NA MWANDISHI MAALUM
OFISI ya Wakili Mkuu wa Serikali leo tarehe mosi Februari 2023 imeshiriki kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Sheria nchini ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan huku ikiwakilishwa na Naibu Wakili Mkuu wa Serikali Bi. Sarah Duncan Mwaipopo pamoja na Mawakili wa Serikali.
Naibu Wakili Mkuu wa Serikali Mhe. Sarah Duncan Mwaipopo (aliyesimama katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Mawakili wa Serikali wa Ofisi yake kwenye maadhimisho ya Kilele ya Wiki ya Sheria yaliyofanyika jijini Dodoma. (Piha na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali).
Akizungumza katika maadhimisho hayo yaliyofanyika kitaifa katika Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma yenye kauli mbiu isemayo, “Umuhimu wa Utatuzi wa migogoro kwa njia ya Usuluhishi katika kukuza uchumi Endelevu: Wajibu wa Mahakama na Wadau”, Mhe. Rais Dkt. Samia amefurahishwa na juhudi zinazofanywa na Mahakama ya Tanzania pamoja na wadau wake kwa kazi nzuri ya kuhakikisha wanatoa haki kwa usawa na kwa wakati.
Mhe. Rais Dkt. Samia ameongeza kuwa mafanikio makubwa yaliyofikiwa yamechangiwa na uamuzi wa Serikali iliyouchukua mwezi Agosti 2022 wa kuongeza idadi ya Majaji wa Mahakama Kuu kutoka Majaji 78 waliokuwepo hapo awali mpaka kufikia Majaji wa Mahakama Kuu 100 hatua ambayo imeongeza chachu katika kufikia mafanikio hayo leo.
Rais Dkt. Samia ameeleza kuwa kwa sasa Majaji wote nchini wanaendelea kutoa haki kwa usawa na wakati ikiwa ni pamoja na kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utoaji haki nchini pasipo kumuonea mtu yoyote.
Aidha, Rais Dkt. Samia ameipongeza Mahakama kwa ujenzi wa miundombinu na kuendelea kusogeza huduma karibu na wananchi huku akionyesha kufurahishwa zaidi na hatua zilizofikiwa za kukamilika kwa taratibu za upatikanaji wa huduma za Mahakama Kuu katika Mikoa minane ya Singida, Pwani, Songwe, Katavi, Geita, Njombe, Simiyu na Lindi sambamba na mpango wa kujenga Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki katika maeneno mengine ikiwemo kisiwani Pemba.
Kuhusu suala la upungufu wa watumishi pamoja na maslahi kwa watumishi wa Mahakama, Mhe. Rais Dkt. Samia ameahidi kuendelea kulifanyia kazi suala hilo kwa kuanza na hatua ya kuunda Kamati ambayo itakuwa na jukumu la kufanyia kazi suala hilo na baadae itatoa taarifa yake baada ya miezi minne.
Naibu Wakili Mkuu wa Serikali Mhe. Sarah Duncan Mwaipopo akiwa kwenye maandamano kwa ajili ya ufunguzi wa maadhimisho ya Kilele cha Wiki ya Sheria yaliyofanyika Februari Mosi, 2023 jijini Dodoma.
Mhe. Rais Dkt. Samia ameeleza kutambua uwepo wa fedha kutoka kwa wadau wa maendeleo ikiwepo Benki ya Dunia ambazo zimesaidia kuimarisha miundombinu ya Mahakama, ikiwemo Mahakama za Mwanzo 60 na majengo mengine 18 ambapo kati ya hayo ni Mahakama 11 Wilaya.
“Uwepo wa majengo haya ni ishara nyingine na azma ya Mahakama pamoja na Serikali kuhakikisha inasogeza huduma za haki karibu na wananchi hivyo naomba kutoa rai kwa uongozi wa Mahakama kuwa miradi yote inayotekelezwa izingatie ubora unaoendana na fedha iliyotolewa,”alisema Mhe. Rais Dkt. Samia.
Naibu Wakili Mkuu wa Serikali Mhe. Sarah Duncan Mwaipopo akiwa kwenye picha ya pamoja na Katibu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Mary Makondo wakati wa Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Sheria yaliyofanyika jijini Dodoma.
Mhe. Rais Dkt. Samia amesisitiza kuwa azma ya Serikali yake kuhakikisha taasisi zinazoshirikiana na Mahakama katika mnyororo wa utoaji haki, ikiwemo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka pamoja na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali zinapata pia miundombinu wezeshi ili shauri linalofunguliwa Mahakamani linasomeka sawa sawa na lile lililosajiliwa katika Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali pamoja na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza na viongozi na watumishi pamoja na wananchi (hawapo pichani) walioshiriki sherehe za kilele cha Siku ya Sheria nchini Februari Mosi, 2023 katika Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma.
Naye Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka wananchi pamoja na wadau wenye migogoro kutumia njia ya usuluhishi badala ya kukimbilia Mahakamani kwa kuwa tayari Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha Sheria ya Usuluhishi ya Mwaka 2020 (Arbitration Act, 2020) ambayo pamoja na mambo mengine imeweka mifumo madhubuti ya usimamizi na uratibu wa usuluhishi ikiwemo kuanzishwa kwa Kituo cha Usuluhishi Tanzania (Tanzania Arbitration Center)
Naye Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi alimuahidi Mhe. Rais Dkt. Samia kuwa Ofisi yake na ile ya Wakili Mkuu wa Serikali wataendelea kusimamia vyema mashauri yote kwa niaba ya Serikali ikiwa ni pamoja na kutatua migogoro kwa njia ya usuluhishi pamoja na kusimamia kwa karibu maelekezo aliyoyatoa kuhusu jambo hilo ili kuhakikisha migogoro inatatuliwa kwa njia ya usuluhishi.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi akisoma hotuba yake katika Sherehe za Maadhimisho ya kilele cha Siku ya Sheria nchini yaliyofanyika Jijini Dodoma.
Hotuba hiyo ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali pia ilisomwa na Mawakili wa Serikali kwenye kilele cha maadhimisho hayo kwenye Mikoa yote ambayo ina Ofisi za Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali
Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Mahakama akiwemo Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, ambaye ndiye aliyekuwa mwenyeji wa Maadhmisho hayo, Majaji wa Mahakama ya Rufani, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani, Majaji wa Mahakama Kuu, Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Prof. Elisante Ole Gabriel, Msajili Mkuu wa Mahakama, Mhe. Wilbert Chuma pamoja na watumishi wengine.
Majaji wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu ya Tanzania wakisikiliza hotuba ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan leo tarehe 01 Februari, 2023 katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini yaliyofanyika katika Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma.
Wageni wengine walikuwa Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi, Spika wa Bunge la Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson, Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro, Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Wakuu wa Wilaya, Viongozi wastaafu wa Mahakama na Serikali, Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika, Prof. Edward Hosea na wananchi kwa ujumla.