NA JAMES MWANAMYOTO
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama, amesema watumishi wa ofisi yake wametoa msaada wa mahitaji mbalimbali kwa wenye uhitaji katika Kituo cha Matumaini Mihuji na Nyumba ya Amani na Furaha Hombolo inayotunza wazee na watoto ili kujenga matumaini ya wahitaji hao na kuwawezesha kutimiza ndoto za maisha yao.

Mhe. Jenista amesema hayo wakati akikabidhi msaada wa vitu mbalimbali kwa wenye uhitaji katika kituo cha matumaini Mihuji jijini Dodoma.
Mhe. Jenista amesema, msaada walioutoa unaunga mkono malezi kwa wenye uhitaji kwani wanaamini kuwa watoto wenye uhitaji ndio watumishi wa umma na viongozi wa baadae, hivyo msaada huo ni sehemu ya kuchangia ujenzi wa msingi mzuri wa watoto hao kuwa watumishi wa umma na viongozi wa baadae watakaotoa mchango katika maendeleo ya taifa.

Mhe. Jenista ameongeza kuwa, jamii isipowasaidia wenye uhitaji watakosa mwelekeo na hapo baadae hakutakuwa na rasilimaliwatu itakayotekeleza kwa vitendo kaulimbiu ya Rais wa Awamu ya Sita Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya KAZI IENDELEE ambayo inajenga ari ya kila mtanzania kushiriki katika ujenzi wa taifa pamoja na kuandaa rasilimaliwatu itakayokuwa na tija katika utoaji huduma kwa wananchi.

Aidha, Mhe. Jenista amesema, msaada wa vitu uliotolewa na watumishi wa ofisi yake katika Kituo cha Matumaini Mihuji na Nyumba ya Amani na Furaha Hombolo imetokana na michango binafsi ya watumishi na si fedha ya Serikali.
“Michango iliyokusanywa imetuwezesha watumishi wote kuacha familia zetu na kuja kuwafariji wenye uhitaji, niwahakishie hakuna mtumishi yeyote aliyesalia nyumbani kwake wakati wa zoezi hili muhimu la kutoa faraja kwa wahitaji,” Mhe. Jenista amefafanua.
Akikabidhi msaada kwenye Nyumba ya Amani na Furaha inayotunza wazee na watoto Hombolo, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deogratius Ndejembi amesema msaada alioukabidhi kwa niaba ya watumishi wa ofisi yake japokuwa ni mdogo lakini ni sadaka inayojitosheleza na kuongeza kuwa, watumishi wameguswa kwasababu wanathamini mchango wa wazee ambao wakati wakilitumikia taifa walijituma kwa moyo na uzalendo katika maeneo mbalimbali nchini.
Akizungumza kwa niaba ya uongozi wa Kituo cha Matumaini Mihuji, Sista Elizabeth John amewashukuru watumishi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI kwa kuwatembelea na kutoa msaada utakaosaidia malezi ya watoto katika kituo chao na kuahidi kuwa misaada hiyo itatumika kama ilivyokusudiwa.
Mmoja wa watoto anayelelewa katika Kituo cha Matumaini Mihuji Bi. Elizabeth Francis, amemshukuru Mhe. Jenista na watumishi wa ofisi yake kwa msaada walioutoa na kuahidi kuendelea kuwaombea ili waweze kutekeleza vema majukumu yao ya kulitumikia taifa.
Naye, Msaidizi wa Kituo cha Nyumba ya Amani na Furaha Hombolo Sista Maria Radiance amesema, sadaka iliyotolewa na watumishi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI katika kituo chao itasaidia malezi ya wazee na watoto kituoni hapo na kuongeza kuwa ujio wa watumishi hao ni tendo la upendo ambalo linatokana na msukumo wa Mwenyezi Mungu.

Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imeshiriki shughuli za kijamii kwa lengo la kujenga mahusiano mazuri na jamii yatakayokuwa na tija katika kupata mrejesho utakaoboresha huduma katika Utumishi wa Umma.