NGENGA:Bora kuepusha ngenga,mipango tutaipanga

NA LWAGA MWAMBANDE

NI wazi kuwa, kila mmoja wetu huwa ana shauku kubwa ya kuwa na utulivu katika maisha yake ya kila siku, hii ni kutokana na ukweli kuwa ndani ya utulivu kuna siri nyingi za kuyaendea maono, mipango na utekelezaji wa mikakati kikamilifu.
Nguvu ya utulivu huwa inayashinda maamuzi yote ya hali ya kutokuwapo kwa utulivu kwa maana ya ngenga.

Tafiti nyingi zinabainisha kuwa, kitu au jambo lolote linalokukabili unapoingia katika utulivu kuna utatuzi au maamuzi ya busara yatafikiwa.

Hivyo, utulivu katika maisha ni jambo la muhimu sana, yaani wewe mwenyewe kuwa mtulivu wa kujisikiliza kwa sababu kuna mambo mengine huwa hayawezi kuelezeka ama kufundishika iwe katika jamii au shuleni ila yanakutegemea wewe mwenyewe.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa, ukitengeneza utulivu wa hali ya juu sana kila hali ambayo ipo ndani mwako utaisikia, hivyo kufanya maamuzi yenye afya na kuepusha ngenga. Endelea;

1. Bora kuepusha ngenga,
Ili nchi kuijenga,
Mipango tutaipanga,
Tufike tunapotaka.

2. Hatuwezi kujijenga,
Tukiendekeza ngenga,
Tunadharau ukunga,
Hatuwezi tukafika.

3. Ngenga ni kujipinga,
Tusimtafute mwanga,
Hili lazima kulonga,
Wenyewe twaadhirika.

4. Amani moyo hukonga,
Mipango kuweza panga,
Na mwelekeo kulenga,
Tufike tunapotaka.

5. Wapi kuliko na ngenga,
Nyumba wakaweza jenga,
Wenyewe watajitenga,
Huku wote wamechoka.

6. Babeli waliopanga,
Mnara ule kujenga,
Kazi hawakujivunga,
Jinsi waliwajibika.

7. Yote waliyoyapanga,
Kilele kuweza tinga,
Lugha moja bila ngenga,
Jinsi walichakarika.

8. Kucheki waliyopanga,
Mnara wanavyojenga,
Mungu kichwa kikagonga,
Watakako watafika.

9. Mpango wake kapanga,
Walofanya ya kijinga,
Kaitengeneza ngenga,
Kazi ikavurugika.

10. Lugha kujigongagonga,
Uelewa kutochunga,
Yote yale walipanga,
Amani ikachafuka.

11. Mnara waliojenga,
Mbele ukakosa songa,
Kwa lugha wakajitenga,
Kote wakatawanyika.

12. Mambo kuweza kupanga,
Mbele kuweza kusonga,
Lazima epusha ngenga,
Uendako utafika.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news