Ni kesho Vazi la Taifa, Mdundo wa Taifa na wasanii kujazwa fedha Dar

NA DIRAMAKINI

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Hassan Abbasi amesema,kesho Sekta ya Utamaduni na Sanaa itakuwa na tukio kubwa la kihistoria nchini.
Dkt.Abbasi ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo tukio hilo adhimu litafanyika Februari 3,2023 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini humo.

"Tangu kuundwa kwa sekta tatu baada ya kuondolewa Wizara ya Habari na tangu ilipoundwa wizara vitu vingi vimekuwa vikienda kwa kasi sana. Dhamira ya Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan tunaiona katika kuhudumia sekta hizi za Utamaduni,Sanaa na Michezo.

"Leo nimewaita kwa ajili ya Sekta ya Utamaduni na Sanaa na kesho tutakuwa na tukio kubwa tukio adhimu la kihistoria katika. Kwa hiyo, kesho tarehe 3 Februari 2023 tunakuja na mambo matatu ya wizara yetu.
"Sekta hii inaajiri vijana wengi sana na pia ni wizara inayochagiza maendeleo katika sekta nyingine sisi tunatangaza utalii, kuwaleta pamoja watu wengi zaidi, michezo ni afya. Kwa hiyo matukio ya hapo kesho ni mwendelezo wa mchango wa wizara yetu."

Vazi la Taifa

"Tutakuwa na mtukio kwenye ukumbi wa Mwali mu Julius Nyerere pale, tunaomba wadau pale kuanzia saa 7:00 mchana tutaanza mara moja baada ya muda huo jambo la kwanza ni wizara kupokea vazi la taifa, baada ya mchakato wa muda mrefu sasa na majadiliano ya muda mrefu sana na baada ya kukosekana maamuzi kwa muda mrefu sana, hatimaye tunakwenda kupokea.

"Ni mapendekezo ya wadau mbalimbali ambayo wameyatoa kuhusu aina gani ya mavazi,kamati itatuambia maana imeundwa mwaka jana,tujiandae ni aina gani ya mavazi.

"Ninachofahamu msiwe na wasiwasi yatakuwa mavazi yenye heshima,yenye utambulisho wa Taifa letu, haliendi kwenda kuwaondolea watu haki ya kuvaa mavazi mengine, haya yatakutambulisha kama Mtanzania sehemu mbalimbali.
"Hili litakuwa ni tukio la kwanza na wao watatueleza kwa kina tu kwamba wamepita kwa watu wangapi wakatoa maoni na ugumu wa kuchakata maoni hayo hadi kufikia hapo kwenye kupata vazi lenye utambulisho wa taifa,"amesema Dkt. Abbasi.

Mdundo wa Taifa

Pia Dkt. Hassan Abbasi amesema kuwa, Wizara ya Sanaa,Utamaduni na Michezo inakuja na mdundo wa taifa utakaowezesha kuitambulisha nchi.

"Tunataka tuwe na namna ambayo ukisikia ujue huu ni mdundo au hii ni singeli ya Tanzania, ukiusikia huu muziki useme aa! hii ni taarabu ya Tanzania, tunawapongeza hawa wenzetu kwa namna ambayo wamefanya hii kazi.
"Hawa ni watu wabobezi kwa hiyo lazima muziki wetu upate mwongozo fulani kwa hiyo wamekamilisha hilo zoezi baada ya kupitia nidundo ya makabila yetu, tunaamini watakapowasilisha hapo kesho itakuwa vyema zaidi.

"Tutajua muziki wetu una vionjo gani, hatuwezi kwenda shagala bagala muziki ni biashara na ni utambulisho wa taifa, tumekuwa tukisikia muziki fulani tunasema huo muziki ni wa South Africa au America lazima sasa na sisi Watanzania tuwe na hatua.

"Moja ya kazi waliyoifanya wametoa mwongozo katika namna ambayo wanaozalisha muziki kuna maeneo ya ala za midundo msitoke ili kuupa muziki wetu utambulisho wa Kitanzania,tunawaalika wadau wa sanaa Julius Nyerere."

"Jambo jingine ningependa kuwapongeza, kamati hii,kuna wasanii kadhaa wamejitokeza wametunga nyimbo kabisa kwenye hizo biti za midundo za ala ili tuweze kuona. Kuna wasanii wakubwa kabisa wa nchi hii wamerekodi kwa hiyo tutasikia mashairi katika mahadhi mbalimbali na singeli,kesho ni siku muhimu sana. Nawapongeza wasanii wamejitoa sana katika hili wapo wasanii wamefanya colaboration kwa hili jambo muhimu kwenye taifa letu na katika sekta ya sanaa yetu hapa nchini."

Mikopo

Jambo la tatu,Dkt.Abbasi amesema ni baada ya muda mrefu kutokuwepo kwa Mfuko wa Sanaa ambapo amesema hatua iliyofanywa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ni kurejesha mfuko wa maendeleo ya sanaa.

"Mwaka jana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wake wa busara alioufanya ni kurejesha Mfuko wa Maendeleo ya Sanaa, Jambo la pili ikawa ni kuufanya mfuko uanze kazi. Sasa ninayofuraha mnafahamu tulianza mwaka jana mwezi wa 12, 2022 kutoa mikopo midogo midogo kwa wadau wa sanaa ili kuwawezesha waweze kutanua kazi zao za sanaa. Sasa kesho tarehe 3 Februari, 2023 tunakwenda kutoa mkopo kwa awamu ya pili kwa wadau wa tasnia ya sanaa na utamaduni.

"Kesho baada ya awamu ya kwanza itafanyika awamu ya pili na kesho mikopo itakayotoka thamani yake itakaribia shilingi Bilioni moja ambayo itakwenda kuwasaidia wasanii katika mawanda yao mbalimbali na wale wa utamaduni kama ambavyo wameomba, kesho wenzetu watasema wametoa kwa vigezo vipi na mambo mengine."

"Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa fedha za kuwasidia vijana na watu wengine walio katika mawanda haya, fedha zipo zitaendelea kutolewa kwa makundi au watu binafsi wanaokamilisha taratibu, tutakuwa na awamu tofauti tofauti tofauti,"amefafanua Dkt.Abbasi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news