Mzabuni alilamba asali kuliko Halmashauri ya Mji Tunduma, anatoa 10,000/- huku akivuta zaidi ya 100,000 kwa siku/-

NA DIRAMAKINI

HALMASHAURI ya Mji Tunduma mkoani Songwe imekanusha kuhusu taarifa ambazo zilikuwa zikirushwa katika mitandao ya kijamii zikisema halmashauri hiyo imefunga choo cha Soko Kuu la Tunduma kwa muda wa miezi mitatu na kufanya wafanyabiashara kuteseka, na baadhi yao kuomba choo kirudishwe kwa mzabuni wa aliyekuwa akikiendesha hapo awali.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Februari 10, 2023 na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Halmashauri ya Mji Tunduma mkoani Songwe, William Maganga choo hicho kilifungwa kwa muda wa miezi miwili tu na sasa kimeanza kufanya kazi tangu Januari 9, 2023.

"Sababu kuu ya kufungwa choo hicho ni matengenezo makubwa yaliyoambatana na kubadilisha mfumo wa mashimo ya maji taka kutoka mfumo wa zamani wa shimo moja na kutengeneza mfumo wa kisasa wa (biodigester system) ambao hauhitaji kunyonya maji taka na choo hakiwezi kujaa tena.

"Baada ya kuona choo hiki kikijaa kila baada ya wiki mbili na kusababisha kutiririsha maji na kuhatarisha afya, halmashauri ilikaa kikao na uongozi wa soko pamoja na wafanyabiashara wote wa soko na kukubaliana kukifunga ili kifanyiwe matengenezo hayo ya muda mfupi.

"Baada ya maridhiano kwa pande zote wafanyabiashara walikubaliana kutumia vyoo katika masoko jirani kama vile soko la Manzese lenye vyoo vitatu, soko la kisimani karibu na msikiti lenye vyoo viwili na Afrikana lenye vyoo viwili wakati choo cha soko hilo kikiwa katika matengenezo.

"Ikumbukwe choo hiki tangu kimetengenezwa mwaka 2012 kilikuwa hakijawahi kufanyiwa matengenezo makubwa, kwani kilikuwa kinaendeshwa na mzabuni ambaye alikuwa analipa shilingi 300,000 kwa mwezi.

"Kutokana na mkataba wa mzabuni kuisha Halmashauri ilikichukua choo hiki tangu mwezi Oktoba 2021 na tangu hapo mapato ya choo hicho yalipanda toka shilingi 300,000 alizokuwa anatoa Mzabuni kwa mwezi hadi kufikia shilingi 3,000,000 kwa mwezi,"imefafanua kwa kina taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, hapo wastani mzabuni alikuwa analipa shilingi 10,000 kwa siku wakati halmashauri ilipoanza kukusanya yenyewe mapato yakawa shilingi 100,000 kwa siku.

"Uamuzi wa kubadilisha mfumo wa majitaka katika choo hiki ni kutokana na gharama za kunyonya maji machafu ambazo kila mwezi ilitumika shilingi milioni 4,000,000 kwa sasa tatizo hilo halita kuwepo tena na choo kimeanza kutumika na hakina changamoto yoyote.

"Hata hivyo waraka wa serikali namba 16 wa 2016 ulitoa maelekezo kwa kuzitaka Mamlaka za Serikali za mitaa kukusanya mapato zenyewe kwa vyanzo wanavyoweza kuvikusanya ili kuongeza mapato ya serikali lengo kuu ni kukuza mapato ya Halmashauri.

"Kwa hali hiyo Halmashauri ya Mji Tunduma haitoweza kumrudishia chanzo hicho wakala wa awali kwani mapato yake yameongezeka mara kumi zaidi ya alichokuwa anakusanya wakala.

"Halmashauri inaomba radhi kwa taarifa za kushtua zilizotolewa na kuomba kutozitilia maanani kwani zinaleta taharuki kubwa kwa wananchi na wafanyabiashara wengi na hata kuchafua taswira ya Halmashauri.

"Aidha, Halmashauri itaendela kuboresha miundombinu mbalimbali kadri itakavyojitokeza ili kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi wake,"imefafanua taarifa hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news