NA DIRAMAKINI
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameutaka uongozi wa CCM, kuweka usimamizi mzuri wa mapato yanayotokana na mradi wa maduka ya Darajani, “The Darajani Souk” pamoja na kufikiria miradi mingine yenye faida itakayokisaidia chama na jumuiya zake.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi (katikati) akikata utepe kuashiria ufunguzi wa Mradi wa Maduka ya Darajani Souk yaliyojengwa na Kampuni ya Africab Group Tanzania katika Eneo la Darajani Wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi katika hafla iliyofanyika Februari 18, 2023 na kushoto kwa Rais ni Mama Mariam Mwinyi, kulia ni Mkurugenzi Mwenza wa Africab, Bw.Yussuf Ezzi na kushoto kwa Rais ni na viongozi wengine.(Picha na Ikulu).
Rais Dkt.Mwinyi ameyasema hayo kwenye ufunguzi wa mradi wa maduka ya Darajani Souk, Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Amesema, mradi wa maduka hayo ya Darajani ni sehemu ya jitihada za kutekeleza ilani ya uchaguzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) baada ya kuwaahidi wafanyabiashara wadogowadogo kuwajengea maeneo mazuri ya kufanyia biashara.
Pia amesema, maeneo hayo yameanzwa kujengwa yakiwemo maeneo ya wajasiriamali wadogo kwenye mikoa na wilaya zote, ikiwemo miradi ya ujenzi ya masoko makubwa kama Chuini, Jumbi, Mwanakwerekwe na Mombasa.
Aidha alieleza CCM itaendelea kubuni miradi mikubwa ya kiuchumi na uwekezaji ili kukijenga chama kwa nguvu za kiuchumi.
Rais Dkt.Mwinyi amewataka viongozi wa chama hicho, kutumia vyema mradi wa Darajani Souk ili kufanikisha dhamira ya chama kwa kubuni miradi mikubwa ya kiuchumi yenye kipato na kukikuza kiuchumi na kueleza ujenzi wa mradi wa maduka hayo utanufaisha ustawi wa uchumi wa chama.
Katika hatua nyingine Rais Dkt.Mwinyi alimewasihi wafanyabiashara watakaobahatika kupata milango, kuzingatia masharti yaliyowekwa ili kuepusha migogoro isiyo ya lazima.
Aidha, amewataka viongozi wa chama kutumia busara ya ugawaji wa maduka hayo kwa kuwapa kipaumbe wafanyabiashara wote waliopisha mradi huo.
“Kipaumbele cha kwanza wapewe wale wote waliopisha mradi huu, ambao walilazimika kusitisha shughuli zao za biashara na kuacha ujenzi uenedelee,”ameelekeza Rais Dkt.Mwinyi.
Amesema, Serikali imeruhusu eneo hilo kuuzwa biashara saa 24 na kuwahakikishia ulinzi wa mali zao pamoja na kuwataka kulitunza vyema eneo hilo kwa kuendelea kuitunza haiba ya mji kwa mazingira safi na salama.
“Ndugu zangu taaswira tuliyonayo paha tunapaswa kuitunza, tuhakikishe sehemu hii inaendelea kuwa nzuri kila wakati, mfanye ukarabati kwa kila patakapohitajika, rangi ipakwe ikichakaa na kufanyiwa matengezo kwa sehemu itakayoharibika, ili maduka yaendee kudumu muda mrefu,”alishauri Rais Dkt. Mwinyi,
Akizungumzia haiba ya Mji Mkongwe, Dkt.Mwinyi alieleza licha ya mabadiliko ya mji yanavyoendelea alisema Serikali haina nia ya kubadili haiba halisi ya mji Mkongwe bali kuutunza na kuuendeleza udumu.
“Sote tunaimani njema ya kuutunza Mji Mkongwe, ni urithi wetu sisi na vizazi vijavyo, hatuwezi kuruhusu uharibike,”alisema Rais Dkt.Mwinyi.
Naye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalumu za SMZ, Masoud Ali Mohammed alisema Serikali inatekeleza ahadi zake kwa vitendo, aliwasihi wananchi waache chuki, kebehi na lawama kwani hazijengi nchi na aliwaomba washirikiane kwa kupeana moyo ili kuendeleza uchumi na biashara.
Akizungumza kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu CCM - Zanzibar, Katibu wa Kamati Maalum NEC, Idara ya Uchumi na Fedha kutoka ofisi Kuu cha Chama, Kisiwandui, Afadhali Taibu Afadhali, alisema ujenzi wa mradi wa maduka hayo ni utekelezaji wa sera ya CCM, toleo la 2021 inayokitaka Chama kutekeleza miradi na uwekezaji na kuelekeza kazi zote za chama kujikita kwenye kujenga uchumi na uwekezaji.
Aidha, alitoa wito kwa wawekezaji wengine kujitokea zaidi na kuwekeza Zanzibar ambako alieleza kwamba nchi imebarikiwa kuwa na maeneo mengi ya kuwekeza hivyo aliwataka kutumia fursa hiyo vilivyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Idrisa Kitwana alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilikua na mipango mingi ya maendeleo na uwekezaji kwenye eneo hilo la Darajani, alieleza mafanikio ya mradi wa maduka hayo ni miongoni mwa miradi iliyoelekezwa kwenye eneo hilo, aidha alisema Serikali inaendeleza miradi mengine ya kisasa itakayotoa faida nyingi kwa Serikali na watu wake ikiwemo miradi ya maeegesho ya gari ya kisasa kwenye eneo la mji wa Darajani.
Mmoja wa mwakilishi kutoka kampuni ya Africab ambao ndio wajenzi wa mradi wa Darajani Souk, Yussuf Azzi alipongeza juhudi za Serikali ya Awamu ya Nane kwenda kasi kimaendeleo na kueleza kwamba ni awamu yenye upeo unaoona mbali zaidi na kufikiria utekelezaji wa maendeleo ya miaka ya mbele zaidi na kuongeza kuwa eneo la maduka ya Darajani Souk ni sehemu yenye mazingira rafiki kwa wafanyabiashara.
Eneo hilo la maduka ya Darajani Souk awali lilijuuikana kama eneo la makontena ambapo kwa wakati huo kulikuwa na makontena 58 yalibeba wafanyabiashara 168 na sasa eneo hilo limetolewa maduka 445 ambalo linatarajiwa kuhudumia wafanyabiashara wengi zaidi.