NA DIRAMAKINI
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameihakikishia Dunia kwamba Zanzibar ipo salama haina viashiria vyovyote vya kutishia amani kwa wenyeji na wageni watakaoitembelea.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akiwa katika ukumbi wa Jengo la Makumbusho Mnazi Mmoja “Baitul Amaan” Wilaya ya Mjini Unguja wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya Utalii na Uwekezaji Zanzibar, ukipigwa wimbo wa Taifa, na kushoto kwa Rais ni Mwenyekiti wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Bw. Rahim Bhaloo na Mke wa Rais wa Zanzibar,Mama Mariam Mwinyi na Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Mhe. Idrissa Mustafa Kitwana na (kulia kwa Rais) Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar, Mhe.Simai Mohammed Said, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dkt. Mohammed Said Mohammed (Dimwa). (Picha na Ikulu).
Dkt. Mwinyi ameyasema hayo alipofungua maonesho ya Utalii na Uwekezaji kwenye Ukumbi wa Makumbusho ya Beit el Aman, Mnazi Mmoja jijini Zanzibar.
Amesema, maonesho hayo yatatoa mchango mkubwa wa kukuza sekta ya utalii Zanzibar na kuwaomba wageni na watalii kutoa shaka kwa kutembelea visiwa vya Unguja na Pemba kuangalia mandhari nzuri na vivutio vya utalii vilivyomo.
Amesema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ziko imara kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa salama na yenye amani kwa wenyeji na wageni wanaoitembelea.
Dkt. Mwinyi aliitaka Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale kupitia Kamisheni ya Utalii kushirikiana na jumuiya za wafanyabiashara za utalii kujipanga upya na hatimaye kuja na mpango madhubuti wa kuzitumia fursa za biashara ya utalii zilizopo Zanzibar.
Pia aliishukuru sekta binafsi kwa kuendelea kutangaza utalii wa Zanzibar pamoja na kutoa huduma nzuri zinazosaidia kuitangaza Zanzibar na Tanzania kwa ujumla. Alisema ushirikiano wa pamoja unahitajika baina ya Serikali na sekta binafsi kwa kufanyakazi pamoja katika kuzitumia vyema fursa za biashara ya utalii zilizopo nchini.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akimkabidhi Cheti cha Shukrani Mwakilishi wa Shirika la Ndege la Qatar Airways, Bi.Pamela Sookhai, kwa mchango wao wakati wa hafla ya ufunguzi wa Maonesho ya Utalii na Uwekezaji Zanzibar, yanayofanyika katika viwanja vya Makumbusho Mnazi Mmoja "Baitul Amaan" Zanzibar Wilaya ya Mjini Unguja jijini Zanzibar.(Picha na Ikulu).
“Natoa pongezi na shukrani kwa Balozi zetu zote zilizo nje ya nchi kwa kufanya juhudi kubwa za kuvutia watalii kuja nchini,”amepongeza Rais Dkt.Mwinyi.
Akizungumzia utalii endelevu na umuhimu wa kutunza mazingira, Rais Dkt. Mwinyi alieleza maonesho hayo pia yanalenga maudhui ya Zanzibar ya kijani yenye kusadifu utalii endelevu wenye urithi tofauti wa kimaumbile, utamaduni na historia hai pamoja na kuonesha uwiano uliopo baina kutunza mazingira hai, uchumi, jamii na utamaduni ambao ni muhimu kwa maendeleo ya sekta ya utalii na uhifadhi wa mfumo wa ikolojia.
Hata hivyo, Dkt. Mwinyi
amewataka wageni waliopo nchini kufurahia ukarimu wa watu wa Zanzibar
pamoja na kuwataka kuwa mabalozi wazuri watakaporejea kwenye mataifa yao
kwa kueleza mambo mazuri waliyoyashuhudia Zanzibar.
Naye,
Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale.Mhe. Simai Mohammed Said aliwataka
wananchi wa Zanzibar kupenda kununua na kutumia bidhaa zinazozalishwa na
kutengenezwa nchini ili kuzifanya pesa kuendelee kuzunguruka na
kuongeza uzalishaji.
“Tukifanya hivyo thamani ya pesa itaendelea kubakia ndani itazunguruka kwa watu wetu, tuekeze sana na kutengeneza fedha nyingi ili kuboresha maisha ya watu kwaalili ya maisha mazuri kwao yatokanayo na faida ya utalii, Zanzibar,”amesema.
Akizungumzia miundombinu ya mawasiliano na barabara, Waziri Simai alieleza barabara nyingi za mji wa Zanzibar hazivutii kwa utalii, hivyo alizishauri mamkala husika kwa sasa waziboreshe na kupanda miti, bustani na maua mengi kwaajili ya kuwavutia wageni wanaofika nchini kwa uzuri na mvuto wa mwonekano wa kijani na maua hivyo aliwashauri Wakuu wa Mikoa na Wilaya pamoja nawadau wa Utalii kuishawishi jamii juu umuhimu wa kuzitunza na kuzienzi barabara na maeneo yote ili Zanzibar iboreke na kuwa na mvuto wa kipekee kwa watalii.
Waziri Simai alielekeza miti mingi ipandwe kwenye barabara kuu za miji, ambako watalii wengi hupita na kuona mandhari halisi ya mji wa Zanzibar.
Alimuahidi Rais Dkt.Mwinyi kwamba watashirikiana na taasisi nyengine za serikali zikiwemo Wizara ya utalii, usafirishaji na mawasiliano, Ardhi, Afya na wadau wengine wa utalii kufanya kazi kama timu moja ili kuungamkono jukudi za serikali kwenye kufikia lengo la utalii endelevu nchini na kufanikisha malengo ya utalii kwa ajili ya kizazi kijacho
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Rahim Baloo ameyataka mashirika ya ndege ya kimataifa kuunga mkono juhudi za Serikali kwa kuongeza safari za moja kwa moja kutoka mataifa makubwa kutua Zanzibar hali aliyoieleza itaifungua Zanzibar kwenye soko la kimataifa la utalii.
Amesema, maonesho hayo yataifungulia milango Zanzibar kwenye soko la kimataifa hadi kwa mataifa ya kusini na kaskazini mwa bara la Amerika. Maonesho hayo ya siku tatu yanatarajiwa kuhudhuriwa na zaidi ya washiriki 200 kutoka mataifa mbalimbali zikiwemo nchi za Algeria, Argentina, Brazil, Marekani na kwingineko.