Rais Dkt.Samia amekusudia kuwapa furaha wananchi kupitia Sekta ya Habari-Mwalimu Makuru

NA DIRAMAKINI

KADA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Musoma Mjini mkoani Mara, Mwalimu Makuru Lameck Joseph amesema, uamuzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan kutoa maelekezo ya maboresho ya sheria na kanuni ambazo zinaonekana kuwa kandamizi katika Sekta ya Habari nchini umedhamiria kuwapa furaha Watanzania.
Mwalimu Makuru ameyasema hayo katika mahojiano na DIRAMAKINI wakati akielezea namna ambavyo wadau mbalimbali wakiwemo wananchi wana shauku kubwa ya kuona maboresho hayo yanafanyika kwa ustawi bora wa jamii, tasnia ya habari na Taifa kwa ujumla.

"Kwa hiyo alichokifanya Mheshimwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ni kutaka kuwapa wananchi furaha, kuondoa chuki. Zingatia kuwa,kama mwananchi atashindwa kuongea kinachomsibu, vyombo vya habari vikashindwa kuwasilisha taarifa zinazomsibu kwa walengwa.

"Hii inajenga taswira tofauti na wakati mwingine huwa inaibua maswali yenye kujipa majibu ambayo yanaweza kuwa na ukweli au yakakosa ukweli.

"Vyombo huru vya habari ni kioo cha kuwasilisha yale ambayo wananchi wanasema, pengine wanafanyiwa mambo maovu au watu wanakiuka maadili, hivyo vyombo vya habari vikifanya kazi katika mazingira ya kubinywa maana yake wananchi watabakia kuumia moyoni na kama wakiumia watabakia kujenga chuki dhidi ya Serikali yao.

"Sasa Rais Dkt.Samia alichogundua ni kwamba, kama wananchi tukiwaacha katika hali hiyo pengine kushindwa kusema, maana yake nchi haiendelei kwa sababu mhimili wa kuongea kwa maana ya vyombo vya habari vinashindwa kuwajibika ipasavyo, kumbuka panapokosekana mawazo yenye kukosoa na kushauri pakasalia tu watu wa kusifia, Taifa haliwezi kustawi, ndiyo maana unapaswa kufahamu kuwa uhuru wa mawazo ukifa,Serikali nayo haitawajibika."

Mwalimu Makuru ameyasema hayo ikiwa, tangu aingie madarakani mwanzoni mwa mwaka 2021, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan aliudhirishia ulimwengu kuwa, tasnia ya habari ni muhimu kwa ustawi bora wa maendeleo ya jamii na Taifa.

Aidha, alianza kwa kuitaka Wizara ya Habari kuvifungulia vyombo vya habari vilivyofungiwa huko nyuma huku akisisitiza wahusika wafuate sheria, jambo ambalo lilifanyiwa kazi hatua kwa hatua.

Pia, alitaka kanuni ziweke wazi makosa na adhabu zake ili kusiwe na ubabe kwa kuwa Serikali inaamini katika uhuru wa vyombo vya habari nchini.

“Nasikia kuna vyombo vya habari mlivifungia, vifungulieni, lakini wafuate sheria na miongozo ya Serikali, wafungulieni tusiwape mdomo wa kusema tunaminya uhuru wa vyombo vya habari, na kanuni ziwe wazi tusifungie vyombo vya habari kibabe,” Rais Samia aliagiza Aprili, mwaka juzi katika hafla ya kuwaapisha makatibu na manaibu makatibu wakuu wa wizara mbalimbali Ikulu jijini Dar es Salaam.

Kwa sasa,Serikali inatarajiwa kuwasilisha Muswada wa Mabadiliko ya Sheria ya Huduma za Habari Na 12 ya 2016 katika vikao vya Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linaloendelea jijini Dodoma.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news