NHC mguu sawa, yataja wanakopita mwaka huu

NA GODFREY NNKO

MKURUGENZI Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Nehemia Mchechu amesema, shirika hilo limekuja na mwelekeo chanya wa utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya shirika kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Mchechu ameyasema hayo leo Februari Mosi, 2023 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuelezea kuhusu ufanisi wa shirika hilo mwaka 2021/22 na mwelekeo wa utekelezaji kwa mwaka 2022/23.

Pia amesema, Shirika la Taifa la Nyumba katika mkakati wake wamejiwekea malengo kama sita. La kwanza ni kuwa kiongozi mahiri katika uwekezaji milki hususani katika Ukanda wa Afrika ya pili ni kuwa msimamizi mahiri wa milki.

Jambo la tatu, Mchechu amesema ni NHC kuwa na uwezo wa uendeshaji na udhibiti wa shughuli za shirika na nne kutumia kikamilifu rasilimali watu kwa sababu rasimali kuu katika shirika ni watu.

Mkakati wa tano, kwa mujibu wa Mchechu ni kukuza uwezo kisheria, kwani wanaenda kushirikiana na sekta binafsi, kwa hiyo lazima wawe vizuri katika mambo ya kisheria kwa maana ya mikataba na ya sita ni kujenga taswira ya shirika ili liendelee kuwa bora zaidi nchini.

"Hivyo, ili kuongeza mapato ya shirika na kuwahudumia watanzania, katika mwaka 2023 shirika limejipanga kuendelea kukamilisha ujenzi wa miradi iliyokuwa imesimama."

Miongoni mwa miradi hiyo, Mchechu amesema ni Mradi wa Morocco Square uliopo jijini Dar es Salaam ambao ujenzi wake upo kwenye hatua za mwisho kukamilika. Mradi huu unatarajiwa kuanza kutumika rasmi mwishoni mwa mwezi Machi 2023.

Amesema, pia wanaendelea na utekelezaji wa mradi wa Samia Housing Scheme (SHS) katika maeneo mbalimbali nchini na wameanza ujenzi wa nyumba 560 eneo la Kawe jijini Dar es Salaam.

"Na tutaanza ujenzi wa nyumba 240 eneo la Medeli jijini Dodoma kwa ajili ya kuuza. Programu ya nyumba za Samia Housing Scheme (SHS) imelenga kutatua changamoto ya makazi bora kwa watu wa kipato cha chini na kati.

"Tunatarajia kuwa asilimia 50 ya nyumba za programu hii zitajengwa jijini Dar es Salaam, Dodoma asilimia 20 na mikoa mingine nchini asilimia 30. Programu hii inayotekelezwa kwa awamu itakuwa na jumla ya nyumba 5000 zitakazogharimu takribani shilingi bilioni 466.

"Programu hii inaenzi kazi nzuri anayoifanya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt.Samia Suluhu Hassan katika kuijenga nchi yetu kiuchumi na kijamii,"amefafanua Mchechu.

Aidha, amesema NHC wataanza ujenzi wa Shopping Mall ya kisasa jijini Dodoma ili kuweza kuwapa wakazi wa jiji hilo eneo zuri na kubwa la kujipatia huduma mbalimbali za kijamii.

Madeni

Mchechu amebainisha kuwa, ndani ya mwaka huu wanaendelea kukusanya madeni ya kodi ya nyumba yanayofikia shilingi bilioni 21 na madeni mbalimbali yatokanayo na uuzaji wa nyumba na viwanja yanayofikia takribani shilingi bilioni 11.

Amesema, msisitizo utakuwa kuhakikisha kuwa kila anayedaiwa analipa deni lake ili kuliwezesha shirika kuendelea kuwahudumia Watanzania wote kwa kutumia rasilimali hizo za umma.

"Lakini hatumfukuzi mtu kwa kushindwa kulipa kodi mwezi mmoja...lakini tunafurahi mtu akilipa nusu mwaka au mwaka mzima ukienda kwa watu binafsi wanaumizana wanasema nataka kodi yangu mwaka mzima au nusu mwaka kwa hiyo niseme tu kwamba.

