Rais Dkt.Mwinyi:Sayansi na teknolojia ya nyuklia ina manufaa makubwa ikitumiwa vizuri

NA DIRAMAKINI

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imesema ni jambo muhimu kwa Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) kusimamia na kudhibiti matumizi salama ya vyanzo vya mionzi nchini, ili vitoe mchango zaidi katika maendeleo ya Taifa.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akipiga makofi baada ya kuweka Jiwe la Msingi la Ofisi na Maabara ya Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania huko Dungu Zuze Wilaya ya Kati Unguja leo na kushoto kwa Rais ni Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja , Mhe.Rashid Hadidi Rashid.(Picha na Ikulu).

Hayo yamesemwa leo Februari 16, 2023 na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi alipoweka jiwe la msingi la ofisi na maabara ya tume hiyo kwa Zanzibar, huko Dunga Zuze Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja.

Dkt.Mwinyi amesema, Taifa linatumia teknolojia ya nyuklia katika nyanja mbalimbali na kueleza kuwa sayansi na teknolojia ya nyuklia ina manufaa makubwa ikitumiwa vizuri, itasaidia kuongeza kasi ya ukuaji wa sekta mbalimbali za uchumi ikiwemo kilimo, mifugo, nishati na afya.

Amesema, Zanzibar imepata mafaniko makubwa kutokana na kutumika kwa teknolojia ikiwemo kutokomeza wadudu aina ya mbung’o ambao walikuwa wakiathiri afya na uzalishaji wa mifugo hususani ng’ombe.
Alieleza, tume iliwezesha upatikanaji wa mbegu bora ya mpunga aina ya “SUPA BC”, yenye sifa ya kustahamili ukame na maradhi na kuongeza sasa mkulima anaweza kupata tani saba badala ya nne za awali kwa hekta moja.

Akizungumzia faida ya atomiki kwa sekta ya elimu, Rais Dkt.Mwinyi alieleza Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania imesaidia kuimarisha uwezo na utaalamu wa kudhibiti na kuongeza wigo wa matumizi ya teknolojia ya nyuklia nchini.

“Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania, inakamilisha utaratibu wa kufadhili vijana wa Kitanzania kwenda kusoma masuala ya Sayansi na Teknolojia ya Nyuklia katika vyuo bora duniani,”alieleza Dkt.Mwinyi.
Aidha, Rais Dkt.Mwinyi amewataka wadau na wafanyakazi wa Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania kujituma kwa bidii na maarifa ili kuleta mchango mkubwa kwa Taifa.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Naibu Waziri Elimu, Sayansi na Teknolojia wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Omar Juma Kipanga kwa niaba ya Waziri wa wizara hiyo, Prof. Adolf Mkenda alieleza mipango ya wizara hiyo kuongeza uwekezaji kwenye eneo hilo.

Alisema, Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Elimu imedhamiria kuongeza wataalamu zaidi kwenye eneo hilo na kuongeza kwamba tayari imekamilisha mitaala ya shahada tatu za uzamili kwenye Teknolojia ya nyuklia zitakazotolewa kupitia taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Afrika Nelson Mandela, Arusha
Akizungumzia ufadhili wa masomo kupitia mpango wa (Samia Scholarship) Naibu Waziri huyo, alieleza Serikali inawahamisisha vijana kubobea kwenye masomo ya sayansi ili kunufaika na fursa nyengine za ufadhili za ndani na nje ya nchi. Pia alieleza juhudi nyengine zinazochukuliwa na Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ni kuweka msukumo wa kutanua wigo wa matuizi ya sayansi na teknolojia ya nyuklia nchini.

Naye, Waziri wa Afya, Ahmed Nassor Mazrui amesema, sekta ya afya Zanzibar inafanya kazi kwa karibu na Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania, kutokana na miradi yake mingi kuhusisha mionzi.

Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) ilianzishwa chini ya Sheria ya Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania namba 7 ya mwaka 2003 kwa lengo la kusimamia na kudhibiti matumizi salama ya mionzi pamoja na kusimamia vyanzo vyote dhidi ya madhara yanayoweza kusababishwa na vyanzo hivyo. Pia ina jukumu la kuhamasisha na kuendeleza matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia nchini.
Ujenzi wa ofisi ya Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania kwa Zanzibar, utahusisha ofisi 27, maabara sita, kumbi tatu za mikutano, ukumbi mkubwa wenye uwezo wa kuchukua watu 100, jiko na sehemu ya kulia, ukumbi wa bodi, ukumbi mwingine wa mikutano wenye uwezo wa kuchukua watu 21 pamoja na eneo la walinzi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news