NA MWANDISHI WETU
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema, Kituo cha Huduma za Upandikizaji Mimba Kairuki Green IVF, Bunju jijini Dar es Salaam kitatatua changamoto ya Watanzania kwenda nje ya nchi kwa gharama kubwa kufuata huduma hizo.
Mheshimiwa Dkt.Mwinyi ameyabainisha hayo Februari 6, 2023 jijini Dar es Salaam katika uzinduzi wa Kituo cha Huduma za Upandikizaji Mimba Kairuki Green IVF, kilichopo Bunju jijini Dar es Salaam.
Amesema, katika kukabiliana na changamoto hiyo baadhi ya Watanzania wamekuwa wakilazimika kutafuta huduma za upandikiza mimba nje ya nchi na kwa gharama kubwa.
Dkt.Mwinyi ameeleza kuwa, ni dhahiri wananchi wachache tu wenye uwezo ndio wanaomudu, lakini walio wengi wanashindwa kupata huduma hizo.
Aidha, amesema tukio hilo ni muhimu na ni ushahidi wa dhamira na jitihada za taasisi hiyo za kuunga mkono jitihada za Serikali za kuimarisha huduma za afya zinazotolewa hapa Tanzania jambo ambalo lilikuwa harakati za Hayati Dkt Kairuki enzi za uhai wake.
Dkt.Mwinyi ameendelea kusema afya ya uzazi ni jambo ambalo Hayati Prof. Kairuki aliliwekea uzito mkubwa, huenda alifanya hivyo kutokana na changamoto inayowakabili kina mama wengi kutopata ujauzito.
"Nitoe shukrani za dhati kwako Mwenyekiti wa Taasisi ya Afya na Elimu mama Kairuki kwa kunialika kuja kujumuika nanyi katika tukio hili la ufunguzi wa kituo hiki cha Kairuki Green IVF na kumbukumbu ya mzee wetu Hayati Prof. Kairuki,"amesema.
Kwa upande wake Waziri wa Afya, Mhe.Ummy Mwalimu amesema kuwa, Serikali ipo tayari kushirikiana na sekta binafsi katika kuhakikisha wanatatua tatizo la ugumba nchini ili wananchi wapate huduma bora za matibabu hayo.
Waziri Ummy amesema ukubwa wa tatizo la ugumba nchini Tanzania linaanzia asilimia 30 na linafika mpaka asilimia 80.
“Natambua ukubwa wa tatizo hili na sisi wenyewe kama Serikali hatuna hata kituo kimoja cha kutoa huduma hizo,” ameeleza Mhe.Ummy.
Mhe. Ummy amesema Wizara ya Afya itaendelea kushirikiana na Kairuki Green IVF kuhakikisha kwamba wanawafikia Watanzania wengi ili kutoa huduma bora za matibabu na linapokuja suala la afya ni kipaumbele chao.
Waziri Ummy amempongeza Rais Dkt.Mwinyi kwa utendaji mzuri katika mapinduzi makubwa yanayofanyika kule Zanzibar katika upande wa afya na wanajivunia mafanikio hayo.
Pia amesema watahakikisha Serikali ya Awamu ya Sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan inaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi ili kuweza kutoa huduma za afya hususani afya ya mama na mtoto kwa ufanisi na ubora.