zinapofanyika zinakuwa na wataalamu wote wa sekta zote kwenye wizara husika.

"Lolote ambalo mwananchi anakuwa nalo linapatiwa ufumbuzi na nitoe rai kliniki hizi ziendelee, zimeonekana zina mafanikio makubwa katika ufumbuzi. Mlikotoka, mnaposikia kuna kliniki muende mpate fursa ya kuona na kujua wanafanya nini,"Mheshimiwa Waziri Dkt.Mabula amewaeleza wadau hao.

Mheshimiwa Waziri Dkt.Mabula amesema, mkutano huo wa Ministerial Public Private Dialogue (MPPD) ni wa pili toka ameteuliwa kuwa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kukutana na wadau wa Sekta ya Ardhi ndani ya mfumo wa majadiliano wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC).

Amesema, mkutano huo ni mwendelezo wa utekelezaji wa maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Biashara, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan,ambayo aliyatoa kwenye Mkutano wa 13 wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) uliofanyika Juni 7,2022.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news