NA DIRAMAKINI
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewaomba wafanyabiashara nchini kupunguza bei za bidhaa hasa vyakula kwa nia ya kuwapunguzia ukali wa maisha wananchi wa kipato cha chini.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na wafanyabiashara waagizaji wa vyakula na bidhaa kutoka nje ya nchi, mazungumzo hayo yamefanyika Januari 31, 2023 katika Ukumbi wa Ikulu jijini Zanzibar.(Picha na Ikulu).
Dkt. Mwinyi ametoa ombi hilo Ikulu jijini Zanzibar alipozungumza na wafanyabiashara mbalimbali na kujadili kupanda kwa bei ya chakula nchini.
Amesema, bidhaa za vyakula ikiwemo mchele zimepanda mara dufu hali iliyozusha taharuki kubwa kwa kuongeza ugumu wa maisha.
Amesema haijawahi kutokea mchele kupanda bei kiasi kikubwa kama ilivyo sasa na kuongeza kuwa ni bidhaa yenye uhitaji mkubwa kwa wananchi wa visiwa vya Unguja na Pemba.
“Zanzibar mchele ndio kila kitu ni sawa na wenzetu Arabuni ukiadimika unga, kukosekana mkate kunakuwa na vurugu mitaani, hapa Zanzibar watu wetu tu Rahimu sana, lakini sasa hivi wamefikishwa pabaya sana, kilo elfu tatu mchele, kubwa, haijawahi kutokea, tujitahidi Ramadhani inakuja na hili ni ombi langu kwenu."
Ameeleza kuguswa kwake na bei ya awali ya mchele na kueleza hata kama isifikie ilikotoka kutokana na sababu mbalimbali za mabadiliko ya kiuchumi lakini isiwe kwa bei ya 3000 ambayo ni kubwa sana kwa wananchi.
Aliwashauri wafanyabiashara hao kushirikiana kuchukua meli kubwa zitakazobeba zaidi ya tani 30,000 badala ya kuchukua meli ndongo za tani 5,000 kwa nia ya kuwasaidia watu kuondokana na ugumu wa maisha uliopo, ikizingatiwa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani unakaribia.
Amewaeleza wafanyabiashara hao kuchukua meli kubwa kutapunguza utitiri wa meli ndogo zenye kubeba tani kidogo hali aliyoieleza kwamba inaongeza msongamano bandarini.
Kwa upande wao wafanyabiashara walieleza changamoto kubwa iliyosababisha bidhaa kupanda bei ni mkwamo wa utoaji mizigo bandarini pamoja na gharama kubwa za mizigo zinazotozwa bandarini.
“Mzigo wa lawama kwa tatizo hili najua wote unatupiwa serikali, wafanyabiashara tushirikiane kwa umoja wetu kupunguza hali hii, wananchi hawaelewi nini kinaendelea, lakini ukweli hasa bandari yetu imezidiwa sasa mahitaji yameongezeka, lazima kutumiwe njia mbadala ya kuwahisha mizigo, siku 30 nyingi sana mzigo kukaa bandarini,”amesema mfanyabiashara Bopar.