MABEBERU MNACHOSHA:Kweli inasikitisha, kunyonywa hakujaisha

NA LWAGA MWAMBANDE

KIONGOZI wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis ameyataka mataifa ya kigeni yenye nguvu kuacha kupora rasilimali za Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo ikiwemo kulinyonya Bara la Afrika kwa manufaa yao.

Papa Francis ameyasema hayo Jumanne baada ya kuwasili jijini Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku sita barani Afrika. 
 
Ziara ya Papa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Sudan Kusini inafikisha ziara za  kitume 40  za nje ya nchi na ikiwa ni  kwa mara ya  tano anafika barani Afrika

Akizungumza na viongozi wa serikali, wanasiasa, wanadiplomasia, pamoja na wawakilishi wa vyama vya kiraia na mashirika ya kimataifa, katika Ikulu ya DRC, Papa Francis amesema ni jambo la kusikitisha kwamba bara la Afrika linaendelea kuvumilia aina mbalimbali za unyonyaji wa kisiasa ambao umetoa nafasi kwa kile alichokiita ukoloni wa kiuchumi ambao ni sawa na utumwa.

Pia amesema, DRC hainufaiki na utajiri mkubwa wa rasilimali zake na madini yake kwa sababu ya sumu ya uchoyo, inayochochea mzozo nchini humo na kwamba mataifa tajiri hayawezi tena kufumbia macho hali mbaya ya mataifa mengi ya Afrika.

Papa Francis amekuwa nchini DRC kwa ziara ya siku tatu akihubiri injili ya upendo, amani na msamaha huku akiwataka raia waliokosewa kutoa msamaha kama njia moja ya kuiga mfano wa Yesu Kristo.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema kuwa,sauti ya Papa Francis na wito umekuja wakati mwafaka ili kuhakikisha Afrika inaneemeka kupitia rasilimali zake na si kuwatajirisha wageni. Endelea;


1.Papa sauti zidisha, uweze kuwaamsha,
Wafanyayo watuchosha, tunapoteza maisha,
Madini yetu waosha, huku watupiganisha,
Mabeberu mnachosha, hebu acha kutufisha.

2.Unyonyaji wa kutisha, damu unatukausha,
Si aibu kutufisha, waweze jitajirisha,
Wao waponda maisha, wakati sisi twaisha,
Mabeberu mnachosha, hebu acha kutufisha.

3.Papa Francis fikisha, damu wanaovujisha,
Kila siku wanakesha, mifuko kuitunisha,
Huku wanapukutisha, DR Kongo yaisha,
Mabeberu mnachosha, hebu acha kutufisha.

4.Kongo mnajibidisha, utu kuuthaminisha,
Kweli mwajitaabisha, wagomvi kuwafurusha,
Wengine wanazidisha, kuzidi watenganisha,
Mabeberu mnachosha, hebu acha kutufisha.

5.Kweli inasikitisha, kunyonywa hakujaisha,
Mbinu nyingi wazalisha, kuzidi kutukausha,
Huku wanajifanyisha, haki wanaidumisha,
Mabeberu mnachosha, hebu acha kutufisha.

6.Ukoloni uliisha, kisiasa kufurusha,
Utumwa haujaisha, upya wamelianzisha,
Sisi wanatuzamisha, wao wajitajirisha,
Mabeberu mnachosha, hebu acha kutufikisha.

7.Ubeberu unatisha, mali wajimilikisha,
Sisi watupiganisha, wazidi jifurahisha,
Ndiyo hivyo tunakwisha, uchumi wetu waisha,
Mabeberu mnachosha, hebu acha kutufisha.

8.Akili kuiamsha, nasi inatuhusisha,
Nao twajiunganisha, wakati wanatunyosha,
Tutapojitenganisha, rahisi kuwafurusha,
Mabeberu mnachosha, hebu acha kutufisha.

9.Wao watufitinisha, tuzidi jitenganisha,
Silaha wazidondosha, tumalizane maisha,
Huku madini wavusha, wazidi kuneemeka,
Mabeberu mnachosha, hebu acha kutufisha.

10.Papa anawakumbusha, wizi wenu umechosha,
Mnavyojitambulisha, majina twaandikisha,
Vifua mnavimbisha, tutakuja watapisha,
Mabeberu mnachosha hebu acha kutufisha.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news