Kwa nini mitume na manabii Tanzania wana imani kubwa na Rais Dkt.Nabiijoshua Aram Mwantyala?

NA DIRAMAKINI

MWENYEKITI Umoja wa Mitume na Manabii Tanzania (UMMT) Wilaya ya Moshi Mjini mkoani Kilimanjaro, Apostle Goodluck amesesema, Rais wa UMMT, Dkt.Nabiijoshua Aram Mwantyala na jopo lake la uongozi wataendelea kuwaunga mkono kwa maombi, hali na mali ili kuhakikisha umoja huo unastawi zaidi.

Dhamira ya umoja huo ambao unalenga kuwaleta pamoja mitume na manabii kwa ajili ya kueneza habari njema ya neno la Mungu nchini, kuombea, kuwezeshana, kuwezesha wenye mahitaji mbalimbali pia umekusudia kushirikiana na Serikali kuhakikisha wanatekeleza miradi ya maendeleo kwa manufaa ya jamii na Taifa kwa ujumla.

Hivi karibuni,Dkt.Nabiijoshua Aram Mwantyala ambaye ni Kiongozi Mkuu wa Huduma ya Sauti ya Uponyaji Tanzania alitwaa asilimia 80 ya kura katika uchaguzi wa nafasi ya urais katika Umoja wa Manabii na Mitume nchini Tanzania (Unity of Apostles and Prophets Tanzania).

Ushindi huo ulitokana na kura 179 alizopata huku akiwaacha mbali washindani wake akiwemo Mchungaji Ceasar Masisi aliyepata kura 42 na Mtume Joackim Kimanza aliyepata kura nne kupitia uchaguzi uliofanyika katika Ukumbi wa Anatoglo uliopo Ilala, Dar es Salaam.

Kwa matokeo hayo, Askofu Profesa Rejoice Ndalima alimtangaza rasmi Dkt.Nabiijoshua Aram Mwantyala kuwa Rais wa Umoja wa Mitume na Manabii nchini Tanzania.

Aidha, mitume na manabii mbalimbali nchini walionesha imani kubwa juu ya Dkt.Nabiijoshua huku wakimpongeza na kuahidi kumpa ushirikiano mkubwa aweze kutekeleza jukumu lake la kuwaunganisha viongozi hao wa kiroho ili waweze kulihubiri neno la Mungu kwa ufanisi nchini.

Katika hatua nyingine,Apostle Goodluck amefafanua kuwa. "Ndugu Rais pamoja na Umoja wa Mitume na Manabii Tanzania, tuko pamoja na tutausongesha mbele umoja huu,na ninachokiamini ni kwamba Rais wetu amechaguliwa na wazee na amethibitishwa na wazee, na ninaamini kwamba kwa uthibitisho ule ambao aliwekewa mikono na wazee na ni Rais mzuri wa kusimamia umoja huu, na ninamwamini yeye na ninauamini uongozi wake pia, nipo pamoja na wewe na tutausongesha pamoja umoja huu,"amefafanua Apostle Goodluck.

Wakati huo huo Mwenyekiti Msaidizi wa Umoja wa Mitume na Manabii Tanzania (UMMT) Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro,Chief Apostle JR amesema kuwa, Kilimanjaro wataendelea kusimamia imara na Rais wa Umoja wa Mitume na Manabii Tanzania, Dkt.Nabiijoshua Aram Mwanytala.

"Kama kiongozi katika Mkoa wa Kilimanjaro na Wilaya ya Hai, Mheshimiwa Rais Nabiijoshua Aram Mwantyala nikuahidi kwamba tupo pamoja Kilimanjaro na tutaungana na wewe hatua kwa hatua, hakuna mahali tutarudi nyuma iwe kwa jasho, iwe kwa gharama ya fedha au kwa gharama ya muda.

"Lakini tutahakikisha tunafika kwenye kusudi, kwa sababu Umoja wa Mitume na Manabii Tanzania, ni kusudi la Mungu kwa nyakati tulizonazo. Hatuwezi kupita kirahisi, lazima tukubaliane hukumu inayotokea, lakini tuna uhakika kwamba tutashinda, maandiko yanasema kwamba, walitoka kwetu, lakini hawakuwa wa kwetu, kama wangekuwa wa kwetu, wangekaa na sisi.

"Mtu anayetoka katikati ya umoja huu ina tafsri kweli, kwamba, tulikuwa naye lakini hakuwa wa kwetu, na ndiyo maana alishindwa kuwa na sisi. Kwa hiyo, wengine ambao wapo kwenye umoja, wafahamu kuwa, ukitaka kutoka kwenye umoja, unatafuta kuwa mshirikina, kwa sababu umoja ni kusudi la Mungu, na kwa sababu ni kusudi la Mungu, unapokuwa nje ya umoja unakuwa nje ya kusudi na makandokando huwa yamebeba mauti.

"Kwa hiyo sisi hatutashangaa sana, kwa sababu unaweza kuwa katikati yetu, lakini usiwe wa kwetu, saa ya kutoka ikifika unachemka unaenda,lakini niseme wale tuliopo, shika sana ulicho nacho,asije mtu akachukua taji yake, shetani huwa hachukui taji ya mtu, bali mtu huwa anaichukua, kwa hiyo ukichezea nafasi kuna watu Mungu atawaweka pale kwa ajili yako, na wewe utaendelea kuzurura na baadaye utarudi,"amefafanua Chief Apostle JR.

Umoja wa Mitume na Manabii Tanzania (UMMT) unaongozwa na Rais Dkt.Nabiijoshua Aram Mwantyala ambaye pia ni Kiongozi Mkuu wa Huduma ya Sauti ya Uponyaji Tanzania yenye makao yake makuu mjini Morogoro.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news