NDIYE ANAYEWASUMBUA WAULIZE MASWALI

NA ADELADIUS MAKWEGA

SIKU hiyo mwanakwetu alipoingia katika jengo la studio za kurusha matangazo ambalo lilikuwa na studio moja ya kurusha tu matangazo ya moja kwa moja ya TBC TAIFA, studio mbili za kutayarishia vipindi na moja ya kurekodia michezo ya kuigiza na vipindi vya umma na hata kurekodi nyimbo kutoka kwaya na bendi za muziki hapo hapo kukiwa ala kadhaa za muziki.

Siku hiyo palikuwa na tatizo la viyoyozi kufanya kazi, hata matangazo ya moja kwa moja yalihamishiwa studio nyingine, huku viyoyozi katika baadhi ya studio vliikuwa vinafanya kazi, pengine chumba cha studioni alipo mtangazaji kizima wakati huku kwa Injinia kiyoyozi kibovu, hilo lilikuwa changamoto kubwa.

Kumbuka mwanakwetu akaona mlago wa studio upo wazi huku mainjinia wakiwa kazini na ndani ya studio wapo mashekhe wawili, nazo sauti zao zinasikika katika spika walipo mainjinia wa sauti.

Mwanakwetu akasalimia, Shikamoni ! Wakajibu marahaba, hapo alikuwepo Rashidi Mkola (fundi mitambo) na marehemu Tatu Ali (mhandisi), hapo mwanakwetu nayeye anasubiri wamalize ili arekodi kipindi chake cha Uhalifu Haulipi, hakuwa na budi ya kukaa kusubiri kazi inayofanyika na ni kazi ya washitiri,

“Kila akija mshitiri watumishi wa ndani mnawajibu kumpisha, yeye anafanyiwa kazi akimaliza ndipo nyie watumishi wa ndani mnaendelea na kazi zenu “ Huo ulikuwa mwongozo wa TBC TAIFA.

“BAKWATA wanarekodi Maswali na Majibu ya Dini ya Kiisilamu.” Mwanakwetu akauliza leo yupo nani na nani? Nisikilize kabla hakijakwenda hewani? Akajibiwa ni Mkalinga na Salum.

“Ustadh Issa Mkalinga na Shekhe Alhad Musa Salum ? Ngoja niwasikilize.” Mwanakwetu alisema.Ikachukuliwa karatasi ambayo ilikuwa ni barua iliyopokewa katika Sanduku la Barua la 9191 Dar es Salaam,

“Mimi ni mwanamkwe wa Kiisilamu kutoka Morogoro, ninaishi na mwanaume wa Kikristo ninaleta mbele yenu katika Kipindi cha Maswali na Majibu ya Dini ya Kiisilamu, nimefunga naye ndoa ya Bomani, swali langu, je ndoa yangu inatambulika kwa mujibu wa dini ya Kiisilamu?” Ustadh Alhad Musa Salum alichukua karatasi yenye muswada wa kipindi hicho akawa anasoma majibu yake. Swali hilo lilijibiwa vizuri kwa sura na aya na maneno kadhaa ya Kiarabu yaliyofanyiwa tafsiri. Mwanakwetu hazikumbuki kwa leo hizo sura na aya.

Akiwa hapo hapo Injinia Tatu Ali ambaye alikuwa mama mwenye mabinti zake warembo mno, akamfinya mwanakwetu, alafu akasema, “Haya sasa si unataka kuwa mkwe wangu, Shekhe Musa Salum kashemaliza mambo.” Fundi Mitambo Rashidi Mkola yeye akawa anacheka huku akirekebisha level za sauti ya mashekhe hao.

Hapo Shekhe Issa Mkalinga aliendelea kyasoma maswali na Ustadh Alhad Musa Salum anajibu. Mashekhe hao wakamaliza kazi wakafunga kipindi, kumbuka hapo kinarekodiwa ili kirushwe baadaye.

Walipomaliza wakatoka studioni wakapita pale walipokuwapo akina mwanakwettu na hawa mainjinia wa sauti.

Rashidi Mkola akawa sasa anaendelea kusanifu sauti hizo na kuziwekea kiashiria cha kipindi. Kumbuka pia kuwa hapo walipokaa akina mwanakwetu kiyoyozi kaputi (hakifanyi kazi), hawa mashekhe wakatoka nje ya jengo la studio kuna eneo lina minara mingi ya kurusha matangazo, wakakaa hapo hapo hapo.

Mwanakwetu kumbuka ana la moyoni hadi kufinywa na Injinia Tatu Ali akawafuata mashekhe hawa jambo linamkereketa kutokana na majibu ya swali lililoulizwa na Mama wa Kiisilamu kutoka Morogoro.

“Ustadh pale umejibu kwa manufaa ya wengi, huko nyumbani dada yangu wa Morogoro atakaposikiliza majibu yake mambo yataharibika ! “Hapana yeye mwenyewe anafahamu fika hii dini yetu, lakini hata manufaa ya wengine kama ulivyosema.” Haya alisema Ustadh Alhad Musa Salum kwa lugha ya upole kabisa. “Shekhe umeshaoa?” Aliulizwa mwanakwetu.

Kwa kando injinia Tatu akasema “Makwega hajaoa lakini na yeye ni miongoni mwa wanaowafanyia vurugu binti zangu na kuwanyima usingizi, mie staki yawe kama ya mama wa Morogoro, leo nitawaambia wasikilize Kipindi cha Maswali na Majibu ya Dini ya Kiisilamu.”

Mwanawketu alicheka akaingia studioni kurekodi kipindi chake na huku Rashidi Mkola akiwa katika dawati la sauti akimsaidia kuziweka vizuri.

Mwanakwetu tupo pamoja? Kwa nini mwanakwetu amekumbuka tukio hilo? Shekhe Alhadi Musa Salum ni miongoni mwa waliokuwa vijana Kiisilamu kwa muda mrefu waliofanya kazi na Idara ya Dini BAKWATA katika kutayarisha vipindi vya Dini ya Kiisilamu na Redio Tanzania Dar es Salaam baadaye TBC.

Kwa muda mrefu shirika hilo limefanya kazi hiyo huku majina kama ya Shekhe Seleman

Gologosi ambaye aliwahi kuwa Kaimu Mufti wa Tanzania na Shekhe Mkuu wa mkoa wa Lindi alishirikiana na mashekhe Issa Mkalinga, Shekhe Musa Salum, Shekhe Mtaimbo Kisla.

Baada ya Shekhe Gologosi kuwa majukumu makubwa walibaki Issa Mkalinga na Musa Salumu na baadaye Mtaimbo Kisla.

Miaka ilivyosonga yalikuja kusikika majina kama akina Shekhe Said Mpeta na Usatdh Lugendo Madege. Wengine ni wanahabari katika vyombo mbalimbali vya habari nchini lakini sasa kabaki Sheikh Mtaimbo Kisla na Ustadh Said Mpeta wakifanya kazi hiyo.

Shekhe Alhad Musa Salum na wenzake kadhaa wamekuwa ni wajuzi waliojifunza mambo mengi ya habari katika kufundisha dini hiyo kupitia hasa redio na baadaye waliingia katika runinga TVT,TUT na TBC kulingana mabadiliko ya chombo hicho yalivyokuwa.

Katika kipindi hicho waliweza kufanya kazi wakati wa ANALOJIA, hii ni tekinolojia ya zamani,

“Vipindi hivyo karibu vyote wakati wa RTD walirekodi kwa kutumia kaseti ambayo ilizinasa sauti hizo vizuri, walikuja na muswada wa kipindi wanasoma huku mashine ikirekodi katika kaseti hizo. Tekinolijia hiyo ilikuwa na changamoto kiasi hasa katika kuzisanifu sauti kabla ya kwenda hewani.

Kama muswada wa kipindi umeshasomwa na kuwa mawimbi ya sauti , zilisanifiwa awali katika mikanda miembamba kama ile ya sinema za kizamani (Reel to Reel) , sehemu yenye makosa ya sauti ilikatwa na kuunganishwa na sehemu isiyo na makosa, mara baada ya tekinolojia ya kaseti kuingia ilifanyika kitu kinaitwa Dubbing yaani kaseti inarekodiwa mara ya kwanza inakuwa na makosa alafu unarekodi tena huku ukiacha kurekodi makosa ya awali, hapo mtangazaji/ mtayarishaji na hata anahojiwa walitakiwa kuwa makini kukwepa makosa mengi ili kipindi kisiharibike na kupunguza kazi ya kukata au kurekodi mara mbili mbili.

Hivyo ndivyo hata awali Mawaidha ya Ramadhan ya Mufti wa kwanza wa Tanzania Hayati Hemed Bini Jumaa yalivyorekodiwa ambayo hadi kesho BAKWATA wanayatumia katika mwezi wa Ramadhani hapoTBC TAIFA. ”

Msomaji wangu tambua kuwa hata hiki kipindi hiki ambacho mwanakwetu aliwakuta Ustadh Musa Salum, Issa Mkalinga, Injinia Tatu Ali na Rashid Mkola hii ilikuwa mara baada ya mabadiliko ya awali kutoka ANALOJIA kwenda DIGITALI.Inawezekana jambo hilo halifahamiki na wengi kwa sasa ndiyo maana mwanakwetu anasimulia jambo hilo.

Ukitazama hiki kisa kilichosimulia kinaonesha hata mazingira ya kufanya kazi katika vyombo vya umma yalivyokuwa. Hawa Mashekhe kutoka idara ya Dini ya BAKWATA wanakutana na Wakristo akina mwanakwetu wanataniana na kuulizana maswali na kujibiwa vizuri tu.

Hilo lilijenga udugu na mahusiano mema baina ya UISILAMU na UKRISTO, pia ilisaidia watu wa dini zingine kufahamu Imani ya Waisilamu na mafundisho yake hata kama kijana/binti anaingia katika mahusiano anafahamu fika msimamo wa dini hiyo, hilo liliepusha migogoro ya kidini katika jamii.Kumbuka sana haya maneno yaliyosemwa na Injini Tatu Ali,“Mie staki yawe kama ya mama wa Morogoro, leo nitawaambia wasikilize Kipindi cha Maswali na Majibu ya Dini ya Kiisilamu.”

Mwanakwetu anamsimulia leo hii Ustadh Alhad Musa Salum kwa kuwa alimsikia tangu akitangaza vipindi hivyo na alimuona wakati huo akirekodi vipindi hivyo na ndiyo leo amemkumbuka ndugu huyu.
Mwanakwetu anaona fursa kubwa aliyonayo Ustadh Alhad Musa Salum kwa sasa kuanza kuandika vitabu vya namna alivyokuwa akizifanya kazi hizo tangu enzi ya RTD na baadaye TBC ambao ni uzoefu mkubwa wa kutoka Analogia kuelekea Digitali katika masuala ya kuandaa na kutayarisha vipindi katika vyombo vya habari.

Msomaji wangu kumbuka kuwa Ustadh Alhad Musa Salum na Shekhe Seleiman Gologosi wakiwa ni miongoni mwa watayarishaji vipindi vya dini vya Waisalamu waliofanya kazi na Idara hiyo na kupanda kufika ngazi kadhaa za uongozi wa BAKWATA.

Mwanakwetu upo?
makwadeladius@gmail.com
0717649257

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news