OWEZA: Tuendelee kuwa faraja kwa wengine

NA LWAGA MWAMBANDE

UKISOMA Biblia Takatifu katika kitabu cha Warumi 8:35 utaona kuna swali ambalo linasema, “Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je! Ni dhiki au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga?”.

Katika swali hilo utaona neno dhiki kwa maana ya huzuni au tabu ambayo mara nyingi binadamu amekuwa akipitia katika maisha ya kila siku kwa sababu moja au nyingine, kwa wengine wanapokishuhudia kipindi hicho kinamtokea mtu huwa wanaguswa sana na wakati mwingine kuwashika mkono.

Kumfurahisha mtu baada ya kupata dhiki kwa maana ya Oweza ni moja wapo ya faraja kubwa inayotoka katika jamii iliyojengeka katika misingi ya hofu ya Mungu, upendo, ushirikiano, amani na mshikamano kama ilivyo kwa Watanzania wengi.

Oweza ambalo ni neno la kiswahili kwa mujibu wa Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA) linamaanisha kuwa, ni ile hali ya kumfurahisha mtu baada ya kupata dhiki.

Rejea, Wafilipi 2:4 “Kila mmoja wenu asiangalie mambo yake mwenyewe tu, bali pia ajishughulishe kwa faida ya wengine.”

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa,Mungu anabariki watu ili wawe baraka kwa wengine katika kipindi chote ikiwemo wakati wa dhiki. Endelea;


1.Amepata shida sana,
Na amepambana sana,
Yaishe ya kusigana,
Anapaswa kuowezwa.

2.Watesi tuliwaona,
Ndoa walipotengana,
Na ameumizwa sana,
Anapaswa kuowezwa.

3.Walivyoshirikiana,
Wakati wanapatana,
Maendeleo kuona,
Anapaswa kuowezwa.

4.Nyumba yao tuliona,
Kujenga kuchangishana,
Ilibidi kugawana,
Anapaswa kuowezwa.

5.Pale walipoachana,
Wakaanza kupishana,
Kwa mali wakagombana,
Anapaswa kuowezwa.

6.Kwa vile wameachana,
Eti yeye kitu hana,
Juhudize wazikana,
Anapaswa kuowezwa.

7.Mume eti wamuona,
Ndiye afaa kuvuna,
Mwanamke wamkana,
Anapaswa kuowezwa.

8.Watoto tuliwaona,
Na mama kuambatana,
Eti kurithi hapana,
Anapaswa kuowezwa.

9.Mwanamke kapambana,
Kote wamefikishana,
Haki aweze iona,
Anapaswa kuowezwa.

10.Kufika kutishiana,
Kwamba eti ataona,
Lakini akang’ang’ana,
Anapaswa kuowezwa.

11.Mwisho mwema tumeona,
Mali wameshagawana,
Naye ametulizana,
Anapaswa kuowezwa.

12.Kama asingepambana,
Kitu asingekiona,
Kilio tungekiona,
Anapaswa kuowezwa.

13.Mtu akisota sana,
Jambo jema tunaona,
Vema naye kuungana,
Anapaswa kuowezwa.

14.Hata kuandaliana,
Pate ndogo kujichana,
Machungu tena hakuna,
Vema sana kuowezwa.

15.Dunia tunapambana,
Tunahangaika sana,
Na hata kuvurugana,
Vema mtu kuowezwa.

16.Hapo mtu ajiona,
Kazi yake imefana,
Nanyi naye mwaungana,
Vile anavyoowezwa.

17.Oweza neno twaona,
Ikifa dhika kufana,
Watu wanapongezana,
Huko ndiko kuowezwa.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news