"Tunahitaji ushirikiano wa karibu wa wale wanaoumizwa kwa ajili ya uzembe. Hutendewi haki kwa ajili ya kupangishwa na mpangaji. Haki yako ni kupangishwa na NHC, mtu anakulangua unalipa kodi kubwa hii haifai kabisa.

"Kuna watu wanachukua nyumba, lakini wana nia ya kufanya hivyo. Sisi nia yetu ni kuwahudumia wananchi, watu wetu wamekuwa wakipita wakiangalia na wanapoona, tunachukua hatua na ukiona kuna sehemu mwananchi anafanyiwa hivyo toa au atoe taarifa kwa sababu orodha ya Watanzania wengine wenye mahitaji ni kubwa sana,"amefafanua Mchechu.

Ubia

Pia amesema, wanaendelea kutekeleza miradi ya ubia kwa kushirikiana na sekta binafsi kadri itakavyokuwa imepitishwa na Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Nyumba la Taifa. Hii itasaidia kukuza uchumi na kuwapatia watanzania makazi bora na nafuu.

"Majengo ambayo hayaleti tija kwenye uchumi wa nchi hii lengo letu ni kuhakikisha majengo haya yanaondolewa na kujemgwa upya na wajenzi ni sisi NHC tukishirikiana na sekta binafsi kwa lengo la kukuza uchumi wa nchi.

"Mipango tuliyonayo tunafikiri ndani ya miezi mitano tutasababisha ujenzi wa shilingi trilioni mbili. Fedha hizi sio kidogo, sasa tunaipata vipi tunataka tulenge wawekezaji angalau 200 kwa miaka mitano walau mwekezaji mmoja atajenga nyumba ya dola milioni tano,kwa hiyo ukipata watu 200 inakuwa vizuri.

"Kwenye hii miradi ya mwanzo tumepata wawekezaji wengi,tunazungumza, tukishakamilisha zoezi tutawaambieni hatua ya kwanza ya utangazaji wa zile tenda na hili tutalitangaza ndani na mwezi huu ili zoezi liishe haraka waanze uwekezaji wao,"amefafanua Mchechu.

Wakati huo huo, Mchechu amesema wanaendelea kusimamia miliki ya nyumba za shirika zipatazo 18,622, kwa kuzifanyia matengenezo ipasavyo. Katika kufanikisha hilo amesema, shirika litatenga bajeti ya kutosha kila mwaka kutekeleza mpango huo.

"Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) linamilikiwa kwa asilimia 100 na Serikali kwa maana kwamba ni shirika la umma. Watanzania wote wana umilki wa shirika hili kwa asilimia 100, lakini ni shirika ambalo halipati ruzuku na ndio maana katika sheria yetu iliyoidhinishwa mwaka 2005 inatutaka pia tujiendeshe kibiashara.

"Hivyo ni jambo jema kuwa na masharikia machache ndani ya Serikali ya biashara, kuna baadhi ya mashirika machache yatakayohangaika na kutoa huduma, na kuna baadhi ya mashirika machache yatakayohangaika na biashara ndani ya Serikali,"amefafanua.

Aidha, amefafanua kuwa, wataendelea kushirikiana na taasisi na wadau mbalimbali ili kurahisisha utekelezaji wa miradi yao hususan ushiriki wao wa kuweka miundombinu muhimu ya barabara, maji na umeme katika maeneo ya ujenzi wa nyumba.

"Na tutaendelea kujenga mahusiano yenye tija na wabia na taasisi mbalimbali yakiwemo mashirika, Bunge na vyombo mbalimbali vya sheria ili kuweza kupata manufaa kwa shirika ikiwemo kusimamia nidhamu ya utendaji kazi ndani ya shirika ili kuweza kuamsha ari na tija kwa watendaji. Huduma bora kwa wateja ndiyo kipaumbele cha utendaji wa watumishi wa shirika,"amefafanua Mchechu.

Mbali na hayo Mchechu amebainisha kuwa, wataendelea kushirikiana na vyombo vya habari kama muhimili muhimu wa upashanaji habari kwa wananchi, uelimishaji na kujenga taswira ya shirika hilo.

Vyanzo

Shirika hilo ambalo mtaji wake umeongezeka kutoka shilingi trilioni 2.9 mwezi Juni, 2019 hadi shilingi trilioni 3.4 mwezi Juni, 2022 vyanzo vyake vya mapato ni kodi za nyumba zake,mauzo ya nyumba wanazojenga na mapato wanayopata katika kazi za ukandarasi.

"Ukienda Dodoma pale tunajenga makao maku ya wizara nane, vyanzo vingine tunafanya ushauri katika miradi mbalimbali ya Serikali na isiyo ya Serikali kwa hiyo vyanzo vyetu hivi ndivyo vinavyochangia mapato ya shilingi bilioni 257. 47,"amefafanua Mchechu

Amesema, kwenye mapato ya miradi ya ukandarasi nayo yamekuwa kutoka shilingi bilioni 25.6 hadi kufikia shilingi bilioni 43.98.

"Sasa haya ni kwa sababu ya uwezo wa shirika katika ujenzi wa nyumba umeongezeka, watu wengi wamekuwa na imani kwetu na uzoefu wa ujenzi ukiangalia sasa hivi tuna ujenzi wa hata kitengo chetu cha ujenzi wa ndani kimekuwa kwa kasi.

"Ndio maana nasema majengo nane ya wizara pale Dodoma tunajenga sisi na miradi mingine mikubwa tunajenga sisi wenyewe Kawe, Samia Housing Scheme tunajenga maghorofa 10, ni mtaa mzima wa maghorofa 10 tumelenga wa watu wa kipato cha kati na chini,"amefafanua Mchechu.

Pia amesema, sababu ya shirika kujikita katika kutekeleza miradi mingi kwa mwaka huu inatokana na mahitaji mengi ya watu na wanatarajia kuitekeleza kwa ufanisi mkubwa.

Jamii

Kwa upande wa Sera ya Uwajibikaji kwa Jamii ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Mchechu amesema katika kipindi cha mwaka 2021/2022 shirika limeendelea kuchangia kwenye sekta ya elimu na afya.

Kwa upande wa elimu, amesema shirika limechangia ujenzi wa madarasa na kwa upande wa afya michango ililenga kuboresha huduma za afya kwa kupunguza changamoto za afya na masuala mengine ya kijamii ili kuleta unafuu na maisha bora kwa jamii. Katika kipindi hicho shirika lilitumia kiasi cha shilingi milioni 415.2.

"Katika huduma za jamii pia tumekuwa tukijikita kama sehemu ya kurudisha shukrani kwa jamii kidogo kutokana na kile tunachokipata, mara nyingi shughuli yetu kwa asili inarudisha unapomuuzia mtu nyumba, unapompangisha mtu nyumba inagusa maisha ya mtu, lakini pamoja na hayo huwa tunachukua sehemu ya faida tunaenda kusaidia sekta ya elimu na afya.

"Huwa tunaangalia na maombi pia kwa hiyo kiasi cha pesa ambacho kilitumika kwa ajili ya kusaidia jamii ni shilingi milioni 415. 2 kwa hiyo karibia nusu bilioni tuliipeleka kwenye huduma za jamii na mwaka huu bajeti yetu ilikuwa shilingi milioni 500, ninafikiri kwa mwaka ujao tutaweza kuongeza kwa sababu mahitaji ni makubwa walau mara mbili ya kiwango hicho,"amesisitiza Mchechu.

Shirika la Nyumba la Taifa lilianzishwa kwa Sheria ya Bunge Na.45 ya mwaka 1962.NHC baadae liliunganishwa na iliyokuwa Msajili wa Majumba kwa Sheria Na. 2 ya mwaka 1990 ambayo ilirekebishwa mwaka 2005 ili kulifanya Shirika lijiendeshe lenyewe kibiashara.

Malengo ya shirika kwa mujibu wa Mpango Mkakati wake (2015/16-2024/25) ni pamoja na kuwa msimamizi mahiri wa miliki, kuimarisha uwezo wa kiuendeshaji na udhibiti, kutumia kikamilifu rasilimali watu, kuwa kiongozi katika uendelezaji miliki, kuhuisha mikataba na mazingira ya kisheria na kujenga taswira ya shirika nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news