NA DIRAMAKINI
MAJINA ya watu 14 wa familia moja waliofariki katika ajali iliyotokea jana usiku wilayani Korogwe mkoani Tanga yametajwa.
Ajali hiyo iliyotokea usiku wa kuamkia leo Februari 3, 2023 huko Korogwe imesababisha vifo vya watu 17 wakiwemo ndugu hao wa familia moja na kujeruhi 12.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji Korogwe, Salma Sued ametaja ndugu waliofariki ni Atanasi Rajabu Mrema, Nestory Atanasi, Augustino Atanasi, Kenned Mrema, Godwin Mrema, Yusuph Saimon, Zawadi Mrema, Elizabeth Mrema, Julieth Mrema, Suzana, Rozina A Lamosa, Evelina Cosmas Mrema na watoto wawili (mtoto wa binamu na mtoto wa Julieth).
Wakati huo huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameeleza kusikitishwa na ajali iliyoua watu 17 mkoani Tanga.
Hayo ameyabainisha leo Februari 4,2023 kupitia taarifa fupi aliyoitoa katika kurasa zake rasmi za mitandao ya kijamii.
"Nimesikitishwa na vifo vya watu 17 vilivyosababishwa na ajali iliyotokea jana saa 4:30 usiku eneo la Magila Gereza, Wilaya ya Korogwe, Mkoa wa Tanga.
"Nawapa pole wafiwa na wote walioguswa na vifo hivi. Nawaombea ndugu zetu hawa wapumzike mahali pema na majeruhi wapone haraka,"amesisitiza Rais Dkt.Samia.
Awali katika taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Omary Mgumba imeeleza kuwa ajali hiyo imehusisha magari mawili na kusababisha vifo vya watu 17 na majeruhi 12.
"Ajali hii imesababisha vifo 17 na majeruhi 12 ambao majina yao wote hayajafahamika, miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali yetu ya Wilaya ya Korogwe na majeruhi 10 wamehamishiwa Hospitali ya Mkoa wa Tanga, Bombo na majeruhi wawili wamebaki Hospitali ya Korogwe kwa matibabu.
“Ajali hii imehusisha gari aina ya Mitsubishi Fuso na Coaster iliyokuwa imebeba mwili wa marehemu na abiria 26 ikitokea Dar kwenda Moshi kwenye mazishi,”ameeleza.
Katika hatua nyingine, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa maelekezo kuwa Serikali isimamie msiba wa watu 17 waliofariki kwa ajali mkoani Tanga hadi utakapomalizika.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Omary Mgumba amesema baada ya agizo hilo la Rais tayari hadi sasa majeneza 16 yameshakamilika ambapo bado mawili mafundi wanaendelea nayo ikiwemo la Atanas Mrema ambaye alikuwa anasafirishwa kwenda kuzikwa Kilimanjaro na baada ya ajali jeneza alilobebewa likapasuka.
Aidha, RC Mgumba amesema kuwa tayari wameshapata magari mawili kwa ajili ya kusafirisha miili hiyo ambapo kwa sasa wanasubiri maelekezo ya familia.
"Tuliwapa pumziko kidogo familia kwa sababu wana mambo mawili kuna maiti zipo mochwari na kuna majeruhi wako hospitali, kwa hiyo tulitaka utulivu wao sasa hivi tunaenda kukaa nao ili tuone kwa pamoja kama wapo tayari kusafiri leo au wapo tayari kusafiri kesho."