NA DIRAMAKINI
WAKATI Serikali kupitia Wizara ya Utamaduni,Sanaa na Michezo ikiwa katika mchakato wa kupata vazi la Taifa ambapo imewataka watanzania kuendelea kutoa mapendekezo kuhusu aina ya vazi, hatimaye Watanzania wamezidi kuonesha mwitikio.
Miongoni mwao ni Johannes Braison Mariki ambaye ametoa pendekezo lake kuhusu vazi la taifa huku msisitizo ukiwa ni vazi litokanalo na pamba.
Pamba inapatikana?
Kwa mujibu wa Bodi ya Pamba Tanzania (TCB), wakulima wa pamba ni wadau wakuu katika sekta ndogo ya pamba huku mchango wao ndio unaotegemewa zaidi kuiinua tasnia ya pamba.
Pamba inalimwa na wakulima wadogo wenye mashamba ya ukubwa wa kuanzia ekari 1 hadi ekari 10.
Sehemu kubwa ya wakulima hutumia jembe la kokotwa na wanyama kazi na jembe la mkono huku sehemu ndogo wakitumia trekta kuandaa mashamba.
Idadi ya Wakulima
Wakulima wa pamba Tanzania wanakadiriwa kufikia 600,000 waliotapakaa katika mikoa takribani 17 iliyogawanyika katika kanda mbili (Kanda ya Magharibi na Mashariki) nchi nzima.
Wakulima wa mikoa hii yote 17 inayolima pamba pamoja na ukweli kwamba wanalima mazao mengine wanategemea zao la pamba kama zao lao kuu la biashara.
Familia nyingi zimeweza kujikwamua kutoka katika lindi la umaskini na kuweza kujitosheleza kwa chakula na mahitaji mengine ya msingi kutokana na uwepo wa zao la pamba.
Tasnia ya pamba imeendelea kukua na kuimarika kutokana na uwepo na kuongezeka kwa wakulima na eneo la kilimo.
Miongoni mwa ongezeko la wakulima kuwahi kushuhudiwa hivi karibuni ni kuanza kwa uzalishaji katika mikoa ya Dodoma na Katavi ambayo pekee inakadiriwa kuwa na jumla ya wakulima wapya 30,000 kwa mujibu wa takwimu za msimu wa kilimo wa 2018/19.
Tija
Wakulima wana jukumu kubwa la kuimarisha tija katika uzalishaji wa zao la pamba kwa kuwa wao ndio wamiliki na walezi wakuu wa zao kabla ya mdau mwingine yeyote katika tasnia ya pamba.
Kutokana na umuhimu wao aina budi wawezeshwe ili kuweza kutimiza azma hiikwa lengo la kuikuza sekta ya pamba.
Tija katika zao la pamba inakadiriwa kuwa kilogramu 300 kwa ekari moja, takwimu ambazo zipo chini sana kulinganisha na uwezo halisia unaoweza kufikiwa na mkulima endapo atapata huduma toshelevu za ugani na kuzingatia kanuni za kilimo bora kwa usahihi
Pembejeo
Pembejeo kuu muhimu kwa wakulima nchini ni mbegu na viuatilifu na mbolea za viwandani kwa kiwango kidogo sana.
Matumizi ya pembejeo yamekuwa ya chini kwa miaka mingi kutokana na wakulima kukosa uwezo wa kumudu gharama za pembejeo hizo hasa viuatilifu na mbolea.
Mfumo wa ukopeshaji wa pembejeo umeweza kuamsha na kuongeza hali ya matumizi ya pembejeo (viuatilifu) kwa wakulima kwa takribani 80% ndani ya misimu mitatu.
Kutoka ekapaki 1,050,000 msimu wa 2015/16 hadi kufikia ekapaki 6,090,000 msimu wa kilimo 2018/19.
Pamoja na ongezeko la matumizi ya mbolea za viwandani zinatumika kwa kiwango cha chini kutokana na gharama na vilevile kutokuwepo kwa elimu ya kutosha juu ya umuhimu namatumizi sahihi ya mbolea
Mifumo ya Uendeshaji Kilimo
Katika kujisimamia wakulima wa pamba wamepitia vipindi/mifumo mikuu miwili tofauti katika juhudi za kutafuta upi ni mfumo ambao utawaongezea tija ya kilimo wanachofanya.
Mifumo hiyo ni Ushirika na Kilimo cha Mkataba,mfumo wa awali wa ushirika ndio uliweka msingina kuimarisha sekta ya pamba tangu ilipoanza kulimwa chini ya usimamizi wa serikali baada ya kupata uhuru kwa Tanganyika 1961.
Mfumo wa kilimo cha mkataba ulikuja kwa lengo la kuchochea tija kupitia ongezeko la matumizi ya pembejeo na kuongeza ushirikiano na ushirikwashaji kikamilifu zaidi wa wadau wakuu wa zao hili ambapo mchambuaji/mwekezaji alimpatia pembejeo mkulima kwa mkopo na mkulima anauza pamba yake kwa mwekezaji.
Hali ya usimamizi ya sasa imeimarishwa kwa serikali kuurejesha mfumo wa ushirika kwa lengo la kuwafanya wakulima wawe na nguvu zaidi ya kimaamuzi kwa kuwaleta pamoja na kupitia vyama vya msingi vya kilimo na masoko –AMCOS zaidi ya 1,400 kujiongezea tija na kipato.
Soko
Pamba inayolimwa Tanzania inategemea zaidi soko la nje (export) kwa asilimia 60% na 40% inatumiwa na viwanda vya ndani. Soko la pamba bado lina mahitaji makubwa zaidi kuliko uzalishaji uliopo kwa sasa ambapo kwa mwaka unakadiriwa kufikia marobota 300,00.
Wakulima wote wa pamba uuza pamba yao kupitia vyama vyao vya msingi “AMCOS” ambayo navyo vina jukumu la kuiwasilisha pamba iyo kwa mchambuaji baada ya hatua za manunuzi kukamilika.
Kiwango cha pamba tunachozalisha bado ni kidogo sana hali inayopelekea tukose nguvu ya kuwa na ushawishi wa bei katika soko la kimataifa.
Wakulima wa Tanzania ni wapokeaji tu wa bei inyopendekezwa katika soko la dunia,lakini serikali mara zote imekuwa ikifanya jitihada bei anayopokea mkulima iendane na gharama za uzalishaji za mkulima ili kupata faida na vilevile aendelee kuwa na uwezo wa kuhudumia zao.
Soko bado lina uhitaji mkubwa wa pamba ya Tanzania kutokana na sifa ya kuwa na matumizi madogo ya viuadudu na mbolea ivyo kuifanya sifa zake kukaribiana na pamba inayolimwa kwa kufuata taratibu za kilimo hai.