NA MWANDISHI WETU
WAZIRI wa Madini Dkt. Doto Biteko ameipongeza Kampuni ya Shanta Mining Limited kwa kukamilisha ujenzi wa mgodi ambao unatarajiwa kuanza uzalishaji Machi 2023.
Dkt. Biteko ametoa pongezi hizo mara baada ya kukutana na kuzungumza na Kampuni hiyo katika ukumbi wa Prof. Abdulkarim Mruma jijini Dodoma.
Aidha, ameipongeza kampuni hiyo kwa kukamilisha mpango wa ufungaji wa mgodi na mpango wa ushirikishwaji wa Tanzania katika uchumi wa Madini.
“Mgodi mzuri ni ule ambao baada ya kufunguliwa unaanza kuandaa mpango wa kufungwa,” amesema Dkt. Biteko.
Amesema, Wizara ya Madini inajukumu kubwa la kulinda na kuhamasisha uwepo wa wawekezaji nchini ambapo ameahidi kuendelea kuweka mazingira bora kwa wawekezaji kwa lengo la kuongeza tija kwenye uzalishaji wa madini nchini na kukuza Pato la Taifa kutokana na shughuli za madini.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Shanta Mining Limited Honest Mrema amesema mgodi wa Shanta-Singida unarajiwa kuanza uzalishaji Machi, 2023 ambapo utaajiri zaidi ya wafanyakazi wa moja kwa moja 220 na wafanyakazi 150 wa muda mfupi.
Mrema amesema Kampuni ya Shanta imewekeza zaidi ya Dola za Kimarekani milioni 42 katika mgodi wa Shanta-Singida ambapo maisha ya mgodi huo unatarajiwa kufika mwaka 2028 ambapo kwa sasa utafiti unaendelea kwa lengo la kuongeza maisha ya mgodi huo.
Pamoja na mambo mengine, Mrema amesema Kampuni ya Shanta imesambaza maji safi katika vijiji vinavyozunguka mgodi huo ikiwa ni moja ya kuchangia huduma kwa wananchi wanaozunguka mgodi huo.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amekutana na uongozi wa Kampuni ya Mantra Tanzania Limited kwa lengo la kutambulishwa Meneja mpya wa Kampuni hiyo ambayo inajishughulisha na uchimbaji wa madini ya nishati (Uraniam).