NA MWANDISHI WETU
MWENYEKITI wa Kamisheni ya Utumishi wa Umma Zanzibar, Mheshimiwa Fatma Gharib Bilal amesema Kamisheni ya Utumishi wa Umma katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) ni chombo kilichoundwa kutokana na mageuzi yaliyofanyika pamoja na marekebisho ya Sheria, Kanuni na Taratibu ili kusimamia masuala ya rasilimali watu kuwezesha kuwa na Utumishi wa Umma wenye matokeo.
Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma, Jaji mstaafu Mhe. Hamisa Kalombola (wa tatu kulia waliokaa), Mwenyekiti wa Kamisheni ya Utumishi wa Umma Zanzibar Mhe. Fatma Gharib Bilal (wa pili kushoto waliokaa), wakiwa katika picha ya pamoja na Makamishna na baadhi ya Watendaji wa Tume wakati wa ziara ya Kamisheni kuitembelea Tume.
Mheshimiwa Fatma Bilal amesema hayo wakati wa ziara iliyofanyika kutembelea Ofisi ya Rais Tume ya Utumishi wa Umma jijini Dodoma yenye lengo la kujifunza, kubadilishana uzoefu na kuimarisha ushirikiano kati ya Tume na Kamisheni.
“Lengo la ziara yetu hii ni kujifunza, kupata uzoefu kuhusu masuala ya uendeshaji na usimamizi wa rasilimali watu katika utumishi wa umma na kukuza ushirikiano wa pamoja kati yetu Kamisheni na Tume.
"Tumepata fursa ya kujifunza kupitia mawasilisho mbalimbali yaliyotolewa na Sekretarieti ya Tume namna wenzetu Tume wanavyotekeleza majukumu yao ya kushughulikia rufaa na malalamiko, wanavyofanya urekebu masuala ya rasilimali watu, kuwezesha na kutoa miongozo mbalimbali kuhusu uzingatiaji wa Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo katika Utumishi wa Umma.
"Mawasilisho haya mazuri yametujengea uwezo na tukirudi Zanzibar katika Kamisheni yetu tutaweza kuboresha zaidi,”amesema Mheshimiwa Bilal.
Mwenyekiti wa Kamisheni ya Utumishi wa Umma Zanzibar, Mhe. Fatma Gharib Bilal (kulia) akizungumza na Makamishna na Watendaji wa Tume ya Utumishi wa Umma (hawapo pichani) wakati wa ziara kuitembelea Tume, kushoto ni Mwenyekiti wa Tume Jaji mstaafu Mhe. Hamisa H. Kalombola.
Akizungumza kuhusu Kamisheni ya Utumishi wa Umma Zanzibar alisema, Kamisheni ni chombo huru kinachojitegemea chenye wajibu wa kusimamia, kufuatilia na kushauri namna ya kuimarisha utumishi wa umma ndani ya Zanzibar.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma, Jaji Mstaafu Mheshimiwa Hamisa Hamisi Kalombola ameishukuru Kamisheni ya Utumishi wa Umma Zanzibar kwa kuamua kuitembelea Tume kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu katika masuala mbalimbali.
“Tume na Kamisheni zina jukumu la kutoa haki ni mamlaka za rufaa katika utumishi wa umma kwa Tume, Tanzania Bara na Kamisheni hii kwa Zanzibar.
"Jukumu la kushughulikia rufaa na malalamiko ni jukumu muhimu na la msingi sana, linatoa sura ya Serikali ni kwa namna gani inashughulikia kutoa haki kupitia rufaa na malalamiko yanayowasilishwa ili kutolewa uamuzi kati ya mrufani na mrufaniwa.
"Tume na Kamisheni zina jukumu la kuhakikisha haki inatendeka kwa pande hizi. Ni imani yangu ziara hii imesaidia kubadilishana uzoefu na mwanzo wa kuzidi kuimarisha ushirikiano wenye lengo la kuleta tija kwa pande hizi,” amesema Mheshimiwa Kalombola.
Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma Bw. Mathew Kirama (kushoto) akitoa ufafanuzi kuhusu uendeshaji na usimamizi wa masuala ya rasilimali watu katika utumishi wa umma wakati wa ziara ya Kamisheni ya Utumishi wa Umma Zanzibar kuitembelea Tume, wanaomsikiliza kutoka kulia ni Bibi Miriam R. Mbarouk, Mkurugenzi wa Rasilimali watu na Mipango na Mhe. Halima R. Taufiq, Mjumbe wa Kamisheni ya Utumishi wa Umma Zanzibar.
Awali akizungumza, Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bw.Mathew Kirama amesema kupitia kikao kazi cha Kamisheni ya Utumishi wa Umma Zanzibar na Tume, mengi wamejifunza katika maeneo mbalimbali hususani ya mifumo ya utendaji, usimamizi na hata mifumo ya uwasilishaji taarifa, jambo la msingi zaidi ni kuzidi kuimarisha mahusiano haya katika nyanja mbalimbali.
Tume na Kamisheni zinatambua miongoni mwa vipaumbele vya Serikali zetu ni kuufanya Utumishi wa umma kuwa wenye matokeo na unaotoa huduma bora kwa wananchi.
Katika ziara hii, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Utumishi wa Umma Zanzibar aliambatana na Mheshimiwa Halima R. Taufiq, Mjumbe wa Kamisheni na Bibi Mariam R. Mbarouk, Kaimu Katibu na Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Mipango, Kamisheni ya Utumishi wa Umma Zanzibar